Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mashirika ya Posta kuboresha Biashara Kenya, Tanzania

E94508d514b1d7be9da715bbaa51b142.jpeg Mashirika ya Posta kuboresha Biashara Kenya, Tanzania

Fri, 17 Dec 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Serikali imesema ushirikiano baina ya Shirika la Posta la Tanzania na lile la Kenya utasaidia kuboresha biashara kati ya nchi hizo mbili.

Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk Zainab Chaula amesema Ijumaa jijini Dar es Salaam baada ya kupokea ugeni wa Shirika la Posta Kenya na kuyapongeza mashirika yote mawili kwa kuimarisha mahusiano yenye tija.

"Ushirikiano huu unaenda kuboresha sekta ya biashara kati ya Kenya na Tanzania na Mashirika haya Posta yatumike kama kitivo cha biashara na zilete fursa kwa wafanyabiashara wa pande zote mbili, "amesema Dkt. Chaula.

Ugeni wa Shirika la Posta Kenya uliongozwa na Postamasta Mkuu, Dan Kagwe aliyeambatana na Milka Mugwe, Meneja Uendeshaji na Huduma kwa Wateja pamoja na Joel Mageto, Meneja wa Miradi Maalum na Katibu katika Ofisi ya Postamasta Mkuu wa Shirika hilo.

Dkt. Chaula ametaka Mashirika ya Posta yafungue milango ya biashara kwa wananchi ili kuleta wepesi wa upatikanaji wa huduma stahiki kwa wananchi kulingana na mahitaji yao.

Aidha, amelitaka Shirika la Posta nchini kwa kushirikiana na Posta zingine Afrika na kuendelea kukipa kipaumbele Kiswahili kwa lengo la kukuza na kutumika kama fursa kwa wafanyabiashara ili kuleta tija kwa Taifa.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dk. Jim Yonazi amesema ni vema kujifunza kwa kushirikiana na wanapotoka nje ya Afrika Mashariki kuwa wamoja ili kuleta manufaa ya kuwa pamoja.

Ameongeza kuwa, zinapotokea fursa wanapaswa kwenda kama Washirika kutoka Afrika Mashariki na kuendelea kusisitiza taasisi hizi kuona umuhimu wa kuendelea kufanya tafiti ili kuleta maendeleo kwani tafiti zitawasaidia kuongeza maarifa, uelewa na kuongeza ubunifu katika kuhudumia wananchi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Dk. Jabiri Bakari amemshukuru Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Kenya Bw. Dan Kagwe kwa kuja kutembelea Tanzania na kujionea maboresho yanayoendelea kufanywa na Shirika la Posta Tanzania.

Kaimu Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania Macrice Daniel Mbodo, ameeleza mikakati ya Shirika la Posta nchini katika kukuza mahusiano kati yake na Posta nyingine Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla, lengo ikiwa ni kurahisisha huduma za kiposta Barani Afrika.

Bw. Mbodo amesema, kuwa sasa Posta ni zaidi ya barua kwani Shirika linaendelea kuboresha huduma zake na kuzitanua zaidi ili kuwafikia wananchi wengi zaidi na kuwa Posta ya mfano katika Bara la Afrika

Kaimu Postamasta Mkuu ameongeza kuwa kutokana na maboresho makubwa yanayoendelea kufanyika katika Shirika la Posta nchini, wanatarajia kupokea ugeni kutoka nchi mbalimbalimba za Afrika ikiwemo Kongo Brazzaville, Zimbabwe, Oman na nchi zingine za Afrika.

Kwa upande wake, Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Kenya Bw. Dan Kagwe ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa mapokezi makubwa na ushirikiano mkubwa aliopata katika ziara yake ya kujifunza na kubadilishana uzoefu katika Shirika la Posta Tanzania

Vilevile, Bw. Kagwe ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuendelea kuboresha na kuimarisha Sekta ya Posta nchini ili kuhakikisha linatoa huduma stahiki kwa wananchi na kwa kutumia mifumo ya kidijitali inayofanya wananchi wengi wanahudumiwa kwa wakati mmoja

Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Kenya Bw. Kagwe ametoa mwaliko kwa Viongozi wa Shirika na Wizara kutembelea Kenya ili kuendelea kujenga mahusiano na kubadilishana uzoefu ili kuhudumia jamii zetu.

Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Zainab Chaula amekabidhi zawadi kwa Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Kenya Bw. Dan Kagwe pamoja na maafisa waandamizi walioongozana naye.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live