Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) imekusanya Sh171 bilioni kwa mwaka 2022/23 kutoka Sh31 bilioni kwa mwaka 2020/21 kiwango hicho ni cha juu kuwahi kukusanywa na mamlaka hiyo.
Kamishna wa Uhifadhi wa NCAA, Richard Kiiza amesema wanatarajia kukusanya Sh200 bilioni kwa mwaka 2023/24 baada ya kukusanya Sh123 bilioni katika kipindi cha nusu ya mwaka huo.
“Mapato haya yameongezeka kwa asilimia 13 ukilinganisha na mapato yaliyokusanywa katika kipindi kama hicho kwa mwaka 2022/23,” amesema Kiiza.
Akizungumza katika kikao kazi na wahariri na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Februari 26, 2024, Kiiza amesema idadi ya wageni katika Hifadhi ya Ngorongoro imekuwa na matokeo chanya kwenye ongezeko la mapato yatokanayo na utalii.
Amesema juhudi za Rais Samia katika kufufua sekta ya utalii baada ya Uviko 19 kupitia filamu ya Tanzania The Royal Tour, zimechangia ongezeko kubwa la idadi ya wageni wanaotembelea hifadhi hadi kufikia 752,232 mwaka 2022/23 ikilinganishwa na wageni 191,614 waliotembelea mamlaka hiyo mwaka 2020/21.
Amesema wanatarajia idadi itaongezeka na kufikia takribani wageni milioni moja mwaka 2023/24.
Katika nusu ya kwanza ya 2023/24 amesema hifadhi imepokea wageni 534,065 ikiwa ni ongezeko la asilimia 10 kulinganisha na idadi ya walitembelea hifadhi katika kipindi kama hicho mwaka 2022/23.
“Ni ukweli usiopingika matokeo haya ya kuongezeka kwa watalii ni juhudi kubwa zilizofanywa kupitia filamu ya Royal Tour kwa kusaidia kutangaza utalii ndani na nje ya nchi,” amesema Kiiza wakati akizungumzia mafanikio yaliyopatikana katika miaka mitatu ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.
Ushauri wa wadau
Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wamiliki wa Hoteli Tanzania (HAT), Kennedy Edward amesema mapato ya utalii ni ya msimu kutokana na uingiaji wa watalii nchini, hivyo kuna haja ya kufanyia kazi malengo ambayo NCAA imejiwekea.
Amesema wakati unaposubiriwa msimu wa watalii Mei na Juni, kuna haja ya Serikali kuangalia soko la ndani ambalo litahusisha watu wa mashirika na balozi mbalimbali kwa kuwa wanakuwepo nchini kwa muda mrefu.
“Kuna muda mfupi uliobaki ili kumalizika kwa mwaka wa fedha na kwa hesabu zilizopo imebaki miezi minne hamasa inayotolewa kwa sasa iangalie soko la ndani ambalo ni la watu wanaopokea wageni mara kwa mara kuona namna ya wao kuwapeleka kwenye maeneo ya kitalii,” amesema Edward.
Pia, amesema wakati wanaendelea kuhamasisha utalii wanatakiwa kuboresha maeneo ya hifadhi yaliyopo na kuendeleza mapya.
“Tunaweza kufurahia mapato ambayo tumeyapata na kuingiza watalii wengi lakini tusipoboresha maeneo yetu watalii wanapokuja wanaweza kuharibu zaidi na tukajikuta tunatumia pesa nyingi kukarabati,” amesema Edward.
Ameiomba Serikali kukaa na sekta binafsi zinazojihusisha na masuala ya utalii kujadili namna ya kuboresha sekta hiyo ili kutoa huduma bora.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Chama cha wenye Kampuni za Utalii (Tato), Sirili Akko amesema mamlaka wanatakiwa kuboresha mfumo wa malipo ambao umekuwa ukilalamikiwa kuwa si rafiki.
“Tunawapongeza mamlaka kwa makusanyo, pamoja na hayo wanatakiwa kuboresha miundombinu ili kuendana na gharama anayolipa mgeni,” amesema Akko.
Hata hivyo, katika kikao kazi na wanahabari, Kiiza amesema kupitia fedha za Uviko 19, Serikali ilitoa takribani Sh6.645 bilioni zilizotumika kuimarisha miundombinu ya barabara, kununua magari na mitambo ya kutengenezea barabara, kuimarisha viwanja vya ndege na miundombinu mingine ya utalii ili wageni waweze kufikia vivutio vya utalii kwa urahisi.
Amesema Serikali imetenga Sh69 bilioni kwa ajili ya kujenga tabaka gumu kipande cha barabara chenye urefu wa kilomita 29.5 kutoka lango kuu la kuingilia NCAA hadi Seneto.
Kuhama kwa hiari
Kuhusu kuhama kwa hiari wananchi wanaoishi ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro, Kiiza amesema hadi Februari 25, 2024 kaya zilizohama ni 1,042 zenye watu 6,461 na mifugo 29,919.
Maeneo yaliyotengwa na Serikali ni Kijiji cha Msomera, wilayani Handeni, Saunyi wilayani Kilindi na Kitwai B wilayani Simanjiro.
Kiiza amesema awamu ya kwanza ilianza Juni, 2021 kwa kujenga nyumba 503 pamoja na huduma zingine za kijamii kama vile shule, miundombinu ya maji, zahanati, barabara, mawasiliano, umeme, majosho, mabwawa, maeneo ya malisho na huduma ya posta.
“Hadi Januari, 2023 wakati awamu ya kwanza inakamilika kaya 551 zenye watu 3,010 na mifugo 15,521 walihamia Msomera,” amesema.
Amesema awamu ya pili ilianza Julai, 2023 kwa mpango wa kujenga nyumba 5,000 Msomela (2,500), Saunyi (1,000) na Kitwai B (1,500).
Wananchi hao amesema hulipwa fidia za kisheria na motisha.
Fidia za malipo ya kisheria amesema zinajumuisha za maendelezo, gharama ya usafiri wa watu na mali zao.
Malipo ya motisha amesema ni nyumba moja katika eneo lenye ukubwa wa ekari mbili na nusu kwa kila mkuu wa kaya, shamba lenye ukubwa wa ekari tano kwa kila mkuu wa kaya na hati miliki ya kiwanja na shamba na eneo la malisho ya mifugo.
Nyingine ni Sh10 milioni kwa kila mkuu wa kaya, chakula wakati wa kusafiri na malazi siku ya kusafiri katika eneo la Karatu. Chakula kiasi cha gunia mbili kwa kipindi cha miezi mitatu.
“Kwa wale wanaoenda maeneo waliyochagua wenyewe wanapewa malipo sawa na wengine isipokuwa motisha inakuwa Sh15 milioni,” amesema.
Amesema uamuzi huo wa Serikali umeongeza hamasa kwa wananchi na kujenga imani juu ya nia njema ya kuwaboreshea maisha yao na kuinusuru hifadhi kwa ajili ya manufaa mapana ya Taifa.