Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Makamu wa Rais Zanzibar atoa siku 10 kuangamiza bidhaa zilizopita muda

Bidhaaa Madumu ya Mafuta

Fri, 20 Aug 2021 Chanzo: ippmedia.com

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, ametoa muda wa siku 10 kuangamiza au kurejesha zilipotoka bidhaa zilizopitwa na wakati.

Hemed ametoa agizo hilo wakati alipofanya ziara ya kushtukiza katika Bandari ya Malindi Jijini Zanzibar.

Makamu wa Pili wa Rais alitembelea ghala lililohifadhiwa mafuta lainishi ambayo yaliingizwa nchini mwaka 2019 kutoka Dubai na kukosa kiwango kwa matumizi ya vyombo vya usafiri.

Alisema ni vyema wizara ikahakikisha Zanzibar haipokei bidhaa zilizopitwa na wakati kwa usalama wa wananchi wake, pamoja na kuitaka Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda kuchukua hatua kali kwa wafanyabiashara wanaoingiza bidha zilizopitwa na wakati ili iwe fundisho kwa wafanyabiashara wengine.

“Zanzibar sio sehemu ya kuja kutupa bidhaa zisizo salama, naitaka Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda kuhakikisha inachukua hatua kali kwa wahusika wanaoleta bidhaa hizo kwa kufuata sheria na taratibu,” alisema.

Katika ziara hiyo Hemed alikagua mchele aina ya Asha Kuku, ulioletwa na kampuni ya A.R.Y ulioingia Zanzibar Julai 11, mwaka huu na mchele ulioletwa na I.A Siwje Traders ulioingia Juni 30, mwaka huu, ukiwa ni jumla ya kontena 10 sawa na tani 260.

Aliitaka Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu wa Uchumi Zanzibar (ZAECA), kumaliza kesi ya mchele wa I.A Siwji Trader na kampuni hiyo imeashiria kutenda vitendo vya uhujumu uchumi kwa kutoa rushwa ili kuhalalisha bidhaa yake iliyokwishapitwa na muda.

Akitoa taarifa kuhusu bidhaa ya mafuta lainishi, Kaimu Mkurugenzi Mamlaka ya Viwango Zanzibar (ZBS), Muhamed Mwalim Simai, alisema bidhaa hiyo ilikaguliwa na TBS na kukataliwa na hatimaye mhusika huyo kuhamishia Zanzibar bidhaa hiyo na ZBS imeizuiia kuingia sokoni.

Kwa upande wake Mkuu wa usajili na tathmini ya chakula kutoka Taasisi ya Udhibiti wa Dawa na Chakula (ZFDA), Khadija Ali Sheha, alisema mchele ulioingizwa Zanzibar kutoka kampuni hizo umeshafanyiwa vipimo na kuonekana kupitwa na wakati na kugundulika kuwa haufai kwa matumizi ya binadamu na mamlaka yao imetoa maelekezo kwa wahusiku kuchukua hatua zaidi.

Wakati huo huo, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alitembelea gati kuu ya Malindi na kutoridhishwa na mandhari ya eneo hilo kutokana na uchakavu wa miundombinu.

Katika kulipatia ufumbuzi tatizo hilo la miundombinu Makamu wa Pili amempa muda wa wiki moja Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bandari kuhakikisha maeneo yote yalio na hitilafu kwa usalama wa wananchi yanafanyiwa marekebisho.

“Naomba mfahamu kuwa Bandari hii ndio uso wa Zanzibar yetu haifurahishi bandari yetu kuwa katika mandhari kama hii isiyoridhisha,” alisema Hemed.

Pia alikagua eneo la kupumzikia abiria, Ofisi ya Uhamiaji, ofisi ya wakaguzi wa afya na kutoridhishwa na mazingira ya maeneo hayo.

Chanzo: ippmedia.com