Jukwaa la Wahariri nchini (TEF) limetoa wito kwa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kuongeza kasi katika ujenzi wa mabomba ya gesi ili kuipunguzia Serikali gharama za uagizaji wa mafuta kutoka nje nchi.
Wito huo umetolewa mkoani Dar es Salaam na Mwenyekiti wa TEF Deodatus Balile wakati wa mkutano uliowakutanisha TPDC na Wahariri wa vyombo vya habari kwa lengo la kujadili mafanikio ya shirika hilo katika utekelezaji wa majukumu yake.
"Tujenge mabomba ya gesi iwafikie watu majumbani ili kuondokana na matumizi makubwa ya fedha kupata huduma za nishati. Ukisema unachukua mkopo wa Dola Bilioni 40 kutandaza mabomba ya gesi nchi itapiga hatua kubwa kiuchumi," amesisitiza Balile.
Ameongeza kuwa hivi karibuni Rais William Ruto wa Kenya ameomba bomba la gesi lijengwe kwenda nchini humo kuwarahisishia Wananchi wa Taifa hilo kupata nishati hiyo kwa urahisi, hivyo ameishauri Serikali kuchangamkia fursa hiyo.
Balile pia ameishauri Serikali kuona uwezekano wa kujenga kiwanda cha kubadilisha mfumo wa magari ya mafuta kwenda kwenye mfumo wa gesi, kwani kufanya hivyo ni njia mojawapo ya kupanua wigo wa kukusanya mapato kupitia nishati ya gesi.