Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Makusanyo kielektroniki yapaisha mapato

98efd93edc0ba3bef4437d013f12f3ef Makusanyo kielektroniki yapaisha mapato

Thu, 4 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

SERIKALI imebainisha kuongezeka makusanyo ya serikali kwa ujumla na kwa taasisi moja moja kwa kutumia Mfumo wa Kielektroniki wa Ukusanyaji Mapato ya Kodi, Maduhuli, Tozo na Huduma za Serikali (GePG).

Aidha, imemtaka kila mwananchi anayelipia huduma yoyote ya umma, ahakikishe amepewa kumbukumbu namba ya malipo na taasisi inayotoa huduma hiyo, na akiwa analipa ahakikishe amelipa kwa kutumia namba hiyo.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James aliyasema hayo jana jijini Arusha katika hotuba ya ufunguzi wa kikao kazi cha siku mbili cha wizara hiyo na wahariri wa vyombo vya habari.

Alitoa mfano huo kuwa kwa kutumia mfumo huo, makusanyo ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) yameongezeka kutoka Sh bilioni 95 kabla ya kuanza kwa mfumo hadi kufikia Sh bilioni 115 kwa mwezi baada ya kuanza kutumia mfumo huo.

Aidha, Wakala wa Vipimo (WMA) mapato yao yameongezeka kutoka Sh bilioni moja kwa mwezi kabla ya mfumo wa GePG mpaka Sh bilioni 2.5 kwa mwezi baada ya kujiunga na GePG. Pia taasisi nyingine zimepunguza gharama walizokuwa wanalipia ada za miamala ya kielektroniki inayohusu makusanyo ya fedha za umma.

Kwa mfano, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) lilikuwa likilipa zaidi ya Sh bilioni 38 kwa mwaka kwa mawakala wa kuuza umeme, lakini baada ya kufunga mfumo huo sasa hawalilipi chochote.

Katibu mkuu huyo alisema mfumo huo umeunganishwa na taasisi mbalimbali za serikali za mitaa, halmashauri, taasisi na Serikali Kuu zipatazo 670. Mchumi Mwandamizi anayesimamia mapato ya Serikali kutoka Idara ya Uchambuzi wa Sera, Neema Maregeli alibainisha kuwa mfumo wa GePG umeongeza mapato ya serikali kutoka wastani wa Sh bilioni 800 kabla ya mfumo huu hadi wastani wa Sh trilioni 2.4 kwa mwaka.

Alisema mapato hayo yamewezesha serikali kutekeleza shughuli zake mbalimbali ikiwemo kuimarisha utoaji wa huduma kwa jamii na utekelezaji wa miradi ya maendeleo. “Wizara ya Fedha na Mipango inatambua kuwa mafanikio ya mfumo huu wa GePG yanategemea sana ushiriki wa wananchi wote katika kuutumia.

Hivyo, kila mwananchi anayelipia huduma yoyote ya umma ni lazima ahakikishe kuwa amepewa “Control number” (kumbukumbu namba) na taasisi inayotoa huduma hiyo, na akiwa analipa ahakikishe amelipa kwa kutumia “control number” hiyo,” alisema Katibu Mkuu Hazina.

Katika hotuba yake iliyosomwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Richard Kwitega, James alisema mfumo huo unawezesha kukusanya fedha za umma kielektroniki, na umebuniwa na kutengenezwa na wataalamu wa ndani wa serikali. Alisema ulianzishwa mwaka 2017 kwa taasisi chache.

“Kupitia kwenu wahariri na wanahabari, ninatoa wito kwa wananchi kutumia “control number” wanapofanya miamala ya serikali kwani kwa kufanya hivyo watakuwa na uhakika kwamba fedha walizolipa ziko salama na zimekwenda moja kwa moja mikononi mwa serikali kwa ajili ya kuboresha maisha yao kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kijamii inayotekelezwa na serikali,” alisema.

Alisema tathmini ya kiutendaji mfumo wa GePG iliyofanywa na wataalamu kutoka Chuo cha Tehama cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (CoICT), Septemba mwaka jana, ilibaini kuwa mfumo huo umeongeza makusanyo ya serikali kwa ujumla na kwa taasisi moja moja. James alisema kuanzishwa na mfumo wa GePG kumeleta faida kubwa na nyingi ikiwamo kuongezeka kwa uwazi na udhibiti katika ukusanyaji wa fedha za umma na kupata taarifa sahihi na kwa wakati zinazohusu makusanyo.

Alizitaja faida nyingine ni kuwa na viwango na utaratibu unaofanana katika ukusanyaji wa fedha za umma kwa taasisi zote za umma; kuchochea ubunifu katika ukusanyaji wa fedha za serikali na sekta ya fedha kwa ujumla kwa kuweka mazingira rafiki na ya usawa kwa wakusanyaji; kutoa huduma bora na rahisi ya malipo ya fedha za umma hivyo kuchochea ongezeko la makusanyo na fedha kufika haraka katika Akaunti Kuu za Makusanyo zilizoko Benki Kuu.

“Kuwasaidia benki na mitandao ya simu kuwa na sehemu moja tu ya kuunganisha mifumo yao na mifumo ya taasisi za umma, hivyo kuzifikia taasisi za umma na kutoa huduma za kifedha kwa urahisi; kuziwezesha benki na mitandao ya simu kuwa na mazingira rafiki na ya usawa katika ukusanyaji wa fedha za umma.

“Kuzisaidia taasisi za umma kupunguza gharama zitokanazo na uwekezaji katika miundombinu ya Tehama pamoja na “Software Development” katika suala la ukusanyaji wa mapato; urahisi katika usuluhishi wa miamala na usuluhishi wa taarifa za kibenki; kupunguza gharama za miamala inayohusu ukusanyaji wa fedha za umma na kumuongezea mlipaji wa huduma za umma machaguo mengi ya njia za kulipia huduma za umma (benki za biashara zaidi ya 25, mawakala wa benki, na mitandao ya simu yote sita,” alieleza Katibu Mkuu

Chanzo: habarileo.co.tz