Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Maputo, farasi na baiskeli zinavyovutia utalii Ngorongoro

867046dcc7daf584e447081b55ada28e Maputo, farasi na baiskeli zinavyovutia utalii Ngorongoro

Fri, 12 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

“AINA hizi za bidhaa za utalii yaani utalii wa maputo ya joto, utalii wa kupanda farasi na utalii wa baiskeli, zinaonekana kuwa na nguvu kubwa kwani tangu ziruhusiwe na kuanza kufanyika katika hifadhi hii, zinaonekana kushika kasi, kuvutia wengi, kupendwa na watalii wanazisifia sana.”

Kamishina Msaidizi Mwandamizi (Huduma za Utalii) wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Paul Fissoo, anabainisha hayo anapozungumzo na HabariLEO kuhusu kuanzishwa kwa bidhaa mpya ya utalii wa kuendesha farasi, baiskeli na kupanda maputo ya joto katika Hifadhi ya Ngorongoro mkoani Arusha.

Ifahamike kuwa, Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro (Ngorongoro Conservation Area- NCA) lilianzishwa kwa Sheria Na. 413 ya Mwaka 1959.

Linajulikana kote duniani, hasa baada ya kuorodheshwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco) katika hadhi tatu kwa nyakati tofauti kama Urithi wa Dunia (World Heritage Site).

Hii ni Hifadhi ya Watu na Baianowai (Man and Biosphere Reserve) na Mtandao wa Hifadhi za Jiologia (Global Geopark Network). Inasifika kwa kuwa moja ya maajabu saba ya asili barani Afrika.

Chanzo kimoja kinasema, Hifadhi ya Ngorongoro ina zaidi ya wanyamapori wakubwa 25,000, wakiwa pamoja na vifaru, viboko, tembo, nyati, twiga, simba, chui, pundamilia, nyumbu, fisi na wengine.

Kwa mujibu wa Fissoo, ni eneo unaloweza kumwona faru kwa urahisi katika mazingira yake ya asili.

“Hifadhi hii pia ndipo yanapopatikana mabaki ya zamadamu katika Bonde la Olduvai maarufu, Olduvai Gorge, yanayoonesha kwamba, wanyama hao waliokoma walikuweko tangu zaidi ya miaka milioni tatu iliyopita,“ kinasema chanzo mtandaoni.

Kamishna wa Uhifadhi wa NCAA, Dk Freddy Manongi, anasema katika Hifadhi ya Ngorongoro, kipo kivutio kingine kikubwa na kipya ambacho ni Hifadhi ya Jiolojia ya Ngorongoro- Lengai ambayo licha ya kuwa na vivutio vingi yakiwamo masalia ya viumbe hai vya kale kama mabaki ya binadamu, wanyama, mimea na zana za mawe, pia inavyo vivutio vingine vingi.

Dk Manongi anafahamisha kuwa, Hifadhi ya Jiolojia ya Ngorongoro - Lengai ni ya pili barani Afrika ikitanguliwa na iliyopo Morocco, lakini hii ikiwa ya kwanza na pekee katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Kuhusu Kreta ya Ngorongoro, chapisho la NCAA liitwalo, ‘Hifadhi- Jiolojia ya Ngorongoro Lengai’ linasema: “Hilo ni bonde kubwa lililosababishwa na kuporomoka kwa kilele na hatimaye, kudidimia kwa mlima wa volkeno ambao pengine ulikuwa mrefu kuliko Mlima Kilimanjaro.”

Hata hivyo, kwa miaka mingi watalii wamekuwa wakifanya utalii uliozoeleka wa kutumia magari kutoka sehemu moja hadi nyingine wakiwa ni watazamaji wakati mwingi wa safari, wanakuwa wamekaa tu, kwenye gari bila kujishughulisha huku mambo mengine wakiwa hawawezi kuyaona kama yalivyo matamanio yao.

Fissoo anasema: “Kutokana na hali hiyo tangu Julai 2017, (Hifadhi ya Ngorongoro) tumeruhusu kuanzishwa kwa bidhaa nyingine za utalii kama wa kutumia maputo, kupanda farasi na utalii wa kuendesha baiskeli ili kumfanya mtalii afurahie zaidi safari yake kwa kuiona Ngorongoro katika sura tofauti tofauti na kushirikisha mwili wake ili kujenga afya zaidi. ”

Wadau wa utalii wanaipongeza Hifadhi ya Ngorongoro kwa kuanzisha aina hizi za utalii wakisema zitachochea ongezeko la watalii na siku za watu kutaka kukaa katika hifadhi na hata wanapoondoka, wapende kurudi kwa kuwa wanapokuja, hawaji tu kutazama, bali pia kushiriki.

UTALII WA BAISKELI

Kuhusu utalii wa baiskeli, Fissoo anasema: “Huu ni utalii ambao mtu anaruhusiwa kuja na baiskeli yake na kuitumia akiwa ndani ya hifadhi katika maeneo na utaratibu maalumu.”

Anaongeza: “Wakati unajiandaa kufanya safari kwa kutumia baiskeli, pamoja na mambo mengine suala la usalama limepewa kipaumbele, hivyo mwandaaji anapaswa kuhakikisha usalama wa wageni kwa kutanguliza gari moja mbele na lingine nyuma ya msafara.”

“Maeneo ambayo mtalii anaweza kuzuru kwa kutumia baiskeli si hatarishi kwani ni katika barabara inayopita katika maeneo ya makazi ya wenyeji.”

Mintarafu faida ya utalii wa kupanda baiskeli, Fissoo anasema ni pamoja na kumfanya mgeni kujishughulisha mwenyewe kama mazoezi kwa kupita maeneo mbalimbali ya vivutio ambayo wakati mwingine, inaweza kuwa vigumu kuvifikia kwa kutumia gari mfano kutoka Naiyobi kwenda Oldonyo Lengai.

MAPUTO

Akizungumzia utalii wa kutumia maputo ya joto, anasema ni utalii ambao watalii wanaingia kwenye puto maalumu la kupaa angani na kusafiri kama ndege kutoka sehemu moja hadi nyingine ndani ya hifadhi na kwenda sehemu yenye vivutio wanavyovitaka wageni.

Fissoo anasema utalii huu hushirikisha kampuni maalumu zenye leseni maalumu zilizokubaliwa maana huduma hizi ni kama ndege na kampuni hizo zinao ‘marubani’ wa kuendesha hayo maputo wenye leseni maalumu kama ilivyo rubani wa ndege.

“Kwa kutumia aina hii ya utalii, wageni wanaruka juu na kuangalia vivutio mbalimbali wakiwa angani,” anasema.

Kwa mujibu wa Fissoo, hadi sasa zipo kampuni tatu zilizofanya mazungumzo na kukubaliwa kutoa huduma hizo katika Hifadhi ya Ngorongoro ambazo ni Serengeti Safari Balloon; Miracle Adventure iliyopo eneo la Ndutu na kampuni ya Adventure Aloft iliyopo eneo la Olduvai ndani ya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro.

Meneja Mauzo na Masoko wa kampuni ya Adventure Aloft, Cecilian Samson, anasema utalii huu huwezesha watalii kuona vivutio vingi wakiwamo wanyamapori kwa kushuka na kuwakaribia wakiwa juu kuliko namna nyingine ya utalii ambazo si rahisi kuona mahali na wanyamapori wengine.

“Ingawa utalii huu unapendwa sana, lakini una changamoto kwamba watu wengi hasa Watanzania, wanashindwa kumudu gharama...” anasema Cecilian.

Anaongeza: “Changamoto ya balloon (puto) wakati mwingine ni udhibiti angani kunapotokea hakuna utulivu wa upepo kwa sababu haitegemei control (udhibiti) yako, lakini ikitokea upepo unazidi kiasi, mwongozaji huwashusha hata kabla ya muda.”

FARASI KATIKA UTALII

Kuhusu utalii wa kutumia farasi, Fisso anasema hufanywa kwa mgeni kupewa farasi kutoka kampuni maalumu zilizoruhusiwa kuingiza farasi katika hifadhi zikiwa na leseni maalumu kwa ajili ya huduma hizo.

Anapozungumzia sababu ya mgeni kutokuja na farasi wake, Fissoo anasema: “Farasi kutoka katika kampuni zilizokubaliwa wana mafunzo kutoka wamiliki waliothibitishwa na wana uzoefu wa kuwa katika maeneo yenye wanyamapori kwa muda mrefu. Kampuni hizo zimesajiliwa na Bodi ya Utalii Tanzania kufanya biashara hiyo.”

Imebainika kuwa, kampuni zilizoruhusiwa kutoa huduma za utalii wa farasi katika Hifadhi ya Ngorongoro ni Kaskazi Horse Riding Safaris na Makoa Horse Riding Safaris.

Fissoo anasema ili mtalii aweze kumwendesha farasi, lazima awe na mafunzo ya awali na pia kampuni husika ina jukumu la kumpa mafunzo ya ziada na wakijiridhisha ndipo mtalii huruhusiwa kuendesha farasi na wakati wote, watakuwa na kiongozi kutoka kampuni husika.

Meneja wa kampuni ya Kaskazi Horse Safaris ya Arusha, Mereso Kaika, anasema, mgeni anapopanda farasi hawezi kuwa pekee, bali lazima kuwapo farasi mwingine anayoongozwa na kiongozi na kutoa maelekezo kwa mgeni kuhusu nini cha kufanya.

Anasema kutokana na ukubwa wa gharama, mara nyingi huduma za utalii wa farasi hazitolewi kwa mtu mmoja, bali kwa kundi la watalii.

FAIDA

Kwa mujibu wa Fissoo, faida za bidhaa hizi mpya za utalii kwa jumla, ni pamoja na kuwa rafiki wa mazingira katika hifadhi huku pia, zikiwashirikisha watalii badala ya kuwaacha wakae na kuwa watazamaji kwa muda wote wanaposafiri hifadhini.

Anasema: “Aina hizi za utalii itasaidia kuongeza idadi ya watalii kukaa ndani ya hifadhi na hatimaye, kuongeza mapato yatokanayo na utalii na zaidi ya yote, kufurahia zaidi safari yao.”

Kuhusu uwezo wa puto moja kubeba watalii, anasema maputo hutofautiana ukubwa, lakini ni mengi ni kati ya mtu mmoja hadi 12 kutegemea uzito wa abiria na hali ya hewa kwa kadiri ya maamuzi ya rubani na taratibu za sheria za anga na miongozo ya kampuni yake.

TOZO HIFADHINI

Fissoo anasema watalii wa ndani kwa safari za farasi huilipa hifadhi Sh 10,000, kuendesha baiskeli ni Sh 10,000 na tozo ya kuruka kwa puto la joto hifadhini ni Sh 40,000.

“Kwa watalii kutoka nje ya nchi, ni Dola za Marekani 10 kwa farasi, Dola 15 kwa baiskeli na Dola 33.50 kwa puto la joto bila malipo ya kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwa siku moja au muda maalum hasa puto la joto,” anasema.

Anawahimiza watalii wakiwamo wa ndani ya nchi kujitokeza kufurahisia vivutio mbalimbali na bidhaa hizo mpya za huduma za utalii katika Hifadhi ya Ngorongoro.

Chanzo: www.habarileo.co.tz