Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Maonesho NSSF Temeke ‘yamnasa’ mfugaji wa kuku

542f60a1860d41968265a664e0016e97.png Maonesho NSSF Temeke ‘yamnasa’ mfugaji wa kuku

Fri, 25 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MFUGAJI wa kuku, Zablon Kamando amejiunga na Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) na kujiwekea michango yake papo hapo kwa muda wa miezi mitano huku akiahidi kuwa balozi mzuri wa kuwahamasisha wenzake wajiunge na shirika hilo kwa faida yao ya sasa na baadaye.

Kamando alisema hayo jana wakati akimuonesha risiti ya michango yake Meneja wa NSSF Mkoa wa Temeke, Rebule Maira.

Mfugaji huyo alieleza kuwa akiwa katika maonesho ya kutatua kero za wananchi wa Wilaya ya Temeke yaliyopewa jina la ‘One Stop Jawabu’yanayoendelea kwenye Viwanja vya Mwembeyanga jijini Dar es Salaam, alitembelea banda la NSSF ambako alipatiwa elimu ya hifadhi ya jamii, na kufahamishwa anavyoweza kunufaika akijiunga nalo.

“Asante NSSF, asante sana serikali yetu kwa kutuwezesha wananchi wa kawaida kunufaika na hifadhi ya jamii, jambo hili halikuwepo miaka ya nyuma,”alisema.

Alisema katika maonesho hayo NSSF inawasaidia wananchi wa hali ya chini kupata elimu ya hifadhi ya jamii, kuwaandikisha na ambao tayari wameshajiunga wanapata taarifa kuhusu michango wanayopelekewa na waajiri wao, kuhakiki taarifa za wanachama wastaafu na wategemezi ili kuziweka katika kumbukumbu nzuri.

Alisema mwananchi atakayejiunga na NSSF kupitia sekta isiyo rasmi inayohusisha wajasiriamali wadogo na wa kati, wakulima, wafugaji, wavuvi, mamalishe na bodaboda wanachangia kima cha chini Sh 20,000 kwa mwezi au zaidi kulingana na kipato chao, na kuwafanya wanufaike na mafao yote yanayotolewa na NSSF.

Meneja wa NSSF Mkoa wa Temeke, Maira alisema mwanachama wa NSSF anaweza kunufaika na mikopo ambayo itaanza kutolewa kwa ushirikiano baina ya Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo Vidogo (SIDO), Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) na Benki ya Azania ili waongeze mitaji yao na kuajiri wengine.

Chanzo: habarileo.co.tz