Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Makusanyo halmashauri nchini yaongezeka

Revenue Marketing 1024x629 Makusanyo halmashauri nchini yaongezeka

Sat, 29 Jan 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Innocent Bashungwa amesema makusanyo ya mapato ya ndani ya halmashauri katika kipindi cha miezi sita yameongezeka kwa Sh bilioni 78.9 ikilinganishwa na kipindi cha mwaka 2020 ambapo Sh bilioni 381 zilikusanywa.

Aidha, ametoa siku 14 kwa halmashauri ambazo zimekusanywa chini ya asilimia 50, hazikutoa mikopo kwa vikundi na kupeleka fedha kwenye miradi ya maendeleo kwa asilimia 100 kujieleza na kubainisha mikakati ya siku zijazo.

Bashungwa alisema hayo jana jijini hapa wakati wa taarifa za mapato na matumizi ya mapato ya ndani ya halmashauri kati ya Julai hadi Desemba mwaka 2021 na kuwa makusanyo yaliyoongezeka ni sawa na asilimia 21.

Kwa mwaka wa fedha 2021/2022, halmashauri zimepanga kukusanya Sh bilioni 863.9 kutoka kwenye vyanzo vyake vya ndani. Bajeti ya makusanyo ya mapato ya ndani ya Mamlaka za Serikali za Mitaa iliongezeka kutoka Sh bilioni 814.96 katika mwaka wa fedha 2020/2021 hadi Sh bilioni 863.9 katika mwaka wa fedha 2021/2022.

Bashungwa alisema katika kipindi cha mwezi Julai hadi Desemba, 2021, halmashauri zimekusanya Sh bilioni 460.2 ambayo ni sawa na asilimia 53 ya makisio ya mwaka, sawa na asilimia 107 ya lengo la nusu mwaka.

“Katika kipindi hiki halmashauri za wilaya za Kishapu na Longido zimeongeza jitihada katika ukusanyaji ikilinganishwa na kipindi kama hiki cha mwaka wa fedha 2020/21 ambapo zilikuwa ni halmashauri za mwisho kwa asilimia ya makusanyo.

“Pia zipo baadhi ya halmashauri ambazo katika kipindi cha Julai hadi Desemba mwaka 2021 ufanisi wa kukusanya umeshuka ukilinganisha na kipindi kama hiki cha Julai hadi Desemba mwaka 2020. Moja ya hizo ni Halmashauri ya Wilaya ya Masasi ambayo iliongoza kwa asilimia 88 na sasa imeshuka kwa asilimia 20,” alisema.

Mwenendo wa Ukusanyaji wa Mapato Bashungwa alisema uchambuzi wa taarifa kuhusu ufanisi wa halmashauri katika ukusanyaji wa mapato ya ndani, unaonyesha kuwa halmashauri 113 zimekusanya kwa asilimia 50 au zaidi ya lengo la mwaka na halmashauri 71 zimekusanya chini ya asilimia 50.

Alisema ulinganisho wa ufanisi wa ukusanyaji wa mapato ya ndani unaonesha kuwa halmashauri ya wilaya ya Hanang imeongoza katika halmashauri zote 184 kwa kukusanya asilimia 102 ya makisio yake ya mwaka, ikifuatiwa na halmashauri za wilaya za Kaliua, Shinyanga na Mlele ambazo zimekusanya kwa asilimia 91, ya lengo la mwaka.

“Hata hivyo, kuna uwezekano wa halmashauri hizi kuwa na makisio yasiyoakisi uhalisia wa uwezo wake wa ukusanyaji mapato ya ndani, hivyo kuhitaji kufanya mapitio ya bajeti ili kuongeza bajeti ya makusanyo na kuweza kuendelea kufanya matumizi ya fedha kutoka kwenye makusanyo hayo,” alisema.

Aidha alisema Halmashauri za Wilaya ya Bumbuli na Kilindi zimekuwa za mwisho kwa kukusanya asilimia 27 zikifuatiwa na Halmashauri Wilaya ya Bunda iliyokusanya asilimia 28.

Akizungumzia kigezo cha wingi wa mapato, Bashungwa alisema halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imekusanya mapato mengi zaidi kuliko halmashauri zote yanayofikia Sh bilioni 36.2 ikifuatiwa na Halmashauri ya Jiji la Dodoma iliyokuwanya Sh bilioni 26.8 na Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni Sh bilioni 24.8.

Aidha, halmashauri 13 kati ya 184 zimekusanya kuanzia Sh bilioni tano na zaidi. Bashungwa alisema mkoa wa Manyara umeongoza kwa kukusanya asilimia 69 ya lengo la mwaka, ikifuatiwa na Mkoa wa Songwe asilimia 68, Mkoa wa Njombe asilimia 64 na Ruvuma asilimia 61 huku Kilimanjaro ikiwa ya mwisho kwa kukusanya asilimia 43 ikifuatiwa na Mkoa wa Kigoma, asilimia 44 na mkoa wa Mara asilimia 45.

Makusanyo kwa halmashauri za majiji, Bashungwa alisema Jiji la Tanga limeongoza kwa kukusanya mapato kwa asilimia 56 ya makisio ya mwaka ikifuatiwa na Jiji la Arusha lililokusanya asilimia 55 huku Jiji la Mwanza likikusanya asilimia 54.

Alisema Jiji la Mbeya limekuwa la mwisho kwa kukusanya mapato kwa asilimia 45 likifuatiwa na Jiji la Dar es Salaam kwa asilimia 52 na Jiji la Dodoma kwa asilimia 53.

Kwa upande wa halmashauri za manispaa, Bashungwa alisema Halmashauri ya Manispaa ya Kahama imeongoza kwa kukusanya mapato kwa asilimia 67 ya makisio yake ya mwaka ikifuatiwa na Halmashauri ya Manispaa ya Musoma kwa asilimia 65 na Manispaa ya Ilemela kwa asilimia 55.

Katika kundi hili Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro imekuwa ya mwisho ambapo imekusanya asilimia 37 ikifuatiwa na Halmashauri za Manispaa ya Kigoma asilimia 38 na Ubungo asilimia 40.

Kwa upande wa halmashauri za miji, Bashungwa alisema Halmashauri ya Mji wa Mbulu imeongoza kwa kukusanya asilimia 83 ikifuatiwa na Halmashauri za Miji ya Tunduma kwa asilimia 79 na Njombe asilimia 73.

Alisema Halmashauri ya Mji wa Korogwe imekuwa ya mwisho kwa kukusanya asilimia 39 ya makisio yake ya mwaka ikifuatiwa na Halmashauri ya Mji ya Nzega (asilimia 42) na Halmashauri ya Mji Masasi (asilimia 42).

Bashungwa lisema kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang imeongoza kwa kukusanya asilimia 102 ikifuatiwa na Halmashauri za Wilaya ya Kaliua, Shinyanga na Mlele ambazo zimekusanya kwa asilimia 91.

Aidha, Halmashauri za Wilaya ya Bumbuli na Kilindi zimekua za mwisho katika kundi hili kwa kukusanya asilimia 27 ya makisio yake ya mwaka ikifuatiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Bunda ambayo imekusanya kwa asilimia 28 ya makisio ya mwaka.

Maagizo Bashungwa ametoa siku 14 kwa wakuu wa mikoa kuhakikisha halmashauri ambazo zimekusanya chini ya asilimia 50 ya lengo kuwasilisha maelezo kwa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoana Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kuhusu sababu za kushindwa kufikia lengo na kubainisha mikakati ya jinsi ya kuboresha mapato katika kipindi kilichosalia.

Pia ametoa siku 14 kwa halmashauri ambazo zimetumia chini ya asilimia 100 ya fedha zinazopaswa kuelekezwa kwenye miradi kutoa maelezo kwa Katibu Mkuu kuhusu sababu za kushindwa kupeleka kikamilifu fedha hizo na pia kuonyesha mikakati ya jinsi ya kutimiza malengo.

Bashungwa pia ametoa siku 14 kwa halmashauri ambazo zimetumia chini ya asilimia 100 ya kiasi kilichokusanywa kwa ajili ya asilimia 10 ya mikopo ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kuwasilisha maelezo kwa Katibu Mkuu kuhusu sababu za kushindwa kutoa fedha kwa mujibu wa sheria na kuonyesha mikakati ya jinsi ya kutimiza malengo.

Pia aliwataka wakuu wa mikoa kuhimiza halmashauri kuandaa makisio ya mapato ya ndani yenye uhalisia kulingana na fursa zilizopo kwenye halmashauri zao ikiwa ni pamoja na kuibua vyanzo vipya vya mapato ili kuongeza mapato na hatimaye kuboresha utoaji wa huduma.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live