Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Makandarasi waiomba Serikali iwashike mkono

Wakandarasii Ujenzi.png Makandarasi waiomba Serikali iwashike mkono

Mon, 11 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Makandarasi na watoa huduma wameiomba Serikali iwaruhusu kulipa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) baada ya kuikusanya kutoka kwa mlipaji badala ya utaratibu wa sasa unaowataka kulipa baada ya kupeleka hati ya madai kwa mwenye kazi.

Wamesema malipo ya makandarasi yamekuwa yakichukua muda mrefu hadi miaka miwili, huku masuala ya kikodi yakiwarudisha nyuma na kupendekeza suala la malipo lisiwe la kimkataba tu bali liwe la kisheria ili kusaidia mwenye kazi kutoingia mkataba ikiwa hana fedha.

Rai hiyo imetolewa jana, Jumapili Desemba 10, 2023 wakati wa uzinduzi wa Chama cha Umoja wa Makandarasi na Watoa Huduma Tanzania (Tucasa), ambapo Mwenyekiti wa chama hicho, Samuel Marwa, amependekeza kuanzishwa kwa ‘payment guarantee’ ili uhakika wa malipo uwepo na miradi ikamilike kwa muda na kwa gharama nafuu.

“Malipo ni kipengele cha lazima katika kukua kwa mkandarasi, hatuwezi kusema tunakuza wazawa ikiwa hatutaweka mikakati ya kuwalipa kwa wakati.

“VAT ni eneo la kuliangalia upya hususan kwenye biashara ya ukandarasi maana ni tofauti na biashara ya kuuza bidhaa. Ukimkata mkandarasi VAT kabla hajalipwa unazidi kumpunguzia nguvu ya kuendelea kufanya kazi,” amesema Marwa.

Mwenyekiti huyo pia ameshauri watoa kazi wasilazimishe dhamana za benki badala yake waache mkandarasi achague kama ni benki au bima na kuingizwa kwenye mikataba ya umma.

Amesema vigezo vya zabuni vinavyotolewa ili kupata kazi ni kikwazo kikubwa katika ukuaji wa mkandarasi wa ndani na kutaka vipitiwe upya.

Naye Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi, Ludovick Nduhiye ambaye alimwakilisha Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, amesema kila mwezi Serikali inatenga Sh70 bilioni kulipa madeni ya makandarasi huku Sh50 bilioni zikielekezwa kwa makandarasi wazawa na kuwahakikishia kuwa hadi mwishoni mwa 2023 itamaliza madeni yote ya muda mrefu.

“Tunadaiwa karibu Sh600 bilioni lakini kipaumbele tumekilekeza kwa makandarasi wazawa, hakikisheni mnafanya kazi kwa umahiri na uaminifu ili kuleta tija katika miradi mnayokabidhiwa.

“Chunguzaneni ili kuhakikisha mnadhibiti wanaochafua jina la makandarasi wazawa kwa kazi zao kuwa duni na mkipewa miradi mtembee pamoja na epukeni vishawishi wakati wa kupata mradi hasa rushwa,” amesema Nduhiye.

Amesema Sh600 bilioni zilizotengwa kwa ajili ya kukarabati na kutengeneza barabara zitaelekezwa kwa makandarasi wazawa wakati katika miradi minne ya barabara ambayo kila mmoja una urefu wa kilomita 50 utaelekezwa kwa makandarasi wazawa ambapo makandarasi wanawake watapewa kilomita 20 kila mradi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live