Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Matumaini mapya treni ya SGR safari za Dar-Moro

Tanzania SGR.png Matumaini mapya treni ya SGR safari za Dar-Moro

Thu, 14 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Miundombinu ya umeme kwa ajili ya uendeshaji wa Treni ya Kisasa (SGR) kati ya Morogoro hadi Dar es Salaam imekamilika kwa asilimia 100 huku kipande cha Morogoro hadi Dodoma kikiwa asilimia 99.

Kukamilika kwa miundombinu hiyo kunaweka matumaini ya kuanza kwa safari hizo zinazosubiriwa kwa muda mrefu sasa.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Danniel Sillo ndiye aliyetangaza kukamilika huko baada ya kamati yake kutembelea kituo cha kuzalisha umeme katika eneo la Kinyerezi jijini hapa.

Kamati hiyo pia ilitembelea na kufanya ukaguzi katika kituo cha kupoza umeme Morogoro Desemba 11, mwaka huu na kuridhishwa na kilichofanyika. Akizungumza baada ya kufanya ukaguzi, Sillo alisema kituo hicho kina uwezo wa kuzalisha KV220 huku mahitaji ya umeme kwa ajili ya uendeshaji wa treni hiyo ni KV25 pekee.

“Tumeona kipande cha kwanza kati ya Morogoro hadi Dar es Salaam kilichotumia Sh77.23 bilioni kimekamilika na kipande cha Morogoro hadi Dodoma kilichotumia Sh67.7 bilioni na kipo asilimia 99,” alisema Sillo.

Alisema kukamilika kwa miundombinu hiyo kunaweka matumaini ya kuanza kwa usafiri huo ambao umekuwa ukisubiriwa kwa hamu na Watanzania wengi. “Miundombinu imekamilika na kwa taarifa tuliyonayo ni kuwa wenzetu wa Shirika la Reli Tanzania wameshaanza majaribio ya treni hiyo ya kisasa kati ya Dar es Salaam hadi Morogoro,” alisema.

Licha ya kuridhishwa na mradi huo lakini waliitaka wizara kuangalia namna ya kuongeza uzalishaji wa gesi asilia ili iweze kutumika katika shughuli za kiuchumi hususani viwandani.

Akizungumzia kuongeza uzalishaji gesi, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Athumani Mbuttuka alisema tayari Serikali inao mpango kabambe kwa ajili ya kutekeleza agizo hilo.

Alisema utekelezaji agizo hilo utagusa visima vya uzalishaji gesi ikiwemo kile cha Songosongo huku akieleza kuwa ndani ya muda mfupi kati ya sasa hadi Aprili mwakani kutakuwa na ukarabati mkubwa kuhakikisha uzalishaji unafikia futi za ujazo milioni 30.

“Kwa upande wa Mnazi Bay kutachimbwa visima viwili na kufanya marekebisho mengine na hadi Desemba 2024 kutakuwa na futi za ujazo milioni 25 zinazozalishwa,” alisema Mbuttuka.

Alisema katika visima vya Mtoria na Madimba vitaunganishwa huku akieleza kuwa kufanya hivyo kutaongeza futi za ujazo milioni 40 hadi 60. “Tukiwa na uwezo wa kuongeza uzalishaji na hatua mbalimbali tunazozichukua, usafirishaji gesi kuja Dar es Salaam utaongezeka kwa kiasi kikubwa sana hii ikiwa na maana kuwa viwanda vyetu vinavyofanya uzalishaji vitanufaika,” alisema Mbuttuka.

Licha ya kuwa umeme unaotumika nchini kwa sasa ukitegemea asilimia zaidi ya 50 kutoka katika gesi alieleza kuwa pindi uzalishaji umeme katika Bwawa la Mwalimu Nyerere (JNHPP) utakapoanza Januari mwakani, utapunguza matumizi ya gesi katika kuzalisha umeme.

Mbali na kuongeza uzalishaji pia alieleza kuwa wamejipanga kuhakikisha gesi hiyo inafika maeneo tofauti ikiwemo majumbani.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga alisema asilimia 85 ya gesi inatumika kuzalisha umeme kwa sasa na wamepokea agizo la kamati la kutaka uwekezaji zaidi katika matumizi ya gesi ili kuchagiza uchumi wa Watanzania.

Alisema licha ya kuwekeza katika vituo vya kujaza gesi katika magari Serikali imejipanga kujenga vituo vingine vitatu vya kujaza gesi katika magari.

“Pia tumeingia ubia na kampuni binafsi ili waweze kusaidia katika ujenzi wa vituo hivyo jambo ambalo litasaidia kupunguza msongamano wa watu wanaotumia gesi katika magari vituoni na kuweka moyo kwa wengine kufunga mifumo hiyo,” alisema Kapinga.

Kapinga alisema wapo katika utekelezaji wa mkakati wa kufunga mifumo ya gesi katika taasisi zinazohudumia watu zaidi ya 100 ili ziweze kutumia nishati safi katika kupikia.

SGR Januari mwakani

Kukamilika kwa miundombinu hiyo kunatangazwa ikiwa ni siku chache tangu Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame

Waziri Mbarawa alieleza kuwa mwishoni mwa Januari, 2024 treni ya abiria ya Reli ya Kisasa (SGR) itaanza kutoa huduma kati va Dar es Salaam na Morogoro. Alitoa kauli hiyo, Desemba 6 mwaka huu katika kikao cha mawaziri saba wa Sekta ya Uchukuzi wa Umoja wa Ushoroba wa Kati (CCTTFA) kilichofanyika jijini Dar es Salaama Desemba 2, mwaka huu.

Kauli ya Profesa Mbarawa inakuja ikiwa ni baada ya kutolewa kwa ahadi mbalimbali kutoka kwa viongozi juu ya kuanza kwa majaribio hayo lakini hazikutekelezwa.

Profesa Mbarawa alisema huduma itaanza kutolewa kuanzia mwishoni mwa Januari, mwakani.

“Jambo la kufurahisha mwishoni mwa Januari, 2024 tutaanza rasmi kutumia usafiri wetu wa SGR kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro kwa ajili ya abiria si mizigo,” alisema Profesa Mbarawa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live