Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa wazalishaji wa viwandani hapa nchini kufanya jitihada na kuongeza thamani ya bidhaa ghafi zinazopatikana hapa nchini ili kuondokana na nchi kupata mapato kidogo ya fedha za kigeni na kupoteza ajira za idadi kubwa ya watu nchini.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Hafla ya Utoaji Tuzo za Rais za Wazalishaji Bora viwandani zilizofanyika katika ukumbi wa Serena Jijini Dar es salaam leo tarehe 18 Novemba 2022.
Amesema takribani asilimia 12 ya fedha za mauzo nje ya nchi (export earnings) zinatumika kulipia uagizaji wa bidhaa za walaji (consumer goods) ambazo nyingi zinaweza kuzalishwa hapa nchini na kukidhi mahitaji ya ndani na hivyo kupunguza upotevu wa rasilimali ya fedha za kigeni.
Aidha Makamu wa Rais amesema Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuboresha mazingira ya kufanya biashara na uwekezaji hapa nchini ikiwemo kufanya maboresho zaidi ya kitaasisi, sheria, sera za fedha na bajeti ambapo hadi sasa zaidi ya kodi na tozo 230 zisizo na tija zimefutwa na takribani sheria na miongozo 40 imeboreshwa na majukumu ya baadhi ya taasisi yameendelea kuboreshwa ili kuongeza ufanisi.
Katika kuhakikisha biashara inaendelea kukua nchini, Makamu wa Rais amesema serikali imeendelea kuboresha na kuongeza ufanisi wa Bandari, kuboresha sekta ya Nishati pamoja na Miundombinu ikiwemo nia ya kuiunganisha reli ya kisasa ya SGR na nchi jirani kama Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ili kuchochea biashara ya kikanda na kuwezesha Taifa kunufaika na huduma na usafirishaji wa madini na bidhaa mbalimbali kutoka katika nchi hizo.
Pia Makamu wa Rais amesema Serikali kwa kushirikisha wadau inaendelea kushughulikia changamoto ya tozo kubwa ya stempu za kielotroniki kwa lengo la kuhakikisha huduma hiyo inatolewa kwa gharama ndogo zaidi.
Aidha amesema serikali imeboresha mkakati wa kusimamia madeni ya wazabuni na inaendelea kulipa malimbikizo ya madai ya waliotoa huduma Serikalini ambapo kwa kipindi cha Julai – Oktoba 2022 pekee, zaidi ya shilingi bilioni 420 zimeshalipwa huku ikipunguza kwa asilimia 74 madeni ya ushuru wa forodha wa ziada kwa waingizaji wa sukari ya viwandani na asilimia 32 ya deni la Ongezeko la Thamani (VAT refunds).
Halikadhalika Makamu wa Rais ametoa wito kwa shirikisho la viwanda hapa nchini (CTI) kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais - Mazingira,Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara kupitia kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuchangamkia fursa na rasilimali za kimataifa katika kulinda mazingira ikiwemo Green Climate Fund na kuibua miradi ya utunzaji wa mazingira kama vile utengenezaji wa nishati mbadala pamoja na viwanda vya kuchakata taka ngumu.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Exaud Kigahe amesema Wizara itaendelea kushughulikia changamoto mbalimbali zinazowakabili wazalishaji wa viwandani ili kuwezesha uzalishaji wa bidhaa bora zenye tija na gharama nafuu. Amesema tuzo hizo ni chachu kwa wazalishaji katika kuongeza ubora wa bidhaa wanazozalisha ili ziweze kushindana katika soko la ndani na nje ya nchi.
Awali Mwenyekiti wa shirikisho la viwanda nchini Paul Makanza ameipongeza serikali kwa kutatua baadhi ya changamoto zilizowakabili wazalishaji wa viwandani kwa muda mrefu ikiwemo kuharakishwa kwa upatikanaji wa vibali vya kazi kwa wataalamu kutoka nje, kuboresha sera ya uwekezaji nchini, kufuta kodi za ziada kwa waagizaji wa sukari ya viwandani kutoka nje ya nchi pamoja na kuondoa vikwazo 54 kati ya 68 vya kibiashara baina ya Tanzania na nchi ya Kenya.
Makaza ameiomba serikali kuendelea kushughulikia changamoto mbalimbali zilizobaki ikiwemo kuongeza ufanisi wa utoaji mizigo bandarini.