Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mambo matatu kuondoa adha ya sukari nchini

58413 Pic+sukari

Sun, 19 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa kampuni ya uzalishaji wa sukari ya Kilombero Sugar, Balozi Ami Mpungwe ameshauri mambo matatu ambayo yakifanyiwa kazi yataondoa shida ya upungufu na upatikanaji wa sukari nchini.

Mambo hayo yaliyoshauriwa na Balozi Mpungwe ni kuwepo kwa taarifa za uhakika wa takwimu za uzalishaji, viwanda kuongeza uzalishaji na kudhibiti uagizaji inapobidi kuingiza sukari itokayo nje.

Kumekuwa na nakisi kubwa ya sukari kutokana na uzalishaji mdogo unaofanywa na viwanda vya ndani ambavyo kwa miongo kadhaa vimeshindwa kukidhi mahitaji.

“Ni wazi kuwa uzalishaji haukidhi mahitaji ya soko na nakisi ni tani 120,000 hadi tani 150,000 kuna tatizo la kutokuwepo kwa takwimu sahihi ambazo zingewasaidia wawekezaji kujua kiasi halisi cha upungufu wa soko” alisema.

Kuhusu kuongeza uzalishaji alisema viwanda vya sukari vikubwa vipo vinne; Kilombero ndiyo wazalishaji wakubwa na wao uwezo wao wa mwisho ni kuzalisha tani 134,000 kwa mwaka, lakini endapo wataongeza uzalishaji nakisi hiyo itapunga.

“Kiwanda sasa kimefika uwezo wake wa mwisho, ina maana vingine vinazalisha pungufu ya hapa inaweza kuwa tani 100,000 kushuka chini hivyo ni wazi uzalishaji ni mdogo ukilinganisha na soko ndiyo maana sisi tunakusudia kuongeza uzalishaji wetu hadi kufikia tani 268,000 ifikapo mwaka 2022,” alisema.

Pia Soma

Alisema viwanda vyote vikiongeza uzalishaji kama ambavyo Kilombero wanakusudia kufanya, basi sukari itakayozalishwa itatosheleza soko na pengine hata bei ya bidhaa hiyo inaweza kupungua.

“Kwa ardhi ya Tanzania tunaweza kuwa wauzaji wakubwa wa bidhaa hiyo Afrika Mashariki, tena ni jambo la miaka michache tu (ijayo),”

“Soko la sukari ni kubwa kuliko uzalishaji wetu, kitu ambacho tunapaswa kupambana nacho hapa ni kupunguza gharama za uendeshaji tu na si jambo jingine, tuongeze ubunifu na matumizi ya teknolojia ili kuzalisha kwa bei nafuu,” alisema

Alisema “kwa sasa hakuna kiwanda kinachoshindana na kingine kwa sababu soko tu lililopo hatujalitosheleza”.

Katika suala la uagizaji wa sukari alisema ili kuwa na upatikanaji wa sukari yenye ubora wakati wote, Serikali haina budi kudhibiti uagizaji wa sukari ikiwa ni pamoja na kuvilinda viwanda vya ndani ambavyo vinazalisha sukari bora zaidi na kuwa na manufaa mengi kiuchumi.

“Udhibiti unahitajika ili uagizaji uwe wa kiwango stahiki kwa muda stahiki na kodi inayotozwa iwe stahiki ili kutoharibu ushindani sokoni na kutoruhusu soko holela,”

Alisema hata kama uagizaji utafanywa na viwanda, Serikali isimamie kiwango kinachoingizwa ili viwanda visihamie kwenye biashara ya kuagiza badala ya kuzalisha.

Chanzo: mwananchi.co.tz