Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mashine za kuchakata mbao  zinavyonyanyua vijiji kipamato

A469523fc56367e4ed5f3086fee5d371 Mashine za kuchakata mbao  zinavyonyanyua vijiji kipamato

Tue, 27 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

TAKWIMU zinazotokana na tathimini ya rasilimali za misitu ya mwaka 2015 zinaonyesha kuwa Lindi ni mkoa wa pili kwa kuwa na misitu mingi iliyohifadhiwa kisheria, nyuma ya Katavi.

Ina hekta 959,648 za misitu, kati ya hiyo misitu ya hifadhi ya taifa hekta 370,504, misitu ya vijiji hekta 330,364 na misitu ya mikoko hekta 44,038, sehemu kubwa ya misitu hiyo iko wilaya ya Kilwa.

Akizungumza wakati wa kukabidhi mashine ya kuchakata magogo kwa vijiji 18 vya wilaya za Ruangwa na Nachingwea mkoani Lindi, katibu tawala wa mkoa, Bora Haule, anasema licha ya misitu hiyo kutumika kwa ajili ya uvunaji endelevu, inatoa pia fursa za utalii.

Haule anasema Lindi ina vivutio vingine ikiwemo hifadhi ya taifa ya Mwalimu Nyerere na Pori la akiba la Selous pamoja na maeneo ya Kale ya Kihistoria, fukwe na viumbe hai mbalimbali bila kusahau mjusi mkubwa aliyekuwepo huko Kale.

Anasema licha ya kuwa na vivutio vingi vya utalii, mkoa haujanufaika sana na vivutio hivyo na ndipo anamuomba Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Damas Ndumbaro, kuwa balozi katika kutangaza vivutio vilivyopo kanda ya Kusini inayojumuisha mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma.

Mkuu wa wilaya ya Lindi, Shaibu Ndemanga, anaishurukuru wizara kwa jitihada zake kwa kuwezesha misitu ya vijiji kunufaisha wananchi kwa kuitangaza kwenye gazeti la serikali lakini anaahidi kukaa imara katika kuilinda.

“Tunatakiwa kubadilika badala ya kuvuna magogo holela kwenye misitu, tuone namna ya kuyachakata na kuweza kuyaongezea thamani na hivyo kunufaika zaidi na misitu yetu.

“Kuna vijiji vina uwezo wa kununua mashine za kuongezea thamani magogo vyenyewe kama vitaweka hilo kwenye mipango yao ya vijiji,” anasema mkuu huyo wa wilaya.

Anasema wamejipanga kupanda miti ya asili iliyopo hatarini kutoweka kwa kushirikiana na Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) kwa kushirikiana na asasi ya Mpingo Conservation and Development Intiatives (MCDI), vijiji na wadau wengine.

Anasema wametenga maeneo makubwa ya mashamba ya miti ya asili ikiwemo mipingo kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Ndemanga anasema Lindi kuna maeneo yanayoitwa Mipingo kutokana na uwepo wa miti hiyo kwa wingi lakini sifa hiyo inatoweka kutokana na uvunaji usioendelevu wa misitu ya asili ikiwemo uchomaji moto misitu.

Anasema wameotesha kitalu cha mipingo katika msitu wa hifadhi wa Rondo chenye miche zaidi ya 100,000 itakayopandwa kwenye shamba la zaidi ya hekta 15 na miche mingine kugawawiwa kwenye shule za msingi, sekondari, taasisi za serikali, binafsi na wananchi.

“Tumekubaliana kwamba kila shule ya msingi na sekondari watatakiwa kuwa na shamba lenye ukubwa wa ekari kati ya tatu hadi nne za miti ya mipingo na kuhamasisha jamii kutochoma miti na misitu ovyo,” anasema Ndemanga.

Kilwa ni moja ya wilaya iliyopatiwa mashine ya kuchakata magogo mwaka 2017 kupitia Mradi wa Kuongeza Mnyororo wa Thamani wa Mazao ya Misitu (FORVAC) unaotekelezwa na Wizara ya Maliasili na Utalii, chini ya Idara ya Misitu na Nyuki.

Mkuu wa wilaya hiyo, Chrisptopher Ngubiagai anasema vijiji 11 vya wilaya hiyo viliwezeshwa MCDI kumiliki mashine za kisasa za kuchakata magogo aina ya NoRwood Lumber Pro HD 36.

Anasema kijiji cha Ngea ni cha kwanza kufanya uchakataji wa magogo kwa kutumia mashine hiyo ya kisasa inayopasua mbao nyingi kwa kiwango cha kimataifa na kwamba kiliuza mbao zenye thamani ya shilingi milioni 34 na ushei lakini kama wangeuza magogo badala ya mbao, wangeishia kupata shilingi milioni 26 pekee.

Anasema kijiji cha Liwiti pia kiliweza kuchakata mita za ujazo 154 za mti na kujipatia shilingi mlioni 67.7 lakini kingeuza magogo kingeambulia shilingi milioni 40 tu.

Ngubiagai anasema kutokana na fedha hizo kijiji cha Liwiti kimejenga nyumba ya mwalimu, zahanati ya kijiji, kuchangia chakula kwa wanafunzi wanaosoma shule za msingi na sekondari, kuchangia sare za shule kwa wanafunzi waliojiunga kidato cha kwanza mwaka 2019 na 2010. Pia pesa hizo zilichangia ununuzi wa madawati na viti kwa shule ya sekondari.

Anendelea kueleza kwamba katika mlolongo huo kijiji cha Likawage kilijipatia shilingi milioni 121 badala ya shilingi milioni 43.4 kama kingeuza magogo.

Anasema fedha hizo wameweza kufanyia shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwemo ujenzi wa kisima cha maji ya kunywa, kuchangia madawati ya shule ya msingi, ukarabati madarasa matatu, kuchangia vitanda kwa shule ya sekondari na ujenzi wa darasa moja katika kijiji kidogo cha Nanjumba.

Anasema usimamizi shirikishi wa vijiji ni njia mojawapo ya kuchangia maendeleo ya jamii na pato la Taifa na kwamba hii inatokana na kuwa na sera na sheria nzuri za nchi zinazotoa mamlaka kwa wanavijiji kusimamia misitu yao.

Meneja wa TFS kanda ya Kusini, Manyise Mpokigwa, anasema wameanzisha mpango wa kukabiliana na upotevu wa miti ya asili ikiwemo mipingo, mikongo, mininga, mivule na kisekeseke ambayo wamebaini katika kanda hiyo ipo hatarini kutoweka kutokana kuvunwa kwa njia ambayo siyo endelevu.

Anasema kwa mwaka uliopita jumla ya miti milioni 3.0 ya asili ilipandwa na TFS, Kanda ya Kusini.

Mratibu taifa wa mradi wa FORVAC, Emanuel Msoffe anasema mradi huo unaotekelezwa katika wilaya 12 nchini kwa ufadhili wa serikali ya Finland. Anaahidi kwamba katika bajeti ijayo wataangalia uwezekano wa kuongeza mashine ili ikiwezekana kila wilaya kuwa na mashine yake hasa zenye uhitaji mkubwa badala ya wilaya mbili au zaidi kuchangia mashije moja.

Akikabidhi mashine ya kuchakata magogo kwa vijiji 18 vya wilaya ya Nachingwea na Ruangwa mkoani Lindi, Waziri Ndumbaro alisema serikali kwa kuwapenda wananchi wake ndiyo maana wakaona umuhimu wa kuingia makubaliano na serikali ya Finland kuhusu mradi wa FORVAC.

Anasema mashine wanazopewa wanakajiji zina uwezo mkubwa wa kuchakata magogo kwa kuwa za zamani zilikuwa na uwezo wa kuchakata magogo kwa asilimia 30 tu lakini za sasa zinaweza kuchakata magogo kwa asilimia 60 na hivyo kuongeza mapato kutokana na ubora wa mbao zinazopatikana.

Anawasisitizia wanavijiji 18 waliopatiwa mashine hiyo kuitumia vizuri katika kuongeza mnyororo wa thamani wa mazao ya misitu na kuachana na migogoro ambayo inaweza kukwamisha mipango yao.

Anaziagiza halmashauri zote za Lindi kununua mbao kwenye vijiji hivyo 18 ili kuviwezesha kununua mashine zingine na kuufanya uchakataji wa mbao uwe rahisi zaidi.

Anautaka pia mkoa wa Lindi kuuangalia kwa jicho la pekee msitu wa Hifadhi wa Rondo kutokana na msitu huo kuwa moja ya misitu 20 bora duniani.

Dk Ndumbaro anasema wizara ina mpango wa kuendesha utalii wa kiikolojia katika misitu na kwa mantiki hiyo inapanga kujenga hoteli ya kitalii kwenye msitu huo wa Rondo.

Anasema Mkoa wa Lindi, na hususani katika wilaya ya Kilwa, mtu anaweza kufanya utalii wa malikale, utalii wa kihistoria, utalii wa picha, utalii wa bahari na fukwe, uwindaji wanyamapori na utalii wa kiikolojia na kwamba hakuna eneo lolote nchini lililosheheni aina nyingi za utalii kama Lindi.

Chanzo: www.habarileo.co.tz