Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Masahihisho:Wafadhili watoa asilimia 69 ya matarajio

46542 Pic+masahihisho Masahihisho:Wafadhili watoa asilimia 69 ya matarajio

Wed, 13 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imesema kwa kipindi cha Julai mwaka jana hadi Januari 2019 imepokea Sh1.03 trilioni kutoka kwa wadau wa maendeleo zilizotolewa kama msaada na mkopo. 

Kiwango hicho ni sawa na asilimia 69 ya Sh1.48 trilioni ambazo ziliahidiwa na washirika hao wa maendeleo kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo katika kipindi cha miezi saba kati ya Julai 2018 na Januari 2019. Mtandao wa Mwananchi uliandika kimakosa kuwa asilimia hizo ni 6.7.

Hayo yamesemwa jana Jumanne, Machi 12, 2019 na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango wakati akiwasilisha mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na Ukomo wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2019/2020.

“Kati ya kiasi kilichotolewa, misaada na mikopo nafuu ya Kibajeti ilikuwa Sh125.4 bilioni na miradi ya maendeleo Sh782.0 bilioni. Mifuko ya Kisekta ilipokea Sh127.4 bilioni,” alisema.

Katika mwaka huo wa fedha Serikali ilitenga Sh12 trilioni kwa ajili ya miradi ya maendeleo zikijumuisha Sh9.8 trilioni ambazo ni fedha za ndani na Sh2.1 trilioni za nje.

Dk Mpango alisema Sh2.7 trilioni zilitolewa na Serikali kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo hadi kufikia Januari 2019.

Waziri huyo alisema Sh3.8 trilioni zilitumika kulipa mikopo iliyotumika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo. 

“Serikali imeshatenga na inatarajia kutoa kiasi cha Sh1.4trilioni kwa ajili ya kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo ukiwemo wa kufua umeme kwa kutumia nguvu ya maji ya Mto Rufiji (MW2,115),” alisema.

Aidha katika bajeti ya Mwaka 2018/2019 Washirika wa Maendeleo wanatarajiwa kuchangia Sh2.68 trilioni ambayo ni asilimia 8.2 ya bajeti yote (Sh32.48 trilioni). 

Misaada na mikopo hii inajumuisha misaada na mikopo nafuu ya miradi ya maendeleo Sh2.0 trilioni, mifuko ya pamoja ya kisekta Sh125.9 bilioni na misaada na mikopo nafuu ya kibajeti Sh545.8 bilioni. 

Tunasikitika kwa habari ambayo ilichapishwa katika mitandao yetu jana na kuonyesha kuwa wahisani wamechangia asilimia 6.7 mpaka Januari. Sh144 bilioni  ambazo tulizitumia katika habari hiyo ni fedha ambazo wahisani wamechangia moja kwa moja katika miradi ya maendeleo, hazijumuishi misaada na mikopo mingine.

Kumradhi



Chanzo: mwananchi.co.tz