Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Malinyi wapata matumaini ujio wa NMB

23598419f26cd64370d4dd38f1cb58c2 Malinyi wapata matumaini ujio wa NMB

Fri, 28 Aug 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MKUU wa Wilaya ya Malinyi mkoani Morogoro, Mathayo Masele, amesema ujio na uzinduzi wa Benki ya NMB uliofanywa wilayani kwake utachochea ukuaji wa uchumi na maendeleo.

Meneja wa NMB Kanda ya Mashariki Dismas Prosper, amesema uzinduzi huo unakwenda sambamba na kusaidia wananchi wa Malinyi kwa kutoa mabati 135, kofia 12, misumari 76 na mbao 200 kwa ajili kukamilisha ujenzi wa Shule ya Msingi Nawigo iliyopo Malinyi.

Akizindua tawi jipya la benki hiyo lililopo wilayani Malinyi, Masele alisema ukuaji wa uchumi na maendeleo huo unatokana na kuongezeka kwa kasi ya uzalishaji wa mazao ya kilimo, mifugo pamoja na uchimbaji wa madini ya dhahabu yaliyogunduliwa hivi karibuni.

Alisema ujio wa benki hiyo ulikuwa ukisubiriwa kwa hamu kutokana na kukosekana kwa taasisi inayotoa huduma za kibenki hali iliyowalazimu wananchi kuzifuata kufuiata huduma hizo mjini Ifakara, Kilombero umbali wa takriban kilomita 160.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Wilaya huyo, NMB licha ya kusaidia kukuza uchumi, pia itawapunguzia gharama wafanyabiashara na taasisi za serikali na binafsi zilizokuwa zikitumia gharama kubwa kusafirisha fedha kutokana na kuwepo kwa matukio ya uporaji katika barabara kuu ya Malinyi – Kilombero.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi, Hawa Mposi, alisema walikuwa wakilazimika kutumia wastani wa Sh 500,000 kwenda katika Kilombero kufanya miamala ya fedha ili kutoa huduma mbalimbali kwa wananchi.

Naye mkazi wa Malinyi, Kilongozi Mohamed, alimpongeza Rais John Magufuli kwa kuwaletea benki hiyo kwa kuwa wamekuwa wakilima mpunga kwa wingi, lakini wanapopata fedha wanakumbana na changamoto ya namna ya kutunza fedha zao.

Alisema kulazimika kutafuta huduma hizo kwa takriban kilomita 160, kulikuwa kunawawezeka hatarini kutokana na kuwepo kwa matukio ya uporaji.

Kaimu Ofisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa NMB, Salie Mlay, alisema moja ya kichocheo kikubwa cha kufungua tawi hilo katika Wilaya ya Malinyi ni kutaka kuwasaidia wakulima na wafugaji kupata mikopo pamoja na elimu ya ushirika kwa kutumia mfuko wa NMB Foundation.

“Tunataka wakulima wafanye kilimo chenye tija. NMB ipo tayari kutoa mikopo kwa wakulima na wafugaji kwa hiyo tumieni fursa hiyo kubadilisha kilimo chenu ili kiwe chenye tija zaidi,” alisema Mlay.

Chanzo: habarileo.co.tz