Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Malori 250 yaliyokwama DRC yaachiwa, yazuiwa tena

Malori Yaliokwama Mpaka Wa Tanzania Kuruhusiwa Kuingia Kenya Malori 250 yaliyokwama DRC yaachiwa, yazuiwa tena

Tue, 24 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Malori 250 yanayoshikiliwa katika nchi ya Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC) kwa zaidi siku 53 kwa sababu za mgogoro wa kodi kati ya Serikali ya nchi hiyo na migodi ya madini, jana yaliachiwa kuendelea safari lakini yakazuiwa katika eneo jingine.

Malori hayo yaliyokuwa yamezuiwa katika eneo la Whesky jana yaliruhusiwa kuendelea na safari lakini yalipofika katika mji wa Kasumbalesa yakazuiwa kwa sababu ya kutokamilika kwa vibali

Wakati hali ikiwa hivyo, Chama cha Madereva (TADWU), kimetoa siku 14 kwa Serikali ya DRC kuachia magari hayo.

Msimamo huo ulitangazwa jana na Mwenyekiti wa Chama hicho, Schubert Mbakizao, alipozungumza na Mwananchi ambapo alisema siku hizo zimeanza Oktoba 21 na baada ya hapo watazuia magari yote kwenda kwenye migodi ya DRC.

Wiki iliyopita alipoulizwa kuhusiana na sakata hilo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba alisema Serikali inalishughulikia kupitia ubalozi wake wa DRC.

Naye Balozi wa Tanzania nchini Congo, Said Mshana, alisema magari yanayoshikiliwa kutokana na sakata hilo si ya Tanzania tu bali yapo ya Zambia na Afrika Kusini kwa kuwa hilo ni suala la kidiplomasia wanalishughulikiwa kwa taratibu za kidiplomasia.

Hata hivyo, alipopigiwa simu jana na kutumiwa ujumbe mfupi saa saba mchana kujua kinachoendelea hakupokea wala kujibu ujumbe.

Kauli ya Tamstoa

Mwenyekiti wa Tamstoa, Chuki Shabani, alisema taarifa za kuruhusiwa kwa malori hayo wameipata kupitia mawakala wao waliopo nchini DRC waliowatumia barua kwenye kundi lao la WhatsApp.

Alisema barua hiyo iliyoandikwa kwa lugha ya Kifaransa imetoa kibali kuruhusiwa kuondoka kwa malori hayo.

"Kutokana na barua hiyo, wakala ameomba madereva wakae kwenye magari yao kwani muda wowote huenda wakaruhusiwa, japo tunaambiwa kuna vikao vya makubaliano bado vinaendelea.

"Hii kwetu ni habari njema, kwa kuwa imetuchukua muda mrefu kutaka kukomboa mali zetu zikizokwama huko, tunaishukuru Serikali pia kwa kuwa bila wao isingewezekana kufikiwa kwa makubaliano hayo," alisema Chuki.

Naye Katibu Mkuu wa Tamstoa, Issa John aliiomba serikali kuwasamehe kodi ya makasha kwani kiutaratibu huwa wakipewa siku 45, hivyo mpaka sasa zimezidi siku hizo na kila siku hutozwa dola 60 sawa na Sh153,000 kwa siku.

Katibu huyo alishauri kuwa ili lisijirudie tukio kama hilo, ni vema serikali ya Congo na Tanzania zikakaa chini kukubaliana pindi mgodi unapodaiwa kodi yasishikilwe magari yanayosafirisha mzigo na badala yake yazuiwe tangu awali yasipakie.

“Kuzuia magari yaliyopakiwa mzigo kwa kosa la mtu mwingine si sahihi na kutuingiza hasara tusiostahili, hili lirekebishwe mapema” alisema

Dereva aliyepo nchini DRC, Kennedy Charles, alisema taarifa ya kuwa wanatoka mpakani, wametumiwa tu na wao wenye kundi lao la whatsApp na halikwenda kwao rasmi.

Dereva mwingine aliyetambulika kwa jina la Dula, alimbia Mwananchi kwa njia ya simu kuwa hawajui kama tangazo hilo lima ukweli au ala lakini wamekaa tayari kwa lolote.

Dereva Athuman Msangi, alisema ametoka eneo ambalo malori hayo yanashikilwa saa mbili baada ya kusambaa kwa tangazo hilo, lakini stika zilizokuwa zimebandikwa kuwa magari hayo yanashikiliwa bado hazijabanduliwa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live