Licha ya kuongezeka kwa watumiaji wa simu za mkononi na kuenea kwa matumizi ya intaneti nchini, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeainisha changamoto zinazosababisha Watanzania wengi wasijiunge katika huduma za fedha za kidijitali.
Shirika linalohusiana na masuala ya kifedha la AFI, katika tovuti yake limetafsiri huduma za kifedha kidijitali kuwa ni zile zinazotumia teknolojia ya kidijitali katika kutunza, kupokea, kutuma na kukopesha fedha.
Ripoti ya utafiti wa BoT iliyoitwa ‘Ripoti ya mwaka ya mifumo ya malipo 2022’ imeshauri ili Tanzania inufaike na huduma hizo, watoa huduma wanapaswa kuhakikisha wanapunguza makato na tozo.
“Benki Kuu ya Tanzania inapendekeza makato na tozo katika huduma za fedha kidijitali zipunguzwe, kuwa na mfumo madhubuti wa kuzuia wizi wa mitandaoni na utapeli, itolewe elimu ya uelewa kuhusu hatari zinazoweza kutokea katika huduma ya kifedha ya kidijitali,” imeshauri ripoti hiyo.
Pia, BoT imewashauri watoa huduma hizo kuhakikisha usajili wa watumiaji unafanywa kwa wenye namba za kitambulisho cha Taifa na wachukuliwe alama za vidole na kufanya marejeo ya huduma zao kwa ajili ya kuzirahisisha.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo malipo kwa mitandao ya simu yanaongoza kwa asilimia 52 miongoni mwa njia za kidijitali za fedha zinazotumiwa na Watanzania.
Njia nyingine ni ATM kwa asilimia 25 ikifuatiwa na simu benki (asilimia 22), POS (asilimia 16), msimbo wa QR (asilimia saba), benki kwa njia ya intaneti (asilimia sita) na malipo ya kuvuka mpaka (asilimia nne).
Utafiti huo wa BoT uliofanyika katika mikoa ya Arusha, Tanga, Pwani na Zanzibar umebaini idadi kubwa ya watu wanachagua mfumo husika wa malipo ya kidijitali kutokana na unafuu wa gharama zinazotozwa, huku sababu nyingine ikiwa ni usalama wa huduma.
“Sababu mbalimbali zilibainika kuchangia matumizi ya mtu katika mfumo husika ikiongozwa na kigezo cha unafuu wa gharama, asilimia 86 wanaotumia huduma hizo hukizingatia,” imeeleza ripoti.
Usalama wa huduma (asilimia 80), kiwango cha uelewa (asilimia75), upatikanaji wa huduma husika (asilimia 66), uwazi wa taarifa (asilimia 52), ubora wa huduma (asilimia 48), matumizi rahisi ya huduma (asilimia 41) na ueneaji wa huduma (asilimia 39).
Mbali na kuwapo vikwazo hivyo katika huduma hizo, bado idadi ya watoa huduma nchini imeongezeka mwaka 2022 ikilinganishwa na mwaka 2021.
“Mwaka 2021 kulikuwa na watoa huduma 59 wameongezeka hadi 71 mwaka 2022. Kati ya hizo 44 zilikuwa benki na 27 hazikuwa benki,” imesema ripoti hiyo.
Ripoti ya BoT imezitaja kampuni tano ambazo si benki, lakini zimepewa leseni ya kutoa huduma za kifedha kidijitali kuwa ni Virtual Pay (TZ) Limited, Digicash (T) Limited, Pesapal Tanzania Limited, Simba Money Limited na Smartx Limited.
Kuhusu huduma za fedha kidijitali, mchumi Mack Patrick amesema hatua ya watoa huduma wa fedha kidijitali kuongezeka inaashiria pia watumiaji wameongezeka, jambo linalochagiza uchumi wa nchi huku akitoa rai kuondolewe vikwazo.
“Dunia yote hivi sasa inazungumzia uchumi wa kidijitali na huko ndiko ‘future’ ilipo, ukiona watoa huduma wameongezeka ujue uhitaji nao upo juu, kitu cha msingi ni kuondoa vikwazo visivyo na lazima katika huduma hizi,” amesema.
“Kama kuna kitu kinawazuia Watanzania kutumia huduma hizi kitatuliwe kwa sababu huko ndiko mzunguko mkubwa wa fedha ulipo kwa sasa,” amesema.
Kwa upande wake, Rahma Mgaza ambaye pia ni mchumi, amesema vikwazo hivyo vinatakiwa kuondolewa, ili watumiaji wa huduma hizo kidijitali wawe huru kutumia.
“Moja kati ya vikwazo naungana na BoT ni kuwapo kwa utapeli na kupotea fedha, jambo ambalo bado halijatatuliwa kwa kiwango kikubwa. Hii inaweza ikawafanya watumiaji wa huduma hizi wasiwe huru. Huduma yoyote hasa ya kifedha, ili mtu aitumie vizuri lazima ahakikishiwe usalama wa fedha zake,” amesema Rahma.
Katika hatua nyingine, ripoti hiyo iliyotolewa Februari 5, 2024 inaonyesha thamani ya miamala katika huduma za fedha za mitandao ya simu imeshuka huku miamala ya huduma za simu benki ikipaa mwaka 2022 ikilinganishwa na mwaka 2021.
“Mwaka 2021 miamala katika mitandao ya simu ilikuwa na thamani ya Sh115.2 trilioni ilipungua hadi Sh114.3 trilioni mwaka 2022. Miamala ya simu benki thamani yake iliongezeka kutoka Sh24.9 trilioni mwaka 2021 hadi Sh30.6 trilioni mwaka 2022 sawa na ongezeko la asilimia 22.7,” imeeleza ripoti hiyo.
Takwimu hizo zinaendana na maoni ya mchumi mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Abel Kinyondo aliyesema kupungua kwa wastani wa miamala kunatokana na sababu nyingi ikiwamo tozo.
“Miamala ni sehemu ya kipato na mzunguko wa fedha (velocity of money), katika kipindi ambacho wastani wa idadi ya miamala unapungua utagundua ni wakati ambao tozo ziliwekwa na pia kulikuwa na vita vya Ukraine na Russia na athari za ugonjwa wa Uviko-19,” amesema Profesa Kinyondo alipozungumza na Mwananchi Digital Januari 23, 2024.