Baraza la Ushauri la watumiaji wa huduma za Mawasiliano (TCRA CCC), limepiga marufuku upandaji bei ya vocha za simu kiholela na kudai ni batili na kinyume cha sheria.
Katibu Mtendaji wa TCRA CCC, Mary Shayo Msuya akizungumza jijini Dar es Salaam jana Januari 10,2022 amesema hivi karibuni, kumekuwa na malalamiko ya watumiaji wa huduma za mawasiliano kuhusu kupanda kwa bei za vocha za simu za mkononi maeneo mbalimbali.
Bei hizo zimekuwa zikitofautiana baina ya wauzaji; hivyo kusababisha malalamiko kutoka kwa watumiaji.
”Baraza linashauri watoa huduma kujadiliana na mawakala wao namna bora ya kutoza kamisheni bila kumuongezea mtumiaji mzigo wa gharama zitokanazo na mabadiliko ya kamisheni, pale yanapokuwepo,” amesema Mary.
Kauli ya Mary imekuja baada ya hivi karibuni vocha za simu za mkononi kupanda bei kutoka Sh 500 hadi Sh 550 au Sh 600 wakati vocha za Sh 1,000 zinauzwa kwa Sh 1,100 hadi Sh 1,200.
Amesema baadhi ya watoa huduma wameeleza kwamba wamefanya mabadiliko katika kamisheni wanazopata wasambazaji wakubwa wa huduma za vocha.
Pia baadhi ya wasambazaji wakubwa wameshusha makato ya kamisheni kwa wauzaji wadogo wa rejareja na wauzaji wa rejareja wameongeza gharama za vocha kwa watumiaji.
“Muuzaji yeyote anayeuza vocha kwa bei tofauti na iliyoidhinishwa anafanya kosa la jinai na anapaswa kuripotiwa kituo cha Polisi ili aweze kuchukuliwa hatua,” amesema.
Amesema Baraza, kupitia Kamati ya Watumiaji ya Mkoa wa Lindi imebaini uwepo wa hali hiyo katika Wilaya ya Liwale Kata za Mbaya, Mihumo, Likongowele na Kichonda.
Maeneo mengine ni Nachingwea Kata za Nditi, Mnero, Miembeni, Nambalapala, Kilima Rondo, Lionja na Lindi Manispaa katika Kata za Nangaru, Mtimba, Chikonji, Mipingo, Kitomanga na Kilangala.
Amesema Kamati ya Watumiaji ya Mkoa wa Arusha imebaini hali hiyo katika kata ya Sombetini na sehemu nyingine.
Mary amesema kuwa mujibu wa Mamlaka ya Mawasiliano, gharama za vocha za simu hazijapanda, watumiaji wanapaswa kununua vocha kwa bei husika ambayo inaandikwa katika vocha anayonunua.
“Baraza linatamka kwamba mabadiliko yoyote ya kamisheni kwa wauzaji wa jumla hayapaswi kubebeshwa mtumiaji wa mwisho kwani makubaliano ya kamisheni ni kati ya mtoa huduma na mfanyabiashara husika,” amesema.
Amesema Baraza linashauri watoa huduma kujadiliana na mawakala wao namna bora ya kutoza kamisheni bila kumuongezea mtumiaji mzigo wa gharama zitokanazo na mabadiliko ya kamisheni, pale yanapokuwepo.
“Wakati changamoto hii ikiendelea kupatiwa ufumbuzi Baraza linawashauri watumiaji kununua muda wa maongezi kupitia simu za mkononi,” amesema
Pia amewataka watumiaji wa huduma za mawasiliano kuendelea kutoa taarifa za kupanda bei katika maeneo mbalimbali ya nchi ili wahusika wachukuliwe hatua za kisheria na hali hiyo kukomeshwa.