Dar es Salaam. Kwa mara ya tatu mfululizo mnada wa makontena 20 yaliyoagizwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda umefanyika bila mafanikio, baada ya wateja kushindwa kufika bei.
Mnada huo umefanyika leo Jumamosi Septemba 8, 2018 katika bandari ya kavu ya DICB, jijini Dar es Salaam.
Wakizungumza baada ya mnada kumalizika bila makontena hayo kununuliwa, wateja waliojitokeza wamesema bei iliyowekwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ni kubwa kwa kuwa wanajua thamani ya samani zilizomo katika makontena hayo.
Jimmy Cosmas amesema kontena moja halizidi Sh30 milioni lakini TRA wanauza kontena moja kwa Sh60milioni.
"Wanunuzi wapo wakishusha bei yatanunulika. Mimi ninafanya biashara najua kwa bei hiyo waliyopewa wasitegemee kuuza" amesema Jimmy.
Mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya udalali ya Yono, Scolastica Kivela amesema wanatekeleza jukumu walilokabidhiwa na kwamba wanasubiri maelekezo mengine ya TRA kujua nini cha kufanya.
“Kama mnavyoona samani hazijanunulika wateja wamejitokeza ila bei wanayoishia ni Sh20milioni hadi Sh30milioni, tunasubiri maelezo mengine ya TRA,” amesema.
Soma Zaidi:
·Makontena 10 ya Makonda yazua utata mpya mnadani
Mali makontena ya Makonda zaanza kupigwa mnada