Serikali ya Marekani kupitia Shirika la Misaada la taifa hilo (USAD) imeingia makubaliano ya ushirikiano na Benki ya CRDB pamoja na shirika la DFC kuimarisha uchumi na kuboresha huduma za kijanii kupitia mkopo wa Sh bilioni 100.
Balozi wa Marekani nchini Dr Donald Wright amethibitisha nia ya Serikali ya Marekani katika kuimarisha ukuaji wa uchumi wa Tanzania kupitia ushirikiano huo uliosainiwa katika Makao Makuu ya Benki ya CRDB jijini Dar es Salaam kati ya Benki ya CRDB na mashirika hayo ya Kimarekani Alhamisi, Juni 30, mwaka huu.
Kupitia ushirikiano huo, mashirika ya Kimarekani ya USAID na DFC yatashirikiana na Benki ya CRDB kuwezesha mikopo yenye thamani ya Shilingi Bilioni 100 za kItanzania. Ushirikiano huo utaiwezesha Benki ya CRDB kutanua wigo wa uwezeshaji wa mikopo wa wanawake na vijana sambamba na kutoa mikopo zaidi katika sekta za elimu, afya na sekta zisizo rasmi Tanzania nzima.
Mikopo katika Sekta ya Afya: Benki itatoa mikopo ya hadi Shilingi Bilioni 20.3 katika sekta ya afya. Mikopo hii itatumika kusaidia katika ujenzi wa mahospitali, vituo vya afya, kliniki, vituo cha uchunguzi wa afya, maduka ya madawa na huduma za uzazi pamoja na ununuzi wa vifaa ya matibabu na ujenzi au ukarabati wa maeneo ya kutolea huduma za afya.
Mikopo katika Sekta ya Elimu: Benki itatoa mikopo ya hadi Shilingi Bilioni 37.5 katika sekta ya elimu kusaidia katika mnyororo wa thamani wa elimu ikiwemo uanzishwaji wa elimu isiyolenga kupata faida, shule za msingi na sekondari zinazolenga misingi ya imani ya dini ambazo zitahudumia sekta ya elimU sambamba na utoaji mikopo kwa biashara zinazolenga kutoa upatikanaji wa vifaa vya elimu.
Mikopo kwa Biashara Ndogo na Kati: Benki itatoa hadi Shilingi Bilioni 17.9 katika sekta ya biashara ndogo na kati. Benki itajikita katika biashara za sekta zote za uchumi kusaidia katika mitaji ya uendeshaji, manunuzi ya vifaa, ujenzi na ubadilishwaji wa sehemu za biashara ili kukuza biashara.
Mikopo kwa Sekta zisizo Rasmi: Benki itatoa hadi Shilingi Bilioni 23.1 kusaidia biashara zisizo rasmi kutoka katika sekta zote za uchumi ambapo kipaumbele kitakua kwenye biashara zinazoendeshwa na vijana na wanawake.