Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Makontena ya Makonda yakosa wateja

13928 MAKONTENA+PIC TanzaniaWeb

Mon, 27 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Makontena 20 yaliyo bandarini kwa jina la Paul Makonda yameshindikana kuuzwa baada ya wateja waliojitokeza kwenye mnada jana kushindwa kufika bei iliyotajwa.

Mizigo iliyokuwa kwenye makontena hayo inadaiwa kuwa ni samani za shule za Mkoa wa Dar es Salaam.

Mwananchi lililofika katika mnada huo uliofanyika eneo la bandari kavu ya Malawi Cargo jana saa sita mchana lilikuta ukikaribia kufungwa na kudokezwa kuwa samani hizo zilikosa wanunuzi.

Maofisa wa TRA waliokuwepo walikataa kuzungumzia chochote.

“Kama mnataka taarifa nendeni ofisini kwa meneja wangu,” alisema ofisa wa TRA aliyekuwa akiendesha mnada huo, ambaye hakutaka kuweka wazi jina lake.

Hata hivyo, mmoja wa maofisa waliokuwepo katika eneo hilo alimwambia mwandishi wa habari kuwa mnada umeahirishwa kwa sababu wateja waliofika wameshindwa kufika bei iliyotakiwa.

Ofisa huyo alisema mali zilizokuwemo kwenye makontena hayo ni samani za shule.

Hata hivyo, hakutaja bei iliyokuwa inatajwa na wauzaji badala yake akamtaka mwandishi awaulize maofisa wa TRA ambao hata hivyo hawakutaka kutoa taarifa.

Baada ya kuahirisha mnada huo, msafara huo ulielekea Geti Namba 2 kufanya mnada mwingine wa magari.

Mwananchi lilidokezwa kuwa baadhi ya wamiliki na viongozi wa shule za jijini Dar es Salaam walipigiwa simu kuhusu mnada huo, lakini hawakuwa tayari kuzinunua.

Akizungumza kwa simu, Makonda, ambaye ni mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam alisema hana taarifa ya kupigwa mnada kwa makontena hayo.

“Sina taarifa ya kupigwa mnada wa hivyo vifaa, mimi nipo msibani Mwanza, ila kauli yangu kwa walimu ambao ninawajali na kuwapenda, wasikate tamaa, nawapenda sana, ujumbe wangu mkubwa kwao ni wamtegemeao Mungu ni kama Mlima Sayuni hawatatikisika kamwe,” alisema Makonda.

Historia ya makontena

Tangazo la Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) lililochapishwa kwenye gazeti la Serikali la Daily News Mei 12 mwaka huu, liliwataka wamiliki wa mali zilizokaa bandarini kwa zaidi ya siku 90 kujitokeza kuzilipia.

Tangazo hilo lilionyesha kuwa TRA inakusudia kufanya mnada wa wazi mwezi Juni kwa mizigo iliyokaa bandarini kwa muda mrefu bila kukombolewa, ikiwamo ya Paul Makonda.

Kwa mujibu wa tangazo hilo lililotolewa Mei 12 na Kaimu Kamishna wa Forodha na Ushuru wa TRA, Ben Asubisye na kuchapishwa na Daily News, wamiliki walitakiwa kuitoa mizigo hiyo ndani ya siku 30 kuanzia siku ilipotangazwa.

Katika tangazo hilo lililokuwa na orodha ya makontena zaidi ya 800, jina la Paul Makonda lilijitokeza mara 20 akiwa mpokeaji wa makontena 20 yaliyopo katika bandari kavu ya DICD yakiwa na bidhaa kadhaa kama samani.

Ingawa hakukuwa na uthibitisho kuwa Makonda ndiye mwenye makontena hayo, Februari 16 mkuu huyo wa mkoa alikaririwa katika mtandao wa gazeti la Serikali la HabariLeo kuwa alipokea makontena 20 yenye samani zitakazotumika katika ofisi za walimu zinazoendelea kujengwa. Mzigo huo ulikuwa sehemu ya shehena ya makontena 36.

Samani hizo za ofisini zilizokuwa na thamani ya Sh2 bilioni, zilitolewa na Watanzania wanaoishi Marekani wanaojulikana kama Six Region Diaspora Council.

Wakati huo, alipotafutwa na Mwananchi, mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo alisema mamlaka ilitoa notisi ya siku 30 kwa waagizaji wa mizigo ambao mizigo yao imekaa bandarini kwa zaidi ya siku 90.

“Tangazo lililotolewa ni notice (taarifa) kwa wahusika ili wakomboe mizigo yao ndani ya siku 30. Isipokombolewa itanadiwa. Mizigo hiyo inaweza kuwa ni ile ambayo haijalipiwa kodi au hata ile iliyolipiwa lakini haijaondolewa,” alisema Kayombo alipozungumza na Mwananchi, Mei 17.

Alipoulizwa kama shehena hiyo ni mali binafsi ya Makonda au ya ofisi yake, Kayombo alisema: “Majina yaliyoandikwa kwenye magazeti ndiyo taarifa za consignees (wapokeaji) zilizo kwenye nyaraka. Madhumuni ya matumizi siyo sehemu ya wajibu wetu.”

Baadaye, Mei 20 ilisambaa barua ya TRA, ikionyesha kuwa makontena ya Paul Makonda yana thamani ya Sh1.4 bilioni.

Barua hiyo iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii ilieleza kuwepo kwa ombi la msamaha wa kodi wa mali hizo kutoka kwa Makonda kwenda kwa Waziri wa Fedha, Philip Mpango, maombi ambayo hayastahili kuridhiwa, kwa mujibu wa Sheria ya Kodi.

Kadhalika, barua hiyo ambayo si Mamlaka ya Mapato (TRA) wala Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango waliothibitisha kuitambua, iliandikwa na mamlaka hiyo ya ukusanyaji kodi kumueleza waziri husika kuwa ombi hilo haliwezekani kwa kuwa ofisi ya mkuu wa mkoa haina sifa ya kupata msamaha kwa mujibu wa sheria.

“Baada ya kupitia maombi hayo, tunapenda kukufahamisha kuwa sheria ya forodha ya Jumuia ya Afrika Mashariki ya 2004 na sheria ya kodi ya ongezeko la thamani (VAT) ya mwaka 2014 hazijatoa msamaha wa kulipa ushuru wa forodha na VAT kwa Serikali Kuu na Serikali za Mitaa,” ilieleza barua hiyo.

Ilieleza kuwa kutokana na sheria hiyo, ofisi ya mkuu wa mkoa ni sehemu ya Serikali za Mitaa na hivyo haistahili kupata msamaha.

Barua hiyo ilitaja kiwango cha thamani ya mali hizo, ikirejea ombi la msamaha wa kodi lililowasilishwa na ofisi hiyo ya mkoa.

Kabla ya figisu hizo za msamaha wa kodi na tangazo la TRA, Februari mwaka huu, RC Makonda aliwapeleka baadhi ya walimu wa jijini Dar es Salaam, waandishi wa habari na wadau wengine kwenda bandarini ambako aliwaonyesha makontena yenye vifaa vya ofisi na vya kufundishia, akisema vimetolewa na Watanzania waishio Marekani.

Hata hivyo, vifaa hivyo ambavyo baadhi ni viti, meza na mbao za kuandikia, vilionekana ndani ya makontena vikiwa vimeshaunganishwa, tofauti na hali ya kawaida ya kusafirisha bidhaa zikiwa hazijaunganishwa ili kuziweka nyingi kwenye kontena moja kwa ajili ya nafasi.

Chanzo: mwananchi.co.tz