Mauzo ya nyama nje ya nchi yameongezeka kutoka tani 1,774 kwa mwaka 2020/2021 hadi kufikia tani 10,415 mwaka 2020/2022.
Msajili wa Bodi ya Nyama Tanzania (TMB), Dk Daniel Mushi amesema hayo leo Ijumaa, Oktoba 28, 2022 wakati akielezea utekelezaji wa majukumu ya bodi hiyo kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
Amesema mwaka 2018/2019, waliuza tani za nyama 1,759 wakati mwaka 2019/2020 waliuza tani 692.46.
“Kwa mwaka wa fedha uliopita tuliuza nyama nje ya nchi tani 10,415 ni kiasi ambacho hatujawahi kufikia kukiuza na hii imetupatia Sh96 bilioni,”amesema.
Amesema katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2022/2023 wameuza tani 3,256.60 za nyama nje ya nchi.
Amesema mkakati wao kwa mwaka 2022/2023 ni kuongeza kiasi cha nyama kinachouzwa nje ya nchi ambapo hadi sasa wanauza kwa kiasi kikubwa katika nchi za Mashariki ya Kati.
Amezitaja nchi zinazouzwa nyama kutoka Tanzania ni Qatar, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Bahrain, Kuwait, Oman, Comoro, Hong Kong, Jordan na Saudi Arabia.
Dk Mushi amesema lengo la bodi hiyo ni kuhakikisha kuwa wanaongeza uuzaji wa nyama nje ya nchi hadi kufikia tani 16,000 kila mwaka ifikapo mwaka 2026.
Aidha, amesema takwimu zinaonyesha bado Mtanzania mmoja anakula kilo 15 za nyama kwa mwaka badala ya kilo 50 zinazoshauriwa kitaalam.
“Watanzania wengi tunahitaji kuboresha afya zetu kwa kula nyama, kiasi ambacho kinachoruhusiwa na kupendekezwa,”amesema.