Mapato yatokanayo na ushuru wa mabasi kuingia na kutoka Kituo cha Mabasi cha Magufuli yameongezeka kutoka Sh 500,000 kwa siku hadi Sh 1,195,000.
Ongezeko hilo linatokana na kutiiwa kwa agizo la Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Innocent Bashungwa la kutaka mabasi yote kuanzia safari Kituo cha Mabasi cha Magufuli.
Bashungwa alitoa agizo hilo Mei 30, 2022 wakati akiwa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo alipofanya ziara kituoni hapo.
Agizo hilo lkimefanya mabasi yanayoingia kituoni hapo na kutoka kuongezeka kutoka 100 hadi 265 kwa siku.
Akizungumza na HabariLEO jana, Ofisa Biashara wa kituo hicho, Geofrey Mbwama alisema baada ya agizo hilo kuna ongezeko mara mbili na wanatarajia ongezeko kubwa kuanzia leo kwakuwa siku saba za agizo hilo zinafikia tamati leo.
“Kwa kiasi kikubwa agizo la Bashungwa limezaa matunda hadi muda huu saa 4:15 asubuhi (jana) tayari magari 117 yametoka, bado mengine yanaendelea kutoka, itakapofika jioni tutafahamu ni mabasi mangapi yalitoka kwa siku ya leo (jana), mabasi yaliyoanzia safari kituoni hapa ni 265, na yaliyongia ni 201,” alisema.
Kabla ya agizo hilo magari yaliyokuwa yakianzia safari zake kituoni hapo yalikuwa machache ambapo Mei 30, 2022, yaliyoingia yalikuwa 100 wakati yaliyotoka 103, kwa Mei 31, 2022 yaliyoingia yalikuwa 108 na yaliyotoka yalikuwa 110.
Mbwama alisema lengo lao ni mabasi 300 hadi 350 yaingie na kutoka kwa siku kutoka na msimu wa biashara ulivyo.
Agizo la Bashungwa lilitanguliwa na agizo la Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa Itikadi na Uenezi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Shaka Hamdu Shaka alilolitoa Mei 25,2022 alipofanya ziara katika kituo hicho ambapo aliagiza Tamisemi kushugulikia suala la mabasi kutoingia kituoni hapo haraka.
Kutoingia kwa mabasi kituoni hapo kulikuwa kunakipunguzia kituo mapato na kuwakosesha biashara wapangaji katika kituo hicho na waendesha bodaboda na bajaji ambao hutegemea kituo hicho kuendesha maisha yao.