IKIWA kesho ni Sikukuu ya Krismasi, mamia ya wananchi wamefurika katika eneo la Kariakoo Jijini Dar Salaam kufanya manunuzi mbalimbali kulingana na mahitaji yao.
HabariLEO ilipita katika mitaa mbalimbali ya eneo la kibiashara la Kariakoo, kujua hali ya biashara wakati huu wa kuelekea sikukuu za Krismasi na Mwaka mpya na kushuhudia mamia ya wananchi wamejaa kwenye mitaa ya eneo hilo, hali iliyofanya magari kupita kwa shida.
HabariLEO ilishuhudia bei za nguo za watoto zikiwa juu wakati za watu wazima zikiwa kawaida.
Katika duka la Kareem New Fashion lililopo Mtaa wa Congo ambalo linauza nguo za watoto na za wakubwa, bei zake kwa nguo za watoto wa kiume ni kuanzia Sh 50,000 mpaka 150,000 kulingana na aina ya nguo ya mteja anayotaka.
Kwa mujibu wa muuzaji wa duka hilo, Juma Khalfani, bei hiyo ilianza tangu mwanzoni mwa Desemba mwaka huu. Alisema bei ya kawaida iliyokuwepo kabla ya Desemba mwaka huu ilikuwa Sh 30,000 hadi 70,000.
Duka lingine la New Fashion nguo za watoto wa kike zinauzwa kuanzia Sh 30,000 hadi 80,000 kutoka Sh 20,000 hadi 40,000. Kwa mujibu wa muuzaji sababu ya kupanda kwa nguo za watoto ni kuwepo kwa mahitaji makubwa ya nguo hizo ikilinganishwa na za wakubwa.
Hapo hapo Kariakoo katika maduka ya Mtaa wa DDC, ambayo kwa kiasi kikubwa yanauza nguo za watu wazima, bei zimeonekana kutopanda kutokana na mahitaji ya nguo hizo kuwa chini, ikilinganishwa na watoto. Nguo za watu wazima zinaanzia Sh 25,000 kwa jinsia zote hadi Sh 50,000.
Baadhi ya wateja waliozungumza na HabariLEO walitaja sababu ya nguo za watoto kununuliwa sana kuwa ni utamaduni uliojengeka katika familia kutaka watoto wapendeze kwanza kabla ya wazazi wao, hasa kipindi hiki ambacho fedha ni adimu kwa wananchi.
“Nguo za watoto zinanunuliwa sana kwa sababu hakuna mzazi sasa hivi asiyetaka mtoto wake apendeze. Mimi hapa niko tayari nisivae lakini watoto wangu wote wavae vizuri wapendeze,” alisema Fina Gabriel wa Tabata Barakuda, alipokuwa akifanya manunuzi ya mahitaji sokoni Kariakoo.
Kwa upande wa vyakula, uchunguzi wa HabariLEO umeonesha kuwa mpaka jana bei za vyakula mbalimbali zilikuwa hazijapanda. Masoko ya Mwananyamala, Ilala, Tandika, Buguruni na Kariakoo, bei ya mchele kote ilianzia Sh 1,300 kwa kilo moja hadi Sh 2,000.
Katika masoko hayo, bei ya sukari inaanzia Sh 2,600 hadi Sh 2,800 huku viazi vikiwa Sh 1,000 kwa kilo moja na Sh 4,000 kwa sado moja.
Bei ya nyama katika duka la nyama la Sayuni Kimara Mwisho ni Sh 8,000 huku duka la Asante Mungu la Mwananyamala likiuza kilo moja ya nyama Sh 7,000.
Katika Soko la Samaki la Feri, bei ya samaki haijashuka wala kupanda kwani kilo moja ya samaki inauzwa kwa Sh 7,000 huku kapu moja lenye uzito wa kuanzia kilo 18 hadi 20 likuzwa kwa mnada kuanzia Sh 130,000 hadi 150,000.
Kwa mujibu wa Hashim Amir ambaye ni muuzaji wa mnada wa Soko la Feri, samaki wanapanda bei kipindi cha upepo mkali ambacho husababisha kuadimika kwa kitoweo hicho. Lakini, alisema kipindi kama hiki, kuna samaki wa kutosha, hivyo bei inabaki palepale au kushuka.