Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Matumizi ya gesi ya magari yashusha gharama za uendeshaji kampuni

Gesi Magari Tanzania Matumizi ya gesi ya magari yashusha gharama za uendeshaji kampuni

Fri, 31 Mar 2023 Chanzo: mwanachidigital

Kampuni ya Coca-Cola Tanzania imesema matumizi ya gesi katika moja ya gari lake la kusafirishia mizigo yamesaidia kupunguza asilimia 27 ya gharama za uendeshaji ikilinganishwa na walipokuwa wakitumia mafuta.

Hayo yameelezwa wakati kampuni hiyo ilipokuwa ikikabidhiwa gari yake ya kwanza inayotumia gesi pekee waliyoinunua kutoka Kampuni ya Magari ya Scania Tanzania.

Gari hiyo ambayo haitumii mfumo wowote wa mafuta kama ilivyo kwa magari mengine yanayotumia gesi, imekabidhiwa rasmi ikiwa ni baada ya kufanyiwa majaribio na Coca-Cola tangu mwaka 2021.

Akizungumza baada ya kufanya makabidhiano hayo, Haji Mzee ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Usafirishaji kutoka Kampuni ya Cocacola Tanzania amesema katika kipindi cha majaribio ya gari hiyo wamefanikiwa kupunguza gharama za uendeshaji kwa kiasi kikubwa.

Gari hiyo iliyo na mitungi nane ya gesi yenye uwezo wa kujaza Kg20 kila moja, inaweza kufanya safari zake kati ya Dar es Salaam hadi Morogoro na kurudi bila kuhitaji kujaza.

“Imepunguza gharama za matumizi kwa asilimia 27 katika kila safari tunatofanya. Matamanio yetu ni kuwa na magari mengi zaidi ya gesi,” amesema Mzee.

Amesema moja ya malengo yao ni kuhama kutoka matumizi ya mafuta kwenda katika gesi ikiwa miundombinu ya ujazaji gesi itaimarishwa nchini.

Eliavera Timoth ambaye ni Meneja wa Uendelezaji Biashara kutoka kampuni ya magari ya Scania Tanzania amesema gari hilo linaweza kutembea hadi kilimota 3 kwa kutumia Kg1 ya gesi.

Mbali na kutumia gesi asilia pia linaweza kutumia gesi itokanayo na takataka (biogas) katika kujiendesha.

“Gari hii haina mfumo wa mafuta kama magari mengine, inatumia gesi pekee hivyo kama wakifanya safari kwenda Dodoma ambapo hakuna kituo cha gesi na wakaishiwa wanaweza kujaza biogas na ikafanya kazi kama kawaida.

Amesema mbali na kutumia gesi, gari hiyo pia inatunza mazingira kwani inatoa moshi mweupe ambao hauna athari katika mazingira.

“Tunaweza kuleta gari nyingi zaidi kulingana na mahitaji ya wateja,” amesema Eliavera.

Chanzo: mwanachidigital