Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Malipo ya korosho, Waziri Mkuu Tanzania atoa maagizo wizara ya kilimo

90772 Pic+korosho Malipo ya korosho, Waziri Mkuu Tanzania atoa maagizo wizara ya kilimo

Sun, 5 Jan 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Ruangwa. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Kilimo ihakikishe asilimia tatu ya wakulima wa zao la korosho waliosalia wanahakikiwa na kulipwa.

Hadi sasa zaidi ya asilimia 96 ya wakulima wa korosho waliouza korosho zao katika msimu wa 2018/2019 wameshahakikiwa na kulipwa.

Majaliwa ameyasema hayo leo Ijumaa, Januari 3, 2020 wakati alipokutana na baadhi ya wakulima wa korosho kutoka wilaya za Ruangwa, Masasi na Tandahimba mkoani Mtwara.

Baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wakulima hao, Waziri Mkuu amewataka waendelee kuwa na subira na kwamba haki yao itapatikana.

 “Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais John Pombe Magufuli ipo makini, hivyo hakuna Mtanzania yeyote atakayepoteza haki yake.”

Kadhalika, Waziri Mkuu ametoa wito kwa wanachama wa vyama vya ushirika pale watakapoona ushirika wao hauendi vizuri wasisite kutoa taarifa serikalini.

Amewaagiza wakuu wa mikoa na wilaya wawachukulie hatua viongozi wote wa vyama vya ushirika watakaoshindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Kwa upande wao, wakulima wameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kusikiliza kero zao na kuzipatia ufumbuzi na kwamba wana imani ya kulipwa madai yao.

Mmoja wa wakulima hao, Mariamu Mganda amesema anamshukuru Waziri Mkuu kwa kukubali kuwasikiliza kwani wamepata tumaini la kulipwa fedha zao.

Naye Abdulkareem Said amesema ameridhishwa na utendaji kazi wa Serikali hususan baada ya Waziri Mkuu kukubali kusikiliza kero zao.

Chanzo: mwananchi.co.tz