Dodoma. Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Stella Manyanya amesema tatizo la bidhaa bandia nchini limepungua kwa kiasi kikubwa kutokana na matumizi ya stempu za kielekroniki (Electronic Tax Stamps - ETS).
Serikali ilitangaza kuanza kutumia mfumo wa ETS katika kukusanya kodi mwaka wa fedha 2018/19 lengo likiwa ni kudhibiti udanganyifu wa wazalishaji wa bidhaa zinazotozwa ushuru wa bidhaa.
Awamu ya kwanza ya mfumo wa ETS ulianza rasmi Januari 15 mwaka huu (2019) ambapo stempu za kielektroniki zilianza kubandikwa katika bidhaa 19 za aina ya vilevi tofauti tofauti.
Awamu ya pili ilianza Agosti 1, 2019 ikihusisha bidhaa za vinywaji baridi.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri Manyanya, mbali na kusaidia Serikali kuongeza makusanyo ya kodi, matumizi ya stempu za kielektroniki yamesaidia pia kupunguza tatizo la bidhaa bandia sokoni.
“Tatizo limepungua kwa kiasi kikubwa na tayari bidhaa mbali mbali hivi sasa hubandikwa stempu hizo vikiwemo vinywaji,” alisema.
Pia Soma
- Bei ya mafuta duniani yapanda
- Jinsi matangazo ya uongo ya video za matibabu yanavyoinuisha Youtube
- RC Hapi atoa siku tatu kumbi za burudani, hoteli kufanya kazi saa 24
Naibu Waziri Manyanya alikuwa akizungumza na waandishi wa habari katika kipindi cha vikao vya Bunge vilivyomalizika wiki iliyopita jijini hapa.
Manyanya alikiri awali kuwa kulikuwa na tatizo kubwa ambalo limeendelea kupungua na wamekuwa wakipambana nalo siku hadi siku huku akisema katika vita hiyo lazima ushindi utakuwepo.
Alisema bila kutumia maarifa na ushirikiano baina ya pande zote, jambo hilo hilo lisingewezekana lakini kwa sasa upo mwanga na linaonekana kupungua kwa kiasi kikubwa.
Alisema Tanzania kama zilivyo nchini zingine imekuwa na mkakati wa kulinda bidhaa zake na kuzifanya ziwe na ubora wa hali ya juu ili kuwezesha katika soko la ushindani lakini wajanja wachache ndiyo huvuruga.
Katika Bunge la bajeti 2018/19, aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara wakati huo Charles Mwijage alilieleza Bunge kuwa vita hiyo ilikuwa kubwa kwani ilikuwa ikifanywa na watu wenye fedha lakini akaahidi kupambana hadi Serikali ifanikiwe.