Hati za Makubaliano ya ushirikiano katika Sekta ya Mafuta na Gesi Asilia kwa Taasisi zinazoshughulika sekta hiyo kutoka Tanzania Bara na Zanzibar zimesainiwa na hivyo kufanya ushirikiano huo kuwa rasmi.
Hafla ya utiaji saini hati hizo za Makubaliano imefanyika katika Mkoa wa Mjini Magharibi na kushuhudiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Nishati na Madini Dkt. Mngereza Miraji Mzee, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Kheri Mahimbali, Mkuu wa Wilaya ya Mjini, Rashid Msaraka ((alimwakilisha Mkuu wa Mkoa) na Meya wa Jiji la Zanzibar, Mahmoud Mussa.
Viongozi wengine waliohudhuria Hafla hiyo ni Wakuu wa Taasisi zinazosimamia Sekta ya Mafuta na Gesi kutoka Tanzania Bara na Zanzibar pamoja wenyeviti wa Bodi za Taasisi hizo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Nishati na Madini kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dkt. Mngereza Miraji Mzee, ametaja Taasisi zilizosaini makubaliano hayo kuwa ni Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na Kampuni ya Maendeleo ya Mafuta na Gesi Asilia Zanzibar (ZPDC), Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) na Mamlaka ya Udhibiti wa Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia (ZPRA) pamoja na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (ZURA).
Amesema kuwa, TPDC na ZPDC zitashirikiana katika maeneo mbalimbali ikiwemo kujenga uwezo kwa wataalamu ikiwa ni pamoja na kubadilishana wataalamu, vifaa na teknolojia katika masuala yanayohusu utafutaji Mafuta na Gesi asilia katika pande mbili za muungano, kubadilishana uzoefu katika kuchakata, kutafsiri na kutunza takwimu na taarifa mbalimbali zinazohusu utafutaji, uendelezaji na uzalishaji wa rasilimali ya mafuta na gesi asilia.
Ametaja baadhi ya makubaliano ya ushirikiano kati ya PURA na ZPRA kuwa ni kubadilishana uzoefu katika kuandaa na kutunga miongozo na kanuni mbalimbali zitakazosimamia shughuli za mkondo wa juu wa petroli; kuongeza ujuzi katika kufanya kaguzi za Mikataba ya Ugawanaji Mapato, kubadilishana uzoefu katika kusimamia utunzaji wa taarifa mbalimbali zinazohusu utafutaji, uendelezaji na uzalishaji wa rasilimali ya mafuta na gesi asilia na kushirikiana katika maeneo mengine ya ushirikiano katika eneo la mkondo wa juu wa petrol.
Aidha amesema kuwa, EWURA na ZURA zitashirikiana katika maeneo mbalimbali ikiwemo kutoa ushauri wa kitaalamu wakati wa kutayarisha nyenzo za kiudhibiti, kubadilishana uzoefu wa kiudhibiti katika maeneo ya kiufundi na kiuchumi katika sekta za Nishati na Maji ikiwemo ukokotoaji/ uandaaji wa bei/gharama za huduma na utekelezaji wake na kusaidiana katika masuala ya kiutawala, teknolojia na vitendea kazi pale panapohitajika.
Mgeni rasmi katika hafla hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Mjini, Rashid Msaraka ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi alisema kuwa, utiaji saini wa makubaliano hayo ni matokeo ya juhudi kubwa zinazofanywa na viongozi Wakuu wa pande zote mbili za Muungano pamoja na Mawaziri wanaosimamia sekta hizo ambao wameonyesha umakini katika kusimamia sekta.
Amesema kuwa, Taasisi hizo zimekuwa zikishirikiana kwa muda mrefu lakini sasa imekuwa rasmi kwenye maandishi na ni ishara ya kuendelea kutekeleza ushirikiano uliopo kwa umakini, ukaribu na mafahamiano ya karibu zaidi.
Amesema kuwa, Taasisi hizo ni za kimkakati kwenye uchumi wa pande mbili za Muungano na hivyo amesisitiza kuwa ukaribu na mafahamiano yao yaendelee kwani yataleta mafanikio makubwa.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba amesema kuwa, jambo hilo la kutia saini makubaliano ya ushirikiano katika Mafuta na Gesi Asilia lina lengo la kuboresha na kuimarisha shughuli za utafiti wa mafuta na Gesi na kwa Tanzania Bara na Zanzibar na kwa Tanzania Bara tayari Gesi imegundulika ya kiasi cha futi za ujazo zaidi ya trilioni 57 na bado kuna dalili za upatikanaji mafuta.
Kutokana na makubaliano hayo rasmi ya ushirikiano, amezipongeza Taasisi hizo kwa kufikia maamuzi hayo ambayo yatafanya malengo ya Serikali ya kuendeleza rasilimali za Mafuta na Gesi Asilia kufanyika kwa haraka na kuweza kufikia mafanikio kwa muda mfupi zaidi.