Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mapinduzi makubwa biashara ya madini

45f97b0d29a0712a2f4ef374cf40a898 Mapinduzi makubwa biashara ya madini

Mon, 25 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

MAPINDUZI makubwa katika biashara ya madini yanatarajiwa kuendelea kuonekana baada ya kiwanda cha kusafisha dhahabu mkoani Mwanza na cha uchenjuaji madini hayo mkoani Geita kukamilika mwezi ujao.

Kiwanda cha kusafisha dhahabu cha Mwanza (Mwanza Precious Metals Refinery Ltd) kinachojengwa jijini Mwanza, kinatarajiwa kuanza uzalishaji mwezi ujao; vivyo hivyo kwa kiwanda cha uchenjuaji wa dhahabu cha G2R cha Geita.

Hayo yalifahamika kupitia ziara ya Katibu Mkuu, Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila, aliyetembelea ujenzi wa viwanda hivyo kwa nyakati tofauti wiki hii.

Akizungumzia mradi wa ujenzi wa kiwanda cha Mwanza kinachosimamiwa na Shirika la Madini la Taifa (Stamico) chini ya Mamlaka ya Ukanda Maalum wa Uwekezaji nchini (EPZA), Msanjila alisema utaleta mapinduzi makubwa katika sekta ya madini hususan katika biashara ya dhahabu nchini na utaongeza mapato yatokanayo na madini hayo.

Msanjila alisema, viwango vya usafishaji dhahabu nchini vitakuwa vya kimataifa na hivyo, kuijengea heshima nchi.

Aliipongeza Stamico kwa hatua nzuri ya ujenzi iliyofikiwa na sasa wamepokea magari makubwa mawili yaliyosheheni mitambo kwa ajili ya kufungwa katika kiwanda hicho kwanza cha kusafisha madini kujengwa nchini chenye umiliki wa serikali ndani yake hivyo kitakuwa na faida kubwa.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Stamico, Dk Venance Mwase, alisema Precious Metals Refinery Ltd, utakuwa mtambo mkubwa barani Afrika kwa kusafisha kiwango kikubwa cha dhahabu cha kilogramu 480 kwa siku.

Alisema mtambo huu utakaoanza uzalishaji mwishoni mwa mwezi ujao, pia utatambulika duniani kote kwa kusafisha dhahabu ya viwango vya kimataifa yenye ubora wa asilimia 99.99.

Dk Mwase alisema gharama za mradi huo ambao ujenzi wake ulianza Machi 15, 2020 na kukamilika mwezi Desemba, ni Dola za Marekani milioni 58 ikiwa ni pamoja na gharama za uwekezaji na za uendeshaji na ununuzi wa dhahabu kwa siku 10 za awali.

Alimtaarifu Katibu Mkuu, Msanjila kuwa, mradi huo umejengwa katika eneo la kimkakati kwa kuzingatia kuwa uko katikati ya mikoa inayozalisha dhahabu kwa wingi ambayo ni Geita, Mara, Shinyanga na Mwanza yenyewe.

Aidha, mtambo huo unajengwa sehemu ambayo ni rahisi kupokea dhahabu kwa njia ya anga kutoka nchi jirani kama Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC), Burundi, Msumbiji na Uganda.

Kwa mujibu wa Mwase, mradi unaendeshwa kwa ubia kati ya Stamico, Rozella General Trading LLC ya Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) pamoja na kampuni ya ACME Consultant Engineers PTE Ltd ya Singapore (RGTACE).

Stamico inamiliki asimilia 25 na wabia wanamiliki asilimia 75 huku hisa za shirika hilo la serikali zikitarajiwa kuwa zinaongezeka kwa asilimia tano mpaka miaka 15.

Shirika litakuwa na asilimia 51 na wabia asilimia 49 na itakuwa inapata asilimia 2.5 ya mauzo ghafi kama huduma za usimamizi zinazotolewa na kampuni.

Majukumu ya wabia yametajwa kuwa ni kujenga, kutoa utaalamu wa kuendesha mtambo huo na kutoa mtaji kwa ajili ya kuanzisha vituo vya wachimbaji wadogo vya kuzalisha dhahabu nyingi ili kulisha mtambo wa kusafisha dhahabu.

Stamico itakuwa na kazi ya kusimamia mradi, kusaidia upatikanaji wa vibali vya uendeshaji mtambo huo na kusimamia uendeshaji wa vituo vya wachimbaji wadogo vitakavyoanzishwa Geita kuchenjua dhahabu.

Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu, Wizara ya Madini, Profesa Msanjila alitembelea ujenzi wa kiwanda cha uchenjuaji madini ya dhahabu cha G2R mkoani Geita na kuelezwa kuwa, ujenzi wake umefikia asilimia 99.

Mkurugenzi wa kiwanda hicho, Sarah Masasi, alimweleza katibu mkuu kuwa kufikia mwezi ujao, kitakuwa kimekamilika na kuanza kazi.

Profesa Msanjila alimpongeza mkurugenzi wa kiwanda kwa hatua nzuri ya ujenzi iliyofikiwa.

Tayari mashine mbalimbali zimekwishaingizwa sambamba na kufungwa jenereta kubwa kwa ajili ya umeme wa dharura.

Awali, Msanjila alitembelea Ofisi ya Ofisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Geita, Daniel Mapunda, kupata taarifa za shughuli za madini za mkoa huo.

Alisema mwaka 2020/2021 Wizara ya Madini imepangiwa kukusanya Sh bilioni 528 na kwamba, Mkoa wa Geita umepangiwa kukusanya Sh bilioni 200. Hadi sasa umekusanya zaidi ya Sh bilioni 120.

Mkuu wa Wilaya ya Geita, Fadhili Mohamed Juma, alimpongeza Msanjila kwa usimamizi makini na maelekezo yake ili kuimarisha usimamizi wa sekta ya madini. Aliahidi kutekeleza kila agizo atakalolitoa mkoani humo.

Ofisa Madini Kazi wa Mkoa wa Geita, Daniel Mapunda, alisema usimamizi wa sekta ya madini mkoani humo umezidi kuimarik . Hadi Desemba mwaka jana, mkoa ulikuwa umekusanya zaidi ya Sh bilioni 120.

Chanzo: habarileo.co.tz