Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mataifa kujadili uhalali biashara ya Pembe za Ndovu

IMG 20220524 WA0009 Mataifa kujadili uhalali biashara ya Pembe za Ndovu

Tue, 24 May 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Serikali ya nchi ya Zimbabwe inaomba kuungwa mkono na Mataifa ili iweze kuruhusiwa kuuza tani 130 ya pembe za ndovu zilizokamatwa ndani ya mipaka yake katika matukio ya ujangili zenye thamani ya dola milioni 600.

Zimbabwe imetoa ombi hilo katika mkutano wa siku tatu unaoendelea jijini Harare ulioanza Jumatatu Mei 23, 2022 na kudai pembe hizo zipo katika Hifadhi ya Kitaifa ya Hwange ambayo ni mbuga kubwa ya wanyamapori iliyopo kusini magharibi mwa nchi hiyo.

“Kama hatutaruhusiwa kuuza tani zetu 130 za pembe za ndovu hii ina maana itatubidi  tuachane na mkataba wa Biashara ya Kimataifa katika Viumbe vilivyo Hatarini inayojulikana kama CITES,” alionya mjumbe wa Serikali ya Zimbabwe.

Hata hivyo jitihada za Zimbabwe za kutaka kuuza pembe hizo za ndovu zina utata kutokana na makundi mengi ya uhifadhi wa wanyama pori kupinga hoja hiyo yakisema uuzaji wowote wa pembe hizo ulio halali ama kificho unachochea ujangili.

“Kuhalalisha biashara ya pembe za ndovu ikiwemo kuidhinisha uuzaji mwingine huu ambao ni wa mara moja unaweza kuwa na matokeo mabaya vile vile,” amefafanua Vishal Singh mjumbe kutoka India.

“Hii itakuwa ni ishara hatari inayotoa mwanya wawindaji haramu na vikundi vya wahalifu kwamba tembo ni bidhaa na kwamba biashara ya pembe za ndovu sasa inaweza kuanzishwa tena na kuongeza tishio kwa wanyamapori,” akasisitiza mjumbe wa muungano wa mashirika 50 ya haki za wanyamapori.

Nchi za Kusini mwa Afrika zimewahi ruhusiwa mara mbili kuuza akiba yao ya pembe za ndovu kwa Japan na Uchina mwaka 1997 na 2008 na mauzo hayo yalisababisha kuongezeka kwa kasi kwa ujangili katika bara zima la Afrika.

Hata hivyo Zimbabwe inasema idadi ya tembo imepanda kwa kasi kati ya asilimia 5 hadi asilimia 8 kwa mwaka kiwango ambacho si endelevu na kwamba inahitaji fedha za mauzo ya pembe hizo ili zisaidie udhibiti wa idadi ya tembo wake ambayo imeongezeka mara dufu.

“Nchi ya Botswana ndiyo inayotajwa kuwa na idadi kubwa ya tembo Duniani ikiwa na zaidi ya tembo 130,000 na kwa pamoja sisi (Zimbabwe) na Botswana tuna karibu asilimia 50 ya tembo duniani tunachotaka ni kukabiliana na idadi inayoongezeka ila hatuna fedha kwanini msiruhusu,” alihoji mjumbe wa Zimbabwe.

Zimbabwe na Botswana zinasema hazina vifaa vya kutosha kukabiliana na wawindaji haramu bila pesa za mauzo ya pembe za ndovu kutokana na mapato ya utalii kupungua kufuatia vikwazo vya usafiri vinavyohusiana na ugonjwa wa covid 19 tangu mwaka 2020.

Katika ushawishi wake mpema juma lililopita wajumbe kutoka baadhi ya nchi za Umoja wa Ulaya wakiwepo Uingereza, Marekani na Canada waliongozwa kupitia vyumba vyenye ulinzi mkali jijini Harare ambavyo vimejaa malundo ya meno ya tembo ili kupata uungwaji mkono wa kimataifa kwa uuzaji halali wa pembe hizo.

Lakini upinzani mwingine unatoka Kenya na wanachama wengine wa Muungano wa Tembo wa Afrika ambao wanachama wake 32 wengi wao kutoka nchi za Afrika Mashariki na Magharibi zenye tembo wachache wanasema kufungua tena biashara halali ya kimataifa ya pembe za ndovu hata kwa mnada mmoja kutaongeza ujangili.

Awali mwaka 1989 CITES ilipiga marufuku biashara ya kimataifa ya pembe za ndovu ili kupunguza ujangili na baadae mwaka 2019 iliweka vikwazo kwa uuzaji wa tembo mwitu waliokamatwa Zimbabwe na Botswana hatua ambayo iliwafurahisha baadhi ya wahifadhi na kuwasikitisha maafisa waliosimamia mbuga zilizojaa.

Mkutano huo umehudhuriwa na wawakilishi kutoka nchi 16 za barani Afrika, nchi za Japan na Uchina, watumiaji wakuu wa pembe za ndovu, wadau wa wanyama pori na Viongozi wa sekta ya Utalii kutoka Mataifa mbalimbali na unatarajiwa kumalizika hapo kesho Jumatano Mei 25, 2022.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live