Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Matumaini kibao mnada wa kwanza wa chai ukifanyika Dar

Chai Melt Matumaini kibao mnada wa kwanza wa chai ukifanyika Dar

Mon, 13 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakati Tanzania ikianza kufanya mnada wa kwanza wa zao la chai katika jingo la Millennium Towers jijini hapa, matumaini makubwa yamekuwepo, ambapo tani 57 zinatarajiwa kuuzwa katika tukio hilo la kihistoria.

Mnada huo utakaofanyika kesho Novemba 13 kwa kupewa baraka na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Mweli, unatarajiwa kuongeza matumizi na shughuli zinazofanywa katika bandari za Dar es Salaam na Tanga pamoja na kuongeza uwazi katika biashara ya chai nchini.

Kwa muda mrefu minada ya chai imekuwa ikifanyika nchini Kenya, nchi mbayo pia ni mzalishaji mkubwa wa zao hilo barani Afrika.

Akizungumza leo Novemba 12 katika mahojiano na Mwananchi, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Chai, Mary Kipeja, amesema mnada wa huo utaifanya Tanzania kuwa kitovu cha biashara ya chai katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

“Licha ya kupunguza gharama, mnada huo utakuwa ni sehemu ya utekelezaji wa ajenda ya kuimarisha maudhui ya ndani (local content) na kuwawezesha Watanzania kiuchumi.

“Wadau katika mnyororo wa thamani wakiwemo wanunuzi, madalali, waendesha ghala na wasafirishaji watanufaika moja kwa moja na kuvutia wananchi wengi kushiriki katika kilimo cha chai,” amesema.

Amesema uanzishwaji wa mnada huo utapunguza gharama kwa asilimia 50, ikilinganishwa na kiasi kilichotumika kusafirisha bidhaa hiyo hadi Mombasa nchini Kenya kwa mauzo.

Amesema kupitia bandari za Dar es Salaam na Tanga zitakazotumika kusafirisha bidhaa iliyouzwa mandani, Serikali itaongeza mapato na kuzalisha ajira kwa wananchi.

“Tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa nyuma ya mpango huu na mapinduzi katika sekta ya kilimo kwa ujumla pamoja na Wizara ya Kilimo kwa kuhakikisha kuwa sekta ndogo ya chai inastawi nchini.

“Mnada wa chai unakwenda kubadili kipato cha wakulima wakubwa na wadogo na kuimarisha uzalishaji ya bidhaa hiyo nchini,” ameongeza.

Amesema wasindikaji 10 wametia saini mikataba ya kushirikiana na madalali, wengine saba wanaendelea na mazungumzo na kwamba wanunuzi tisa waliosajiliwa wanatarajiwa kushiriki katika minada ya zao hilo.

Akiwasilisha bajeti ya mwaka wa fedha wa 2023/24 Bungeni jijini Dodoma, Waziri wa Kilimo Hussein Bashe alibainisha kiasi cha chai kilichozalishwa nchini kwa tani na miaka ya uzalishaji kwenye mabano kuwa: 23,187 (2019/20); 24,077 (2020/21); 23,202 (2021/22) na 7,875 (2022/23).

Akizungumza Bungeni mwaka 2021, Waziri Bashe aliliambia Bunge kuwa wizara yake inamalizia maandalizi ya Mkakati wa Miaka 10 wa Sekta ya Chai (2021/22-2029/30) inayokusudia kuongeza kiasi na ubora wa chai inayozalishwa pamoja na kusimamia maendeleo ya tafiti zinazohusu zao hilo nchini.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live