Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Matumaini mapya ya uzalishaji korosho Tanzania

Mwenyeji Korosho Matumaini mapya ya uzalishaji korosho Tanzania

Thu, 12 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Habari njema kwa watanzania baada ya Serikali kutangaza matumaini mapya ya kuongeza ushiriki katika mnyororo wa thamani pamoja na kukuza uzalishaji wa korosho nchini.

Kuhusu kukuza uzalishaji, Bodi ya Korosho Tanzania imesema tayari imefanikiwa kupanua wigo wa uzalishaji bada ya kuongeza idadi ya mikoa ya uzalishaji wa korosho kutoka mitano hadi 13.

Mikoa mitano mama ni Tanga, Lindi, Ruvuma, Mtwara na Pwani inayochangia asilimia zaidi ya 90 ya uzalishaji na mipya iliyoongezwa kwenye mpango ni Morogoro, Dodoma, SIngida, Njombe, Tabora, Katavi, Mbeya, Iringa inayochangia chini ya asilimia kumi ya kiwango kwa mwaka.

Akizungumza leo Oktoba 11, 2023 jijini Dar es Salaam wakati wa Kongamano la Kimataifa la Korosho, Mwenyekiti wa bodi hiyo Brigedia Jenerali Alyoce Mwanjile amesema matumaini ya uongezaji thamani yako katika kiwanda cha ubanguaji wa korosho cha Malanja Wilayani Nanyumbu, mkoani Mtwara.

Amesema kiwanda hicho kitakuwa na uwezo wa kubangua tani 100,000 kwa mwaka kuanzia Novemba mwaka 2024 hatua itakayopunguza korosho ghafi inayosafirishwa nje.

“Baada ya kuokota korosho, kiwanda kitaanza kufanya kazi Novemba. Kwa sasa tunasafirisha nje asilimia 90 ya korosho ghafi, lakini kiwanda kitapunguza asilimia 40 ya usafirishaji huo,” amesema Brigedia Jenerali Mwanjile akifafanua:

“Kuhusu hiyo mikoa iliyoongezeka , tayari tumeshapeleka mbengu kwa hiyo ni fursa mpya, sina takwimu lakini tunarajia uzalishaji utaongezeka kwa kiwango kikubwa kwa msimu ujao.”

Mamia ya washiriki wamejitokeza katika kongamano hilo lililokutanisha makundi ya wakulima, viongozi wa mikoa mitano husika katika uzalishaji wa korosho.

Kongamano hilo la siku mbili pia limehusisha watunga sera, sekta ya fedha, watafiti, mabalozi, wabunge, taasisi za Serikali na uwakilishi wa mataifa ya Bukinafaso, Ghana, India, Kenya, Uganda, Msumbiji, Zimbabwe, Nigeria, Afrika Kusini, Uholanzi, Hispania na Benini.

Agizo la Dk Mpango

Katika tukio hilo, Makamu wa Rais Tanzania, Dk Philip Mpango ametaja hatua nyingine mbili zitakazokuza matumaini hayo kupitia uhakika wa masoko na kutafuta ufumbuzi wa magonjwa.

“Ningependa kutoa wito kwa nchi za Afrika kujitahidi kupunguza bei ya mlaji wa korosho ili kukuza matumizi ya kitaifa na kikanda ya korosho na bidhaa nyingine zinazotokana na korosho kwa kuzingatia uwezo mkubwa wa soko wa Afrika wa takriban watu bilioni 1.4,”amesema Dk Mpango.

Dk Mpango ametumia jukwaa hilo kukaribisha wawekezaji katika sekta ya viwanda katika mnyororo wa thamani wa sekta hiyo huku akishauri wadau wa kongamano hilo kutafuta ufumbuzi wa magonjwa.

“Wakulima hawa wanahitaji msaada ili kukabiliana na wadudu na magonjwa yanayoathiri mavuno.Ni matumaini yangu kuwa mkutano huu, utajadili suala hili na kubadilishana mbinu bora za kuboresha huduma za ugani na utoaji wa pembejeo kwa wakati wakiangalia usajili wa wakulima wadogo.”

Hatua inafanyika wakati Serikai ikitarajia kukuza uzalishaji wa korosho kutoka wastani wa tani 220,000 zilizozalishwa miaka kumi iliyopita (2013/14-2022/23) hadi kufikia tani milioni moja mwaka 2030.

Aidha, katika msimu wa mwaka 2023/24 ,inatarajia kuvuna tani 400,000 na tani 700,000 ifikapo mwaka 2026/27 kabla ya kufikia kiwango hicho cha tani milioni moja.

Pia Serikali inakusudia kuongeza ajira katika mnyororo wa thamani, fedha za kigeni kutoka makadirio ya dola milioni saba mwaka jana hadi dola milioni 10.5 mwaka 2031. Pia asilimia 60 ya malighafi ya korosho hizo iweze kuzalisha bidhaa mbalimbali.

Msisitizo wa soko

Wakizungumza na gazeti hili kuhusu uzalishaji huo, baadhi wa viongozi wa halmashauri walishauri Serikali iongeze uhakika wa masoko ili kuakisi mwitikio wa wakulima.

Mwenyekiti wa halmashauri ya Wilaya ya Muheza, mkoani Tanga Erasto Muhina amesema matumaini mapya katika halmsahauri hiyo ni uwekezaji mpya.

“Mwitikio ni mkubwa. Mwaka 2021 tulizalisha tani 26, mwaka jana tani 30 na mwaka huu bado hatujafahamu lakini tumepata mwekezaji na tumempatia ekari 11,000 kwa hiyo misimu miwili ijayo pengine tunaweza kufikia tani 80, ajira na mapato yataongezeka,”amesema Muhina.

Mwenyekiti wa halmashauri ya Kilindi, mkoani Tanga Idrisa Mgasa amesema licha ya kupata tani mbili msimu wa mwaka jana, wanatarajia kuongeza hadi tani 15 kutokana na mwitikio wa wakulima.

Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde alisema Serikali itaendelea kutekeleza mikakati ya kukuza sekta hiyo ili iweze kuwa na mchango mkubwa kwenye uchumi wa Taifa huku Naibu waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile akiahidi kukamilisha agizo la kuboresha bandari ya Mtwara kwa ajili ya kusafirisha korosho nje.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo ba Mifugo, Mariam Ditopile Mzuzuri ameshauri Mpango wa Vijana BBT (kujenga kesho iliyo njema), iwafikie wakulima wa korosho pia nchini ili kukuza fursa.

Ukubwa wa sekta

Wakati Dk Mpango akielekeza kufikia asilimia 60 ya bidhaa zinazotokana na korosho ghafi, Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (Tari) Tawi la Naliendele, Dk Fortunus Kapinga amesema tayari wamefanikiwa kuzalisha zaidi ya bidhaa 23 kupitia aina 54 ya mbengu za mikorosho inayotumika.

Kwa mujibu wa taasisi hiyo, zaidi ya kaya 700,000 zinajiajiri katika sekta hiyo huku asilimia 95 ya shughuli zote za kujiajiri zikifanywa na wanawake.

“Kuna keki, siagi, juisi, kashata, lakini kwenye mabibo unaweza kuzalisha vinywaji mbalimbali, pia kuna nyama za mabibo watu hawajui,”amesema Brigedia Jenerali Mwanjile kuhusu sekta hiyo iliyochangia asilimia 15 ya fedha za kigeni mwaka jana.

Kwa mujibu wa Tari, asilimia 56 ya waliojiri sekta hiyo ndio wanatumia teknolojia mbalimbali katika eneo la ekari za mikorosho milioni 2.1 katika mikoa husika inayokadiriwa kuwa mikorosho milioni milioni 56.

Kuhusu uzalishaji, umeendelea kukua kutoka tani 0.3 mwaka 1945 hadi tani 236,000 mwaka 2020/21 kupitia matumizi ya mbunge hizo bora, matumizi ya kanuni za kilimo na udhibiti wa magonjwa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live