Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Matembele, ngogwe, fursa Mashariki ya Kati

62950f1b7af30b8e4448f01497eda82e Matembele, ngogwe, fursa Mashariki ya Kati

Mon, 14 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

WAFANYABIASHARA wakubwa na wa kati wameshauriwa kuchangamkia fursa ya kufanya biashara ya mboga za asili katika nchi za Mashariki ya Kati, kwani bidhaa hiyo ina mahitaji makubwa katika eneo hilo.

Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya kimataifa ya utafiti na uendelezaji wa mboga za asili za majani Kurugenzi ya Mashariki na Kusini mwa Afrika (World Vegetable Centre), Dk Gabriel Rugalema, alisema hayo wakati akizungumza na HabariLEO baada ya kufungua semina ya siku tano ya waandishi wa habari kutoka mikoa ya Arusha, Manyara na Dodoma.

Alisema serikali imetoa fursa kwa wafanyabiashara kufanya biashara katika nchi za Ulaya kwa kusafirisha bidhaa mbalimbali ikiwamo mboga mboga, matunda na maua.

Alitoa rai kwa wafanyabiashara wafanye biashara katika nchi za Mashariki ya Kati ambako mboga za asili ikiwamo ngogwe, mchicha, sukuma wiki, matembele, mnafu na bamia vinahitajika kwa wingi. Dk Rugalema alisema Kenya, Afrika Kusini na Ghana zinaingiza mapato mengi kwa kulima mboga za asili na kuziuza katika nchi za Ulaya na Mashariki ya Kati, lakini bado hazikidhi mahitaji ya soko.

“Tanzania ina ardhi kubwa inayofaa kwa kilimo cha mazao hayo, hivyo ni vema fursa hiyo ikatumika kuongeza mapato.”

“Wakati umefika kwa wafanyabiashara wakubwa na wa kati kufanya biashara ya mboga za asili katika nchi za Mashariki ya Kati kwa kuwa nchi hizo ziko jangwani na zinahitaji vyakula hivyo.”

“Natoa wito kwa wafanyabiashara kuuza ngogwe na mchicha katika nchi hizo kwani kuna soko kubwa,” Dk Rugalema.

Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wakulima wa Mbogamboga, Matunda na Maua Tanzania (Taha), Jackline Mkindi, alisema waandishi wa habari wana wajibu wa kuelimisha umma namna taasisi hiyo na na taasisi ya World Vegetable Center zinavyohimiza wakulima walime kilimo bora.

Alisema wakati wa ugonjwa wa covid-19 walifanya biashara kubwa kwa kusafirisha mboga mboga, matunda na maua katika nchi za Ulaya, lakini hawakuweza kukidhi mahitaji.

Alisema kilimo cha mboga za asili ni rahisi kwa kuwa ndani ya muda mfupi mkulima anaweza kuwa milionea na kuwahimiza wananchi walime ili wafanyabiashara wakubwa na wa kati wapate bidhaa za kupeleka nje ya nchi.

Chanzo: habarileo.co.tz