Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mavunde: Tutagawa mitambo kwa wachimbaji wadogo wa madini

MAVUNDEEEEEE Mavunde: Tutagawa mitambo kwa wachimbaji wadogo wa madini

Mon, 16 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amesema Serikali inakusudia kugawa mitambo kwa wachimbaji wadogo wa madini nchini ifikapo Oktoba 21 ili kuimarisha sekta hiyo.

Mavunde ameyasema hayo leo Jumapili Oktoba 15, 2023 wakati Rais Samia Suluhu Hassan aliposimamishwa na wananchi wa Sagala mkoani Singida.

“Mkoa wa Singida ni kati ya mikoa ambayo imebarikiwa ni yenye rasilimali madini ya kutosha na hapa kuna wachimbaji wadogo wengi, Rais umeshatupatia maelekezo tufanye utafiti ili wachimbaji wadogo wasichimbe kwa kubahatisha lakini pia tuwasaidie wapate mitaji na mitambo.

“Tupo tayari kufanya hivyo na tutaanza Oktoba 21 kugawa mitambo pale Dodoma kwa wachimbaji wadogo wakiwamo wa Mpipiti na Mpambaa,” amesema Mavunde.

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema tayari mitambo ya uchimbaji visima eneo la Singida imefanya kazi na maji yanapatikana kwa kushirikiana na wabunge wa eneo hilo.

Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amesema fedha zilizotolewa kwa wilaya ya Singida kwa miradi ya umwagiliaji ni zaidi ya Sh36 bilioni.

“Wakazi wa Singida hawana mito ya kudumu lakini wana mvua za muda na wana maporomoko na tumekubaliana tujenge mabwawa, hawa ndiyo wazalishaji wakubwa wa alizeti ambalo ni zao la uchumi na Serikali inaendelea na juhudi kulikuza zao hili,” amesema Bashe.

Waziri wa Ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi, Jerry Silaa amesema eneo la Sagala lilikuwa na mgogoro wa shamba la Halmashauri ya Singida, “Nichukue fursa hii kuwapongeza viongozi mgogoro huu umeshaisha, nilipita hapa Oktoba 4 wiki jana na nilifanya kikao na suala hili limekwisha.”

Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba amesema Serikali ya Rais Samia imekuwa ikitoa fedha nyingi na kuzielekeza kwenye maendeleo.

“Katika kipindi chako fedha nyingi zimekwenda kwenye maendeleo ya wananchi katika kipindi chote zilikuwa chini ya bilioni200 kwa sasa ni Trilioni 1 na elimu umeshapiga Trilioni 2 na afya tunazungumzia Trilioni 2 hivyo hivyo umeme ulikuta bwawa liko asilimia 37 na tumeshavuka tuko asilimia 90,” amesema Mwigulu

Chanzo: www.tanzaniaweb.live