Mauzo ya bidhaa za Tanzania nje ya nchi yameongezeka kutoka Dola za Kimarekani bilioni 8 Machi, 2021 hadi Dola bilioni 12.2 kufikia Februari, 2023.
Akizungumza wakati wa kongamano la kuadhimisha miaka miwili ya Serikali ya Awamu ya Sita, Katibu Tawala Mkoa wa Geita profesa Godius Kahyarara ametaja bidhaa zinazoongoza kwa mauzo ya nje kuwa ni madini, kilimo, utalii na bidhaa za viwandani.
Peofesa Kahyarara ambaye pia ni mtaalam wa uchumi amewaambia washiriki wa kongamano hilo lililofanyika jana Jumapili Machi 5, 2023 kuwa ongezeko hilo ni matokeo ya utekelezaji wa Sera ya Diplomasia ya kiuchumi ilifofungua nchi tangu Rais Samia Suluhu Hassan ashike hatamu ya uongozi Machi 19, 2021 baada ya kifo Hayati John Magufuli kilichotokea Machi 17, 2021.
“Alipoingia madarakani, Rais Samia alifanya ziara katika Mataifa jirani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ikiwemo Kenya na Uganda; ziara zilizosaidia kuondoa vikwazo vya biashara na hatimaye tija kama takwimu zinazvyoonyesha kuwa Tanzania sasa ni kinara katika mauzo ya nje kwa nchi za EAC,” amesema Profesa Kahyarara
Ametaja faida nyingine ya kuondolewa vikwazo vya kibiashara kuwa ni kukua kwa sekta binafsi na kuvutia uwekezaji na mitaji kutoka ndani na nje ya nchi.
Amesema ndani ya kipindi hicho, mapato kupitia sekta ya utalii yameongezeka kutoka Dola za Kimarekani milioni 678 mwaka 2021 hadi kufikia Dola bilioni 2.4.
Amesema hata idadi ya watalii pia imeongezeka watalii 515, 000 wakati wa janga la Uviko-19 hadi kufikia zaidi ya watalii milioni 1.5; ongezeko analosema ni matokeo ya uamuzi wa Tanzania kuanza kuzingatia kanuni ya Kimataifa ya vita dhidi ya ugonjwa huo ikiwemo kuchanja.
“Tanzania tunafanya vema kwenye eneo la sekta ya kilimo siyo tu kwa kuongeza mauzo ya maua nje ya nchi, bali pia tunauza asilimia 65 ya mchele kwenye Mataifa ya Afrika Mashariki. Hii ni fursa ya kiuchumi kwa wakulima na Taifa kwa ujumla,” Profesa Kahyarara
Amesema uongozi wa Serikali mkoani Geita unatekeleza mikakati ya kuvutia uwekezaji kwenye sekta ya kilimo ili kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara katika hekta zaidi ya 100, 000 za ardhi inazofaa kwa kilimo mkoani humo.
“Endapo tutakuwa na uwekezaji wa kutosha, Mkoa wa Geita unaweza kuzalisha mpunga wa kutosheleza mahitaji ya nchi nzima na ziada ya kuuza nje,” amesema mtaalamu huyo wa uchumi
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigella amesema katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, mkoa huo umezalisha kilo 45, 221 za dhahabu zenye thamani ya Sh5. 053 trilioni, sawa na asilimia 60 ya mapato yote yaliyotokana na madini hayo nchini
“Uzalishaji huo uliofanywa na wachimbaji wadogo, wakati na wakubwa umeiwezesha Serikali kuingiza mapato ya zaidi ya Sh400 bilioni kuptia kodi na ushuru mbalimbali,” amesema Shigella
Akiunga mkono hoja ya kuondolewa vikwazo vya kibiashara na sera nzuri za uwekezaji zilizvyosaidia uchumi wa nchi kukua na kuongeza wawekezaji
Mbunge wa Geita, Constantine Kanyasu amewasihi viongozi, watendaji na watumishi wote wa umma kuunga mkono juhudi za Rais Samia kwa kusimamia vema utekelezaji wa mikakati na Sera ya kuvutia uwekezaji na mitaji kutoka ndani na nje ya nchi kupitia Diplomasia ya Kiuchumi.
“Kila mtu katika nafasi na eneo lake aondoe urasimu na vikwazo vyote kuvutia mitaji ya ndani na nje kuwezesha Tanzania kufikia lengo la kuwa na uchumi wa kati kupitia maendeleo ya sekta ya viwanda, hasa vile vya kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, uvuvi na ufugaji,” amesema Kanyasu