Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Matumizi mifuko ya plastiki mwisho leo

60663 Pic+mifuko

Fri, 31 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Leo ndiyo mwisho wa matumizi ya mifuko ya plastiki baada ya Serikali kuipiga marufuku kutokana na athari za mazingira.

Katazo la matumizi ya mifuko hiyo lilitolewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Jumanne ya Aprili 9, kwenye mkutano wa 15 wa Bunge jijini Dodoma wakati akihitimisha hoja ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, taasisi zake na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2019/2020.

Majaliwa aliiagiza Ofisi ya Waziri wa Nchi, Makamu wa Rais (Mazingira) iandae kanuni chini ya Sheria ya Mazingira ili kulifanya katazo hilo kuwa na nguvu ya kisheria.

Alisema hatua hiyo imechukuliwa ili kulinda afya ya jamii, wanyama, mazingira na miundombinu dhidi ya athari kubwa zinazotokana na taka za plastiki.

Hivyo kuanzia kesho, itakuwa ni kosa la jinai kutengeneza, kuagiza, kusambaza na kutumia mifuko ya plastiki nchini Tanzania na wote watakaokaidi watakuwa wamefanya kosa la kisheria.

Marufuku hiyo inahusisha maeneo yote ya Tanzania Bara. Kwa upande Zanzibar, marufuku hiyo inatekelezwa kwa miaka kadhaa sasa.

Pia Soma

Vifungashio vinavyoruhusiwa

Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ambayo imetungiwa kanuni za kupiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki mwaka 2019, inabainisha kuhusu vifungashio.

Sehemu ya 4 ya kanuni ya 9 inatoa ruhusa kwa vifungashio vya plastiki kutumika kwenye matumizi yafuatayo.

“Bila kuathiri masharti ya kanuni ya 5, vifungashio vya plastiki kwa ajili ya huduma za afya au bidhaa za viwandani au sekta ya ujenzi au sekta ya kilimo au vyakula au usafi na udhibiti wa taka havitahusika na zuio la kanuni hizi,” imeeleza sehemu ya kanuni hizo.

Sehemu ya sita ya kanuni hizo inajikita kwenye matumizi mbalimbali na inapiga marufuku mtu yeyote kuuza bidhaa kama vinywaji au nyinginezo zikiwa zimefungwa kwenye vifungashio vya plastiki ila kwa bidhaa zenye ulazima wa kutumia vifungashio hivyo.

Shehena zilizopo

Kwa wafanyabiashara watakaokuwa na shehena ya mifuko hiyo, juzi Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira, Januari Makamba alisema wataiuza kwa kampuni tatu zilizopewa jukumu hilo ambazo zitaigeuza kuwa malighafi.

Huko, alisema zitarejelezwa (recycle) na kutengenezwa bidhaa kuu mbili; mabomba na madawati.

Mwongozo wa Ukaguzi

Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Joseph Malongo ametoa mwongozo kwa wakaguzi na watekelezaji wa katazo la mifuko ya plastiki katika halmashauri zote nchini.

Ameeleza kuwa watafanya ukaguzi katika maduka, magenge, masoko, maduka makubwa, maghala, mipakani, viwandani na maeneo mengine yanayouzwa bidhaa.

“Hairuhusiwi kuingia kwenye makazi ya watu au kusimamisha magari au vyombo vingine vya usafiri kutafuta mifuko ya plastiki.

“Iwapo magari au vyombo vya usafiri vitasimamishwa kwa sababu nyinginezo na kukutwa shehena ya mifuko hiyo adhabu stahiki itatolewa kwa mujibu wa sheria na wahusika wataelekeza mahala mahsusi itakapopelekwa shehena hiyo,” alisema Malongo.

Malongo alieleza kuwa atakayekutwa na kosa la kuendelea kuhifadhi au kutumia mifuko hiyo, ataelekezwa kwa kuipeleka lakini atatozwa faini na endapo akishindwa kuilipa kwa muda aliopewa, atafunguliwa mashtaka.

Alisisitiza kuwa watakaotozwa na kulipa faini watapewa stakabadhi za Serikali kwa malipo hayo, huku akitaka busara itumike katika utekelezaji wa katazo hilo na kusisitiza kuwa matumizi ya nguvu, ikiwamo kuwapiga au kuwabeba na kuwaweka ndani watu hayaruhusiwi.

Aliwataka wakaguzi kujitambulisha wakati wote kwa kuonyesha vitambulisho vyao kwa wahusika kwenye maeneo wanayoyakagua na kwamba haitaruhusiwa kumsimamisha mtu na kupekua mizigo yake ili kutafuta mifuko ya plastiki.

Mifuko mbadala

Waziri Makamba alibainisha kuwa kuna viwanda 70 ambavyo vimejitokeza kutengeneza mifuko mbadala na kati ya hivyo, sita ni vikubwa na 30 vya kati.

Alisema umoja wa watengenezaji wa mifuko hiyo nchini umebainisha kuwa bidhaa zao zitakuwa zimeshaingia mtaani ifikapo kesho.

“Safari ya kuondoa mifuko ya plastiki hapa nchini lazima iwe kwa hatua, haiwezi kuwa kwa wakati mmoja, mnapiga marufuku kila kitu! Kwa hiyo tumeanza na mifuko ya plastiki, taratibu kadri miaka inavyoenda tutaenda hatua kwa hatua,” alisema Makamba.

“Wale waliokuwa na wasiwasi kwamba bidhaa za vyakula na nyingine zinazofungwa kutoka kiwandani kwamba zitapigwa marufuku hapana! kilichopigwa marufuku ni mifuko ya plastiki tu na wala siyo vifungashio.”

Makamba alieleza kuwa hatua ya kuondoa mifuko hiyo inakwenda sambamba na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kutumia mifuko mbadala na kuachana na plastiki kabisa.

Waziri huyo alitanabaisha kuwa marufuku hiyo itaibua uchumi mpya wa mifuko mbadala ambao utasaidia kuongeza fursa za ajira kwa vijana na kuchangia maendeleo ya Taifa.

Wilaya zilivyojipanga

Katika kikao cha kupanga mikakati ya utekelezaji wa katazo hilo kilichofanyika mkoani Dar es Salaam, mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema alisema hadi sasa wameanzisha vituo 15 kwa kukusanyia mifuko iliyotumika na isiyotumika ili kuwaondolea wananchi usumbufu wa kulipa faini kuanzia kesho.

Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Felix Lyaniva alisema njia mbalimbali zitatumika kuwaarifu wananchi kuhusu marufuku hiyo. Alisema kuna mabango sita yaliyosambazwa katika wilaya hiyo yakiwa na maelekezo ya kina.

Mwitikio mzuri

Waziri Makamba alisema mwitikio wa Watanzania kuachana na matumizi ya mifuko ya plastiki umekuwa mkubwa kwa zaidi ya asilimia 90 kutokana na taarifa anapata kutoka kwa maofisa wa Nemc waliosambazwa kwenye maeneo mbalimbali.

“Tutakuwa na changamoto ya mifuko mbadala katika mikoa ya Katavi na Kigoma ambayo kijografia ipo mbali, lakini tumeshazungumza na wazalishaji wa mifuko hii kuhakikisha bidhaa inafika. Jambo zuri wakazi wa mikoa hiyo wameonyesha utayari wa kutumia mifuko mbadala,” alisema Makamba.

Safari ya marufuku ilianza 2013

Agosti 2013, Serikali kupitia kwa aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Dk Terezya Huvisa ilitangaza kuwa imepiga marufuku uingizaji, utengenezaji, uuzaji, na utumiaji wa mifuko ya plastiki.

Zuio hilo lilihusu mifuko yote ya plastiki ya kubebea bidhaa kutoka madukani, sokoni na majumbani.

Hata hivyo, iliruhusu mifuko yenye unene wa maikroni 100 inayooza na vifungashio vya bidhaa mbalimbali kama vifaa vya hospitalini.

Serikali iliagiza ufanyike msako kukamata watakaokuwa wanaendelea kufanya biashara ya mifuko hiyo na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Mwaka juzi, waziri Makamba alisema Serikali imepiga marufuku moja kwa moja, utengenezaji, usambazaji, uingizaji na matumizi ya mifuko ya plastiki nchini kuanzia mwaka 2017, akisema kwamba hiyo ingehusu matumizi ya mifuko ya plastiki inayofungia pombe maarufu kwa jina la viroba.

Hata hivyo, utekelezaji wa agizo hilo ulifanyika katika vifungashio vya viroba.

Chanzo: mwananchi.co.tz