Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mauzo ya nyama nje yaongezeka

Nyama Za Ng'ombe Mauzo ya nyama nje yaongezeka

Fri, 6 Jan 2023 Chanzo: Habarileo

MAUZO ya nyama nje ya nchi kwa kipindi cha Julai hadi Desemba 15 mwaka jana yalifikia tani 5,158.93 sawa na ongezeko la asilimia 21.7 ikilinganishwa na tani 4,239.42 zilizouzwa kipindi kama hicho mwaka 2021 huku nchi ya Qatar ikiongoza kwa kununua tani 504.

Msajili wa Bodi ya Nyama Tanzania (TMB), Dk Daniel Mushi alisema katika kipindi cha Novemba mwaka jana, Tanzania iliuza nje ya nchi tani za nyama 1,423 zenye thamani ya dola za Marekani 5,370,187.70 sawa na zaidi ya Sh bilioni 10 za Kitanzania.

Akizungumza hivi karibuni jijini hapa wakati akitoa tathmini ya maendeleo ya uuzaji nyama nje ya nchi kwa Novemba mwaka jana, Dk Mushi, alisema kiasi hicho kilichouzwa ni sawa na ongezeko la asilimia 125, ikilinganishwa na tani 632 zilizouzwa Oktoba 2022.

“Tani 1,423 za nyama zilizouzwa Novemba mwaka 2022, ni sawa na ongezeko la asilimia 62 ikilinganishwa na tani 878 zilizouzwa Novemba mwaka 2021, mpaka hapo zimeongezeka tani 545,” alisema Dk Mushi.

Alisema mchanganuo wa tani hizo 1,423 za nyama zilizouzwa ni ya mbuzi tani 1,047, kondoo tani 343, ng’ombe tani 32, kuku tani 0.67 na nyama ya nguruwe tani 0.2.

Meneja wa Idara ya Masoko TMB, John Chassama alisema zaidi ya nchi sita zimeshiriki kununua tani hizo ikiwamo Qatar iliyonunua tani 504, Oman (334), UAE (267), Saudi Arabia (125), Kuwait (56), Bahrain (50) na China tani 38.

Katika hatua nyingine, Chassama alieleza sababu za nyama ya mbuzi kuuzwa zaidi kuliko nyingine ni kutokana na mahitaji yake kuwa juu zaidi sokoni na upatikanaji wa mbuzi kama malighafi kwenye viwanda vya nyama ni rahisi ikilinganishwa na mifugo mingine.

Alitoa wito kwa vijana kutumia fursa ya kufuga kibiashara kwani soko la uhakika la mifugo lipo.

Alisema kwa namna kiwango cha nyama kinachouzwa nje inavyoendelea kukua, ndivyo mahitaji ya mifugo ambayo ni malighafi kwenye viwanda vya nyama inaongezeka.

Alisema ili kuendelea kuuza zaidi nyama nje ya nchi wananchi wanatakiwa kubadilika na kufuga kisasa kupata nyama iliyo bora na itakayoweza kushindana katika masoko ya kimataifa.

Mmoja wa wafugaji ambaye ni mfanyabiashara ya nyama jijini hapa, Emmanuel Stanley aliipongeza TMB, kwa kuwaunganisha na wafanyabiashara kutoka nje ya nchi hali inayowezesha wajikite zaidi katika ufugaji wa kisasa kutokana na uhakika wa soko.

Hata hivyo, aliiomba TMB kuendelea kutoa elimu kwa wafugaji na wafanyabiashara wa nyama juu ya namna bora ya ufugaji wa kisasa ambao gharama yake ni ndogo ukilinganisha na faida itakayopatikana baada ya kuvuna mifugo yake.

Chanzo: Habarileo