Jumla ya mashine 24 za michezo za bahati nasibu zenye thamani ya zaidi ya Tsh. Milioni 36 zimevunjwa na Bodi ya Michezo ya Bahati Nasibu Mkoani Kigoma baada ya msako ulifanywa na Bodi hiyo ikishirikiana na Polisi.
Bodi imefikia hatua ya kuharibu mashine hizo kutokana na ukiukwaji wa sheria ya michezo ya bahati nasibu ya mwaka 2003 kifungu namba 4 na Wamiliki kushindwa kujitokeza ndani ya siku 7 ili kueleza sababu za wao kuweka mashine katika maeneo yasiyoruhusiwa.
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Michezo ya Bahati Nasibu, James Mbalwe amesema mashine zilizokamatwa zimekutwa katika maeneo yasiyostahili kuwepo mchezo huo na kwamba ni kosa kisheria kuendesha biashara hiyo bila kusajiliwa.”
“Sheria inayosimamia michezo ya kubahatisha inasema tukikamata mshine tukamate na kilichokua kwenye mashine, tumepata Tsh. Milioni 2.5 kwenye mashine hizi, Wamiliki wametoroka na tunaendelea kuwasaka pindi tutakapowapata tutawafikisha Mahakamani na hatua za kisheria zitachukuliwa”.
Mkurugenzi ametaja maeneo yasiyoruhusiwa kuwa na mchezo huo kuwa ni pamoja na Shuleni, kwenye nyumba za Ibada, karibu na majengo ya Hospitali, karibu na makazi ya Watu pamoja na maeneo ya Usalama wa Taifa na kwamba mpaka sasa Bodi imesajili mashine 17,000.