Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mamlaka ya Bandari kufumuliwa, nafasi 68 za vigogo zatangazwa

30114 Pic+tpa TanzaniaWeb

Tue, 4 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) imetangaza nafasi 68 za vigogo ikiwa ni mpango wa kuifumua mamlaka hiyo na kuisuka upya, Mwananchi  imeelezwa.

Akizungumza na Mwananchi leo, Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Deusdedit Kakoko amesema mbali na nafasi hizo 68, nyingine zaidi zitatangazwa baadaye.

“Serikali sasa hivi inapitia watumishi na sifa zao, si ndiyo utaratibu wa kawaida? Mnaona TRC (Shirika la Reli Tanzania) imetangaza zote. Hamkuona TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania) wametoa nafasi 52. Mimi sasa siyo hizo tu (68), zinakuja nyingine utaziona nyingi tu.”

“Serikali nzima hivi sasa inapitia mambo yake ya watumishi kuhakikisha inawapata wenye sifa, hilo ni jambo la kawaida, sio habari,” amesema.

Kakoko amesema jambo hilo ni la ndani licha ya kuulizwa na Mwananchi kuwa tangazo hilo la kazi limechapishwa katika tovuti ya mamlaka hiyo.

“Hayo ni mambo ya ndani hatutoi maelezo. Aliyekwambia hizo nafasi nyingi ni nani? Nyingi ni ngapi? Tatizo ni nini? Kwani wewe hujaona nchi nzima mashirika yote yanafanya hivyo, si Rais (John Magufuli) amezungumza, Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa) kila mahali kila siku anazungumza,” amesema.

Tangazo hilo lililotolewa Novemba 26 na Sekretarieti ya Ajira ya Ofisi ya Rais lenye kumbukumbu Na. EA.7/96/01/J/22 likisema nafasi hizo zinatolewa ikiwa ni mikakati ya kuendelea kuimarisha mamlaka hiyo.

Nafasi zilizotangazwa ni pamoja na wakurugenzi, mameneja na maofisa wa vitengo mbalimbali.

Katika nafasi za wakurugenzi nafasi zilizotangazwa ni mkurugenzi wa mipango, majanga, utawala wa ubora, uhandisi, miundombinu na uwekezaji, usafiri wa maji na operesheni za bandari na wa rasilimali watu na utawala.

Nyingine ni mkurugenzi wa ununuzi na mikataba, mkurugenzi wa ukaguzi wa ndani, meneja wa sheria, meneja wa uhandisi mchundo, meneja wa uhandisi wa makenika, meneja wa makazi na mali, meneja wa utawala wa mazingira, meneja wa mapato, meneja  utawala, meneja masoko, meneja wa uhusiano na mawasiliano na meneja wa huduma zisizo za ushauri.

Nyingine ni ofisa mtakwimu, maofisa sheria (nafasi nne), wakaguzi wa hesabu za ndani (nafasi mbili), ofisa wa ubora, ofisa wa kudhibiti majanga na ofisa ununuzi (nafasi nane).

Mtaalamu wa ardhi, ofisa uthamini, ofisa masoko (nafasi sita), huduma kwa wateja (nafasi mbili), zima moto na uokoaji (nafasi mbili), wahasibu (nafasi tatu) ofisa mifumo ya uongozi (nafasi mbili), maofisa utawala (nafasi tatu) na maofisa maabara (nafasi mbili).

Nafasi nyingine zipo kwenye chuo cha Bandari ambazo ni ofisa programu, msaidizi wa programu, ofisa mitihani, msaidizi wa ofisa mitihani, mkutubi msaidizi, fundi, ofisa mwandamizi wa rasilimali watu na nafasi mbili za watunza kumbukumbu wasaidizi na ofisa wa utawala wa data.

Waombaji wametakiwa kuwa Watanzania walio na umri chini ya miaka 50 kwa nafasi za wakurugenzi na mameneja, huku nafasi nyingine wakitakiwa kuwa chini ya miaka 45.

Wametakiwa pia kuambatanisha vyeti vyao vya elimu na vyetu vya kuzaliwa.



Chanzo: mwananchi.co.tz