Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mapya yaibuka Stendi ya Magufuli

Stendi Magufuliii Magufulii Mapya yaibuka Stendi ya Magufuli

Thu, 2 Nov 2023 Chanzo: mwanachidigital

Ikiwa imepita miaka miwili tangu kuanza kutumika kwa stendi ya mabasi ya kwenda mikoani ya Mbezi-Magufuli baadhi ya wafanyabiashara wamelalamika moja ya jengo kuvuja kipindi cha mvua.

Wafanyabiashara hao waliiambia Mwananchi Digital kuwa stendi hiyo imekuwa na tatizo la kupitisha maji eneo la juu ambalo kuna sehemu inatumika kufanya ibada kwa dini zote.

Ili kuthibitisha malalamiko hayo leo, Jumatano Oktoba 1,2023 Mwananchi lilikwenda kwenye jengo linalolalamikiwa kuvuja ambalo lipo kwenye mlango wa kuingilia magari na kukuta baadhi ya maeneo yakiwa na maji licha ya kufutwa na wafanyausafi wa stendi hiyo baada ya mvua kukatika.

Mmoja wa wafanyabiashara na mkaribisha abiria wa stendi hiyo, Aboubakar Kuzika amesema walishaongea na uongozi kuhusu eneo hilo ambalo ikifika kipindi cha mvua kunajaa maji na kusababisha baadhi ya vitu vyao kuloa lakini hawajafanyia kazi.

"Stendi yetu ni nzuri lakini inahitaji ukarabati wa hali ya juu kwa kutumia mapato yanayokusanywa hapa na si kusubiri bajeti kutoka Serikali kuu,"amesema Kuzika.

Amesema kuna baadhi ya ofisi zinaingia maji na kusababisha kuhamishwa kwa baadhi ya nyaraka zao.

Sara Lyimo mfanyabiashara wa chakula amesema kuvuja kwa eneo hilo limewanyima fursa baadhi ya wafanyabiashara kutokana na maelezo ya wenyeji kuwaeleza hali halisi iliyopo.

"Kuna watu walikuja kuulizia ili kuweka biashara tuliwaambia eneo lipo lakini linavuja hivyo watajikuta wanakula hasara,"amesema Sara.

Akizungumza kwa simu Kaimu Meneja wa Stendi hiyo, Salehe Ngole amekiri amekiri kuwepo changamoto hiyo na kusema wameshamtafuta mhandisi kwa ajili ya kufanyia maboresho sehemu husika.

"Tulipompata mhandisi alikuja akaangalia kabla ya mvua kunyesha tukakubaliana arudi kipindi cha mvua na juzi alikuja akafanya tathmini yake,"amesema Ngole.

Alisema kutokana na mvua zinazoendelea atampigia leo kwa ajili ya kuuliza siku ya kuanza ukarabati huo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo, Elias Ntiruhungwa amesema hafahamu uuvujaji wa kituo hicho, hivyo atatuma mhandisi kufuatilia jambo hilo.

"Nipo safarini Arusha na sina taarifa ya tatizo hilo nitampigia simu mhandisi sasa hivi afuatilie hilo tatizo ili nijue,"amesema Ntiruhungwa.

Chanzo: mwanachidigital