Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mambo yaiva bandari ya Kwala

F2f2eca8 7652 41fd B3ea 30a8f75dad9b Mambo yaiva bandari ya Kwala

Wed, 22 Mar 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Bandari Kavu ya Kwala iliyopo mkoani Pwani inatarajiwa kuanza kufanya kazi muda wowote pamoja na kutoa huduma zote za kiforodha kama zinavyotolewa katika bandari zingine.

Akizungumza Meneja Miliki wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Alexander Ndibalema amesema hatua zote za ukamilishaji wa bandari hiyo zimekamilika.

“Bandari Kavu ya Kwala ipo tayari kufanya kazi kwa sababu miundombinu yote ya msingi imekamilika na leseni zingine kutoka mamlaka zingine za Serikali zimeshakamilika ambapo kinachosubiriwa kwa sasa ni kupata leseni kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),” alisema Ndibalema.

Alisema lengo kuu la kuanzishwa kwa bandari hiyo ni kuongeza ufanisi na kiasi cha shehena inayohudumiwa katika bandari ya Dar es Salaam na kupunguza msongamano katika bandari hiyo pamoja na kuongeza mapato ya Serikali kupitia huduma zitolewazo katika bandari.

Ndibalema alisema bandari kavu ya kwala ina uwezo wa kuhudumia wastani wa makasha 823 kwa siku sawa na makasha 300,395 kwa mwaka ambayo ni sawa na asilimia 30 ya makasha yote yanayohudumiwa katika Bandari ya Dar es Salaam kwa sasa.

“Tunatarajia kuwa bandari kavu ya Kwala itachangia kwa kiwango kikubwa katika Pato la Taifa kwani sehemu kubwa ya mizigo itakayohudumiwa katika bandari hiyo ni ile inayokwenda nchi Jirani,” alifafanua.

Bandari kavu ya Kwala imejengwa kwa awamu mbili zilizojumuisha usafishaji wa eneo lenye ukubwa wa kekta 60 na ujenzi wa ukuta uliogharimu zaidi ya Sh bilioni 9 ujenzi wa yadi hekta tano kiwango cha zege uliogharimu Sh bilioni zaidi ya bilioni 36, ujenzi wa reli mchepuko yenye urefu wa km 1.3 uliogharimu Sh zaidi ya milioni 600 na ujenzi wa barabara yenye urefu wa km 15.5 kwa kiwango cha zege uliogharimu zaidi ya bilioni Sh 36 ambayo imekamilika kwa asilimia 100.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live