Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mapinduzi makubwa soko la dhahabu

32ac7a2cb5a681a8129360762b471d1b.png Mapinduzi makubwa soko la dhahabu

Tue, 16 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

UJENZI wa kiwanda chenye mtambo wa kisasa wa kusafisha dhahabu kwa kiwango cha kimataifa, Mwanza Precious Metal Refinery (MMPR), umekamilika.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Dk Venance Mwasse, amesema kukamilika kwa kiwanda hicho, kutaiwezesha dhahabu ya Tanzania kuwa na ubora wa kimataifa.

Aliyasema hayo jana jijini Mwanza wakati akitoa taarifa ya ujenzi wa kiwanda hicho kwa Waziri wa Madini, Doto Biteko.

Dk Mwasse alisema mtambo wa kisasa ya kiwanda hicho, una uwezo wa kusafisha kilo 480 za dhahabu kwa kuanzia kwa siku na unaweza kuongezewa uwezo usafishe hadi kufikia kilo 960 kwa siku.

"Mwanza sasa inakwenda kuwa "trading centre na suala zima la biashara ya usafishaji wa dhahabu litahamia hapa," alisema na kubainisha Rozella General Trading ndio waliojenga kiwanda hicho.

Alisema ujenzi huo uliogharimu Sh bilioni 8.9 ulianza Machi 15 mwaka jana na kwa sasa umekamilika kwa kazi za kiuhandisi, ukiwemo ufungaji mtambo unaotarajiwa kuanza kazi ya kusafisha dhahabu Machi Mosi mwaka huu.

"Lengo kuu la mtambo huu ni kuongeza thamani ya madini ya dhahabu yanayochimbwa hapa nchini na kuongeza mapato ya nchi kupitia mrabaha na kodi mbalimbali, ikiwemo kutoa ajira 120 kwa Watanzania," alisema Dk Mwasse.

Alisema, mradi huo unatarajiwa kuongeza ajira chache kutoka nje ya nchi, ajira za wazalishaji wa dhahabu, wazabuni, watoa huduma na wasafirishaji.

Alisema serikali kupitia STAMICO imeingia ubia na kampuni ya Lozera General Trading kutoka Dubai, na inamiliki asilimia 25 ya hisa na Kampuni hiyo ya Lozera inamiliki asilimia 75.

Dk Mwasse alisema, mtambo huo utaongeza mapato kwa STAMICO kupitia huduma za usimamizi na faida ya kila robo mwaka.

"Faida nyingine ni kupunguza utoroshaji wa dhahabu kwenda nje ya nchi, kwani tutakuwa na soko la uhakika la dhahabu ambayo haijasafishwa na iliyosafishwa na kuifanya dhahabu inayozalishwa Tanzania kutambulika na kuwa na nembo yake maalumu," alisema.

Dk Mwasse alisema madini mengine kwenye dhahabu, yataainishwa na kuthaminishwa nchini na kuwezesha Benki Kuu ya Tanzania kuanza kununua dhahabu kwa mujibu wa sheria za nchi.

Alisema, kutokana na uwekezaji na ujenzi wa kiwanda hicho, kwa mwaka STAMICO inatarajia kupata mapato ya Sh bilioni 22 na Tume ya Madini inatarajia kuvuna kati ya Sh bilioni 500 hadi bilioni 600 kwa mwaka.

Dk Mwasse alisema fedha hizo, zitaongeza mapato yanayotokana na dhahabu hadi kufikia Sh trilioni moja kwa mwaka na kuiwezesha Wizara ya Madini kuchangia asilimia 10 kwenye Pato la taifa.

”Lakini pia Serikali itaanza kukusanya mrahaba kwa kuchukua dhahabu badala ya fedha, na wananchi wanaozunguka mradi huu watanufaika na fedha itakayotolewa na STAMICO kwa ajili ya huduma za kijamii(CSR)," alisema.

Mwenyekiti wa Kamati ya Pamoja ya Usimamizi wa mradi huo, Deusdedit Magala, alisema kwa sasa wanaunda kampuni ndogo itakayosaidia wachimbaji wadogo waweze kunufaika na madini wanayochimba.

Alisema utafiti mdogo uliofanywa katika mikoa ya Mara, Tabora (Nzega), Geita, Mbeya (Chunya) ulibaini kuna faida kubwa, endapo wachimbaji wadogo watawezeshwa vifaa vya kuchimbia dhahabu, watazalisha kwa wingi na kwa ubora na hivyo kujiongezea kipato na kuongeza mapato ya Serikali.

Waziri wa Madini, Dotto Biteko alimpongeza Mtendaji Mkuu na mwakilishi wa Rozella Trading nchini, Ananel Mahojan na menejimenti, kwa kazi kubwa waliyofanya ya ujenzi wa kiwanda na mtambo huo kwa kushirikiana na watalaamu kutoka STAMICO.

Alisema kukamilika kwa kiwanda hicho, kutaziwezesha kampuni na mashirika yanayojihusisha na uchimbaji dhahabu, kuhakikisha madini hayo yanasafishwa kiwandani hapo ili fedha zinazotokana na dhahabu zibaki nchini.

Alisema, lengo lingine la serikali ni kuhakikisha migodi yote ya dhahabu nchini, inasafishia dhahabu kupitia kiwanda hicho ili madini mengine yatakayokuwa yanapatikana kwenye dhahabu kama vile shaba, chuma na mengineyo, yathaminiwe ili thamani ya fedha ibaki nchini.

Chanzo: habarileo.co.tz