WAZIRI wa Madini, Dk Doto Biteko amesema masoko ya madini yameingiza Sh trilioni 1.68 kutokana na mauzo ya madini katika masoko hayo kuanzia Julai mwaka jana hadi mwezi uliopita.
Dk Biteko alisema hayo bungeni Dodoma jana wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2023/2024 na aliliomba Bunge lijadili na kumuidhinishia bajeti ya Sh bilioni 89.4.
Alisema wizara hiyo imeimarisha usimamizi na ukaguzi kwenye maeneo ya uchimbaji, mipaka ya nchi, viwanja vya ndege, bandari pamoja na kuanzisha na kuimarisha masoko na vituo vya ununuzi wa madini.
“Hadi kufikia mwezi Machi mwaka huu, jumla ya masoko 42 na vituo vya ununuzi wa madini 93 vimeanzishwa, mauzo katika masoko na vituo vya ununuzi yamefikia shilingi trilioni 1.68 kuanzia mwezi Julai mwaka jana hadi mwezi Machi mwaka huu,” alisema Dk Biteko.
Alisema uwepo wa masoko na vituo hivyo umechangia kwa kiasi kikubwa ukusanyaji wa maduhuli ya serikali.
Aidha, alisema serikali imeendelea kuhamasisha uwekezaji katika sekta ya madini ili kuongeza mchango wa sekta hiyo kwenye Pato la Taifa.
Alisema kuanzia Julai mwaka jana hadi Machi mwaka huu, wizara hiyo kupitia Tume ya Madini ilitoa leseni kubwa ya uchimbaji wa madini ya kinywe kwa Kampuni ya Faru Graphite Corporation Limited (FGCL) na leseni ya uchimbaji wa kati wa madini ya tanzanite kwa Kampuni ya Franone Mining Limited kwa ajili ya kuendeleza Kitalu “C” Mirerani.
Kutokana na uhamasishaji uliofanyika katika sekta hiyo, alisema leseni 6,381 zilitolewa katika utafutaji, uchimbaji, biashara na uongezaji thamani madini kati ya leseni 6,116 zilizopangwa kutolewa katika kipindi husika.