Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Malori zaidi ya 250 yaliyokwama DRC yaachiwa

MALORI 1 780x470 Malori zaidi ya 250 yaliyokwama DRC yaachiwa

Thu, 26 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Hatimaye malori ya Tanzania zaidi ya 250 yanayobeba shaba yaliyokuwa yakishikiliwa Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC), yameanza kuruhusiwa kuondoka, huku baadhi yakishikiliwa kwa kudaiwa tozo ya maegesho.

Akizungumza na Mwananchi jana, Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi Madereva (Tadwu), Schubert Mbakizao alisema baadhi ya magari hayo yalianza kuondoka jana saa 12.00 asubuhi.

Siku tatu zilizopita, Tadwu ilitoa siku 14 malori hayo yaachiwe, la sivyo wangezuia magari yote kutoka Tanzania kuingia mgodini kubeba mizigo. Siku hizo zilianza kuhesabiwa Oktoba 21, mwaka huu.

Tadwu ilitoa tamko hilo baada ya Oktoba 21 magari hayo kuruhusiwa kuondoka nchini humo, lakini yakakamatwa tena mpakani mwa DRC na Zambia kwa kile kilichoelezwa migodi bado ilikuwa haijamalizana na Serikali kuhusiana na kodi.

Hata hivyo, Mbakizao alisema walioshindwa kuendelea na safari kwa sasa wanadaiwa tozo ya maegesho ya siku zote walizokaa mpakani.

Mpaka kufika jana, gari hizo zilikuwa zimefikisha siku 56 tangu zishikiliwe, japokuwa wengine walikuwa huko siku nyingi zaidi wakishughulikia vibali vya kuondoka wakakutwa na mkasa huo wa kamatakamata.

Akizungumza na gazeti hili, mmoja wa madereva hao, Kennedy Charles ambaye hajafanikiwa kuondoka alilalamikia kuzuiwa kwa sababu ya tozo ya maegesho.

Alidai wanaowadai fedha ya maegesho wanawafanyia uhuni kwa sababu ilipaswa wawe wamefanya kazi ya kuyalinda magari hayo, lakini hawajawahi kufanya hivyo tangu washikiliwe.

“Hizo hela za maegesho wanazitaka za nini wakati siku zote tulikuwa wenyewe hapa hakuna hata anayetulinda, tumeibiwa vitu vyetu, baada ya kusikia tumeruhusiwa ndio wanakuja kudai hela ya maegesho.

“Nadhani wangeongea na wamiliki wa migodi ambao ndio wametusababishia haya yote, sisi tulichofanya ni kutekeleza agizo la Serikali wapi tuegeshe magari yetu,” alisema dereva huyo.

Dereva mwingine, Fracis Mwamalongo katika maegesho ya Whesky alisema kulikuwa na magari 35, yaliyoruhusiwa kuondoka jana ni 29 ambayo nayo pia yalienda kuzuiwa mbele, lakini baada ya kuwasiliana na wenye magari waliachiwa mchana wakaendelea na safari.

“Na hata wenzetu tuliowaacha nao wametuambia wameachiwa wote wanaendelea na safari,” alisema Mwamalongo.

Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa malori wa Kati na Wadogo (Tamstoa), Chuki Shabani alisema mawakala wao nchini humo, wanaendelea kushughulikia kadhia hiyo na huenda magari yaliyosalia yakaruhusiwa kuondoka.

Mwakilishi wa Chama cha Wamiliki wa Malori Tanzania (Tatoa) DRC, Mbuya Mande aliiambia Mwananchi kuwa suala la kulipia maegesho haliepukiki, kwa kuwa ndio utaratibu kwa nchi zote na ametoa rai kwa madereva kuwasiliana na wamiliki wa magari hayo wawatumie fedha walipe ili waondoke.

“Sisi tumeshapambana kuhakikisha magari yanatoka, sasa hili la kulipia maegesho hiyo sio kazi yetu tena, wanapaswa walipe ili waruhusiwe kuondoka,” alisema Mande.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live