Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Malori kuegeshwa hovyo kunavyowatesa wakazi Dar

Malori Msd Malori kuegeshwa hovyo kunavyowatesa wakazi Dar

Mon, 5 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Adha ya malori kuegeshwa pembezoni mwa barabara jijini Dar es Salaam imekuwa mfupa mgumu kwa mamlaka husika kuitatua, ikitajwa kuwa kero kwa watumiaji wengine wa barabara hizo.

Mwananchi Digital kwa miezi miwili imefanya uchunguzi na kubaini kuwapo tatizo hilo katika maeneo kadhaa yakiwamo Tabata Mwananchi (pembezoni mwa Barabara ya Mandela), barabara kuelekea bandarini, Barabara ya Kilwa na Barabara ya Morogoro eneo la Kimara Korogwe.

Katika maeneo hayo, wananchi wanalalamika kuchelewa kwenye shughuli za kiuchumi kutokana na malori kuegeshwa hovyo.

Loading...

Loading...

Holiness Ulomi, mkazi wa Mbezi Makabe, jijini Dar es Salaam amesema malori yanayoegeshwa pembezoni mwa barabara yanasababisha foleni na kuchelewesha wananchi kwend katika shughuli zao za kila siku.

“Hilo ni tatizo hasa Barabara ya Mandela na inayotoka Kibaha, unakuta yamepaki pembeni, yanasababisha foleni kwa sababu kunakuwa hakuna alternative (njia mbadala). Kuna wakati unahisi labda wenye malori wana nguvu sana au wapo juu ya sheria,” amesema Holiness.

Amanda Emanuel, mtumiaji wa Barabara ya Kilwa amesema amewahi kupata ajali kutokana na malori kuegeshwa kando mwa barabara.

“Barabara ya Mandela hilo tatizo lipo sana na barabara ya kwenda darajani Kigamboni miaka miwili iliyopita (2022) nimewahi kupata ajali kwa sababu ya malori kupaki barabarani,” amesema.

Tatizo la malori kuegeshwa hovyo pembezoni mwa barabara limewahi pia kugonga vichwa katika mitandao ya kijamii.

Aliyewahi kuwa Meya wa Ubungo, Boniface Jacob kupitia ukurasa wake wa X (zamani Twitter) alikosoa utaratibu huo wa maegesho akishinikiza hatua zichukuliwe.

“Zamani Barabara ya Mandela ulikuwa ukipaki lori lako hata kwa dakika tano tu pembeni ya barabara basi ujue faini Sh5 milioni kwa gari moja. Sasa hivi kampuni moja peke yake inapaki malori hadi 100 barabarani saa saba mchana bila woga, wananchi wanalia kila siku,” aliandika Boniface.

Chama cha Malori

Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki Malori wa Kati na Wadogo Tanzania (Tamstoa), Chuki Shabani amesema tatizo hilo linasababishwa na kukosekana maegesho rasmi katika Jiji la Dar es Salaam ambalo ni kitovu cha biashara nchini.

“Dar es Salaam haina parking (maegesho), tatizo halipo kwetu, tumepiga kelele sana kuhusu suala la kutengewa maegesho ya malori yanayoingia na kutoka Dar es Salaam,” amesema na kuongeza:

“Tukikutana na Serikali huko kwenye vikao tunalisema hili na tayari tulishapendekeza eneo huko Kibaha (Misugusugu), lakini hatuoni utekelezaji katika hilo.”

Tanroads yatoa msimamo

Mkuu wa Idara ya Mipango wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Mkoa wa Dar es Salaam, Mhandisi Clever Akilimali amesema tatizo hilo ni kubwa na wanalisimamia kwa kuzuia vitendo hivyo na kutoa elimu.

“Kisheria huruhusiwi kupaki gari pembezoni mwa barabara sababu ni kuharibu kingo za barabara, si Tabata Mwananchi tu ndiyo inafanyika hivyo, maeneo ni mengi. Sisi Tanroads tunalisimamia hilo kwa kuwazuia na kuhakikisha tunawapa elimu,” amesema.

Mhandisi Akilimali amesema, “Pia vitendo hivi vimeongezeka zaidi pembezoni au karibu na sehemu zenye ICD (bandari kavu), miezi kadhaa iliyopita kulikuwa na changanoto hiyo, tulikaa na wakuu wa wilaya tukayatoa magari hayo.”

Mhandisi Akilimali ametoa rai kwa madereva kuacha kuegesha magari pembezoni mwa barabara kwa sababu ya usalama na kulinda ubora wa barabara.

Sheria ya Barabara ya Mwaka 2007 inasisitiza hairuhusiwi kufanya shughuli yoyote kwenye hifadhi ya barabara.

“Hifadhi ya barabara ni mahususi kwa ajili ya matumizi ya uendelezaji na upanuzi wa barabara au shughuli zozote zinazohusiana na barabara,” kinaeleza kifungu cha 29(1) cha sheria hiyo.

Loading...

Loading...

Mipango Miji

Ofisa Mipango Miji na Mhadhiri wa Chuo cha Mipango, Gerald Temu amesema tatizo hilo linasababishwa na kutokuwa na kipaumbele cha maegesho katika miji na majiji mengi wanapopanga mipango yao kabambe (masterplan).

“Tatizo hili linasababishwa na viongozi wetu wa mipango miji hawajaliweka wazi suala la maegesho ya malori, huwa kama linasahaulika. Hili ni hitaji jipya linalosukumwa na uchumi kutokana na ukuaji wa sekta ya usafirishaji,” amesema na kuongeza:

“Hii ni changamoto mpya kwa jiji kama la Dar es Salaam, hata walivyoandaa mpango kabambe wa mara ya kwanza na walivyofanya rejea sina uhakika kama walizingatia haya maeneo.”

Temu amesema kwa maeneo ambayo yanatengwa maegesho ya malori bado changamoto inabaki kuwa miundombinu si rafiki.

Kauli ya Temu inashabihiana na uhalisia wa Mpango Kabambe wa Dar es Salaam (Dar es Salaam Master Plan 2012-2032) ambao katika mapendekezo yake muhimu haukuliweka suala la maegesho ya malori.

Mapendekezo muhimu katika mpango huo wa miaka 20 ni urekebishaji wa taasisi, muundo wa Halmashauri za Dar es Salaam, mahusiano baina ya Serikali, ufadhili, ushiriki wa jamii, ufuatiliaji, kuzingatia na kutekeleza, makazi yasiyo rasmi na marekebisho ya sheria.

Malori yakiwa yameegeshwa pembeni karibu na eneo la Tabata Mwananchi. Picha na Michael Matemanga

Wachumi waeleza athari

Mchambuzi wa masuala ya uchumi, Mack Patrick amesema kuegesha malori pembezoni mwa barabara kuna athari kiuchumi kutokana na kusababisha foleni inayochelewesha watu kufanya kazi.

“Foleni inapokuwa kubwa wananchi wanachelewa kufanya kazi, hivyo uzalishaji unapungua lakini pia katika fikra za kawaida tu foleni humaliza mafuta ya gari kwa hiyo lazima maumivu yawepo,” amesema Mack.

Mack amesema Jiji la Dar es Salaam vikwazo vya uzalishaji mali vikiondolewa, tija itaonekana kwa uchumi wa Tanzania kwa ujumla kutokana na asili yake ya kuwa makutano ya kibiashara Afrika Mashariki.

Kulingana na takwimu za Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwenye ripoti ya ufanisi wa uchumi katika kila kanda iliyotolewa Oktoba 5, 2023 wastani wa kipato cha mkazi wa Jiji la Dar es Salaam lenye wakazi milioni 5.28 ni Sh5.39 milioni kwa mwaka.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live