Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Malipo korosho pasua kichwa

95566 Korosho+pic Malipo korosho pasua kichwa

Fri, 14 Feb 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Wakati baadhi ya wakulima wa korosho wakilalamikia kutolipwa kwa msimu wa mwaka 2018/19, Naibu waziri wa Kilimo, Omary Mgumba amesema hakuna mkulima anayedai.

Akizungumza jana na Mwananchi, Mgumba alisema wakulima waliouza korosho zao kwa taasisi za Serikali mwaka 2018/19 walilipwa.

Alisema Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) walilipia kupitia Bodi ya Nafaka Mchanganyiko (CPB).

Hata hivyo, Mgumba alisema changamoto iliyojitokeza ni baadhi ya vyama vya ushirika kupeleka majina ‘hewa’.

“Ni kweli kuna baadhi ya vyama vya ushirika vilipeleka majina feki badala ya wakulima halisi. Timu ya Takukuru inafanya uchunguzi kuwabaini watu hao,” alisema.

Kamanda wa Takukuru mkoa wa Mtwara, Enock Ngailo alisema kazi ya kuwabaini wakulima feki waliolipwa inaendelea ili warejeshe fedha hizo.

Pia Soma

Advertisement
Ngailo alisema kazi hiyo inaendelea kwa kushirikiana na Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (Coasco), walioshindwa kurejesha fedha wanaanza utaratibu wa kuwapeleka mahakamani.

Alisema Sh600 milioni zimerejeshwa na wamekamilisha utaratibu wa kuwafikisha mahakamani watu 20.

Kuhusu fedha zinakopelekwa baada ya kurejeshwa, Ngailo alisema hurejeshwa akaunti ya vyama vya ushirika kwa ajili ya kulipwa wakulima.

Mmoja wa wakulima wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara, Sandali Shaini akizungumza kwa simu, alisema kuna wakulima 135 ambao wanadai zaidi ya Sh400 milioni msimu wa mwaka 2018/19.

“Tumeenda kwa mkuu wa mkoa na wilaya hatujafanikiwa kulipwa fedha zetu. Tunamuomba Rais aingilie kati kwa sababu tunajua hajui kama kuna ambao hatujalipwa,” alisema.

Naye mwenyekiti wa Chama cha Ushirika cha Likokona Amcos, Kasembe Malilo alisema wakulima 10 wa chama chake hawajalipwa.

Malilo alisema kati ya wakulima hao, sita ni wakulima waliouza kilo za korosho kati ya 200 hadi 500 na wanne walikuwa na kilo zaidi ya 1500.

Chanzo: mwananchi.co.tz