Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Makusanyo ya Desemba TRA yavunja rekodi

90508 TRA+PIC Makusanyo ya Desemba TRA yavunja rekodi

Thu, 2 Jan 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Dk Edwin Mhede amesema wamefanikiwa kukusanya Sh4.972 trilioni kati ya Sh5.1 trilioni walizopanga kukusanya katika kipindi cha robo ya pili inayohusisha Oktoba, Novemba na Desemba, 2019.

Dk Mhede ameeleza hayo leo Januari Mosi, 2020 wakati akitoa ripoti kwenye mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika makao makuu ya TRA Dar es Salaam.

Amesema makusanyo hayo ni sawa na ukuaji wa asilimia 19.78 ikilinganishwa na kipindi kama hicho cha robo ya pili cha mwaka 2018/19 ambapo mamlaka hiyo ilikusanya Sh4.151 trilioni sawa na ufanisi wa asilimia 87.59, wakati lengo lilikuwa kukusanya Sh4.739trilioni.

" Makusanyo haya ni mwendelezo wa kiashiria cha wazi kwamba walipakodi na wananchi walio wengi wana uelewa na kukubali kulipa kodi. Rai yangu asiwapo mlipakodi hata mmoja ambaye atathubutu kubaki nyuma," amesema Dk Mhede.

Akizungumzia takwimu za kila mwezi, Dk Mhede amesema Oktoba walikusanya Sh1.484 trilioni, Novemba Sh1.501 trilioni na Desemba Sh1.987 trilioni akisema ni mwezi uliovunja rekodi.

"TRA kwa mara nyingine imevunja rekodi kwa kukusanya kiasi cha Sh1. 987 trilioni kwa Desemba. Mamlaka imevunja rekodi iliyoiweka Septemba (2019) ambapo ilikusanya Sh1.767 trilioni sawa asilimia 97.20, " amesema Dk Mhede.

Kamishna huyo ametumia nafasi hiyo kuwashukuru walipa kodi wote waliosababisha TRA kufikia makusanyo hayo ya kihistoria katika kipindi cha Desemba, akiwapongeza watumishi wenzake kwa kufanya kazi kama timu katika mchakato huo.

Dk Mhede amewakumbusha pia wamiliki wa majengo nchini kujitokeza kulipa kodi haraka ili kuepusha usumbufu wa kulipia mchakato huo mwishoni wa mwaka wa fedha 2019/20,

Amebainisha viwango vya nyumba za kawaida Sh10,000 wakati ghorofa Sh50,000 zilizopo kwenye majiji, manispaa na halmashauri za miji huku maghorofa yaliyopo maeneo ya halmashauri za wilaya yakilipia Sh20,000.

Chanzo: mwananchi.co.tz