Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Matendo ya NMB yagusa watendaji msingi,sekondari

Fbe6eddc7f9dbc236ef43bed640c653f Matendo ya NMB yagusa watendaji msingi,sekondari

Wed, 31 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

BAADHI ya walimu wakuu katika shule za sekondari na msingi Kanda ya Kaskazini wamevutiwa na utaratibu wa misaada wanaopata kutoka Benki ya NMB, kwa kuwa imekuwa na mguso kwenye maendeleo ya elimu nchini.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti walimu hao kutoka mkoa wa Tanga, Kilimanjaro na Arusha wameeleza namna misaada kutoka NMB ilivyofika kwa wakati na kuwa sehemu ya mabadiliko kwenye kujifunza na kuwasaidia wazazi jukumu la kupatikana madawati, madarasa na vifaa vya kufundishia.

NMB wamekuwa na mfuko maalumu ambao husaidia elimu, majanga na huduma za afya ambapo baada ya kukabidhi vifaa hivyo timu maalumu huzunguka kuangalia ikiwa walengwa wamefikiwa na misaada husika.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Msambiazi wilayani Korogwe, Mkoa wa Tanga, Selemani Kombo alisema shule yake ufaulu umeongezeka baada ya kupata msaada wa kumalizia darasa na ofisi ya walimu.

“Mngekuja miezi kadhaa kabla ya leo, mgeshuhudia maajabu sana, maana kwa kweli shule hii ilikuwa na hali mbaya kwa upande wa ofisi ya walimu, hata baadhi ya madarasa hayakuwa hivi mnavyoyaona,” alisema Mwalimu Kombo na kuongeza:

“Tulikuwa na kikao cha wazazi na viongozi wa shule, ndipo tulipopata taarifa kuwa Benki ya NMB inatoa misaada ya vifaa vya kuezekea na madawati, tukasema sisi shida yetu ni vifaa vya kuezekea. Asanteni sana tulipokea mabati na mbao za kuezekea, tunashukuru fedha ambazo tulipanga kuzitumia kuezeka tulizielekeza kwenye kupaka rangi na vifaa vingine hadi jengo likakamilika.”

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Semkiwa iliyopo Korogwe, Deborah Singu akizungumzia msaada wa viti 55 na meza zake, alisema msaada huo umewaonyesha namna wanafunzi wao walivyokuwa na kiu ya kukaa sehemu nzuri.

Mwalimu wa taaluma shuleni hapo, Mwalimu Bashir Abdu alisema kwa kiasi kikubwa shule yao ya Semkiwa imekuwa na mabadiliko makubwa kitaaluma baada ya wanafunzi kupata nafasi nzuri za kukaa madarasani.

“Awali hata utoro ulikuwa mkubwa, mwanafunzi akija akikosa sehemu ya kukaa anatafuta sababu ya kutoroka shule, kesho pia haji. Lakini viti hivi vimewapa hata hamu ya kusoma kwanza vinavutia hata kuvitazama tu. Kwa kweli NMB ahsanteni sana mmetukomboa,” alisema Mwalimu Abdu.

Meneja wa Benki ya NMB Tawi la Korogwe, Lugano Mwampeta alisema utaratibu wa kurudisha kiasi kidogo kinachopatikana kwenye faida ya benki hiyo inampa wepesi wa kupata wateja wengi, kwa kuwa namna jamii inavyoguswa na misaada hiyo huwajengea imani kuwa Benki ni NMB.

“Huwa tunapokea maombi mengi sana, hii inaonyesha ni kwa namna gani benki yetu inaaminiwa. Lakini pia hawa wanafunzi pamoja na walimu ni fursa nzuri si tu kibiashara bali hata kijamii kwa sababu sisi hatufanyi tu biashara lakini lazima tutoe huduma za kijamii kwa kuwa tunaishi nao,” alisema Mwampeta.

Aidha, kiasi cha zaidi ya Shilingi bilioni 2 kimetengwa kwa mwaka huu wa fedha kwa ajili ya kurudisha kwa jamii.

NMB ina matawi 225, zaidi ya mawakala 8,000 (NMB Wakala), ATM zaidi ya 800 nchi nzima na imefika katika kila wilaya. NMB ina wateja zaidi ya milioni tatu na wafanyakazi zaidi ya 3,400.

Chanzo: www.habarileo.co.tz