Dar es salaam. Kampuni ya Saruji ya Dangote ni miongoni mwa kampuni kadhaa zilizopewa siku 30 na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kulipia ushuru wa forodha mizigo yao kabla mizigo hiyo haijapigwa mnada.
Agizo hilo lilitolewa na TRA kupitia tangazo lililotoka Septemba 9,2019 katika Gazeti la Daily News ambalo limeitaja kampuni ya Dangote Cement mara 19 ikitaja pia mali zilizozuiwa kuwa ni pamoja na vifaa vya kimaabara na mashine za kuzalishia saruji.
Mbali na Dangote, kampuni nyingine zilizotajwa ni pamoja na Salim Bakhresa, ambapo inapaswa kulipia bidhaa zake kama matangi, maboksi na bidhaa nyinginezo.
Wadaiwa wengine ni pamoja na Hospitali ya Kairuki, Kampuni ya simu Airtel na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
Siku hizo 30 ambazo TRA imezitoa ni kuanzia Septemba 9,2019.