Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Makandarasi 50 kujenga vyuo vya Veta nchini

Waziri Mkenda Ahimiza Ujenzi Wa Veta Wilaya 62 Kuanza Januari 2023 Makandarasi 50 kujenga vyuo vya Veta nchini

Wed, 11 Jan 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Siku chache baada ya Serikali kuagiza ujenzi wa Vyuo vya Ufundi Stadi (VETA) katika Wilaya 62 hapa nchini, tayari Makandarasi zaidi ya 50 wamejitokeza kwa ajili ya kuomba kufanya shughuli hiyo.

Hayo yameelezwa jana Januari 10, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda wakati alipofanya ziara ya kukagua maandalizi ya ujenzi wa chuo cha Veta Wilaya Mwanga mkoani Kilimanjaro, ambapo ameipongeza wilaya hiyo kwa kutoa ekari 50 kwa ajili ya ujenzi wa chuo hicho.

"Rais aliagiza kila wilaya tujenge chuo cha Veta na tuliomba wilaya zote zitutengee maeneo kwa ajili ya ujenzi wa vyuo vyetu hivi na watusaidie tupate hati miliki ya maeneo hayo na tayari wilaya ya Mwanga imefanya vizuri na wametupatia eneo la ekari 50 kwa ajili ya ujenzi wa chuo cha Veta na kazi ya ujenzi itaanza mara moja," amesema.

Amesema hatua hiyo ni ya kupongeza na kwamba tayari makandarasi wa kutekeleza agizo hilo wameshapatikana.

"Tumeshaita Wakandarasi na mpaka sasa tumepata makandarasi 50 waliojitokeza, tunaangalia wameweka gharama kiasi gani na sisi tutaangalia ni sehemu gani ya kutumia wakandarasi au kutumia 'Force Account.”

Hata hivyo, alisema majina ya makandarasi na kampuni zao nchi nzima, yatatangazwa baadae baada ya mchakato wa ndani kukamilika.

Amesema kwa kuwa ujenzi huo hauwezi kukamilika ndani ya mwaka mmoja, fedha zilizopatikana mwaka huu zitaanza kazi halafu mwakani wataomba fedha nyingine kwa ajili ya ujenzi huo.

Serikali kupitia bajeti yake ya mwaka 2022/23 imetenga jumla ya Sh100 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa vyuo hivyo kwa Wilaya ambazo zilikuwa hazijajengewa vyuo hivyo vya ufundi stadi.

Desemba 21, mwaka 2022, Profesa Mkenda aliiagiza menejimenti ya VETA kuhakikisha ujenzi wa vyuo hivyo uwe umeanza mwishoni mwa Mwezi Januari mwaka huu.

Naye, Mbunge wa Mwanga, Joseph Thadayo amesema kukamilika kwa mradi huo katika wilaya hiyo kutatoa fursa kwa vijana ambao hawajapata fursa ya kwenda vyuo vikuu kujiunga na chuo hicho na pia kuchochea maendeleo katika eneo kunakojengwa chuo hicho.

"Tunaomba kazi hii ianze mapema sana maana tumeshatoa eneo na hatimiliki ya eneo tunayo ya ekari 50, katika vitu ambavyo wilaya hii ya Mwanga inavisubiri ni miradi mitano ya kimkakati ambapo huu ni mmoja wapo," amesema.

Amesema katika nchi ambazo uchumi wake umekuwa sana ni kwamba walitumia zaidi vyuo hivyo vya kati na kuweza kupata watu kufanya kazi kwenye viwanda hivyo ambapo ilileta matokeo ya moja kwa moja kwenye uchumi.

Agnes Mdee, mmoja wa wananchi wa wilaya hiyo, ameishukuru serikali kwa kuwa na wazo hilo na kusema itawapa fursa vijana kujiendeleza pale wanaposhindwa kuendelea na vyuo vikuu hapa nchini.

"Tunaishukuru serikali kwa kutufikiria kuwa na ujenzi wa VETA hapa kwetu Mwanga, kwa kweli hili ni jambo jema sana kwasababu vijana wetu wanaomaliza shule na kushindwa kuendelea na masomo ya ngazi za juu watapata mahali pakupatia ujuzi kupitia chuo hiki," amesema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live